Mjukuu wa Mangi Meli afanyiwa vipimo vya kinasaba DNA ili kutafuta fuvu la babu yake na Mtemi wa Wachaga nchini Ujerumani

Mangi Meli na wakeze Haki miliki ya picha SLUB/Deutsche Fotothek
Image caption Mangi Meli (kushoto) pichani na wake zake alinyongwa na Wajerumani mwaka 1900

Mjukuu wa Mangi Meli, amefanyiwa vipimo vya kinasaba vitakavyosaidia kusaka fuvu la chifu huyo aliyenyongwa na wakoloni wa Kijerumani mwaka 1900.

Mangi Meli alinyongwa baada ya kuongoza mapambano dhidi ya utawala wa kikoloni na baadae kichwa chake kukatwa na kupelekwa Ujerumani.

Fuvu lake yawezekana kuwa ni moja kati ya mafuvu mengi yaliyopo kwenye makumbusho moja kubwa jijini Berlin.

Wanaharakati wanataka fuvu hilo lirejeshwe ili lipate mazishi ya heshima anayostahili kama shujaa nyumbani kwao Moshi, kaskazini ya Tanzania.

Isaria Meli, mwenye miaka 87 ni mjukuu wa Chifu huyo wa jamii ya Wachaga amezitaka serikali za Tanzania na Ujerumani kushirikiana ili kuwezesha kupatikana na kurejeshwa kwa fuvu hilo.

Haki miliki ya picha Konradin Kunze
Image caption Isaria Meli, 87, ni mjukuu wa Mangi Meli na anatamani kuona fuvu la babu yake likirudishwa.

Isaria alifanyiwa vipimo vya DNA jijini Berlin baada ya kukaribishwa na Wakfu wa Urithi wa Utamaduni wa Prussia (maarufu kama SPK) ambao unahifadhi mabaki ya mafuvu yalichukuliwa na wakoloni wa Kijerumani.

SPK tayari imeorodhesha mafuvu sita ambayo yanaaminika kutokea Moshi na yalihifadhiwa katika kipindi ambacho Chifu huyo aliuawa. Mafuvu yote hayo yameandikwa "Dschagga/Wadschagga" ikimaanisha Wachaga, ambalo ndilo kabila la Mangi Meli.

Watafiti wataangalia kama vinasaba vya DNA vya Isaria vitaendana na moja ya mafuvu hayo. Majibu yanatarajiwa kupatikana ndani ya miezi sita ya mwanzo ya mwaka ujao, 2019.

Ujerumani na mafuvu kutoka Afrika

Mwanzoni mwa karne iliyopita, maelfu ya mafuvu kutoka makoloni ya Mjerumani ya Afrika yalipelekwa Berlin. Mafuvu hayo yalikuwa ni sehemu ya utafiti wa kibaguzi ambao hivi sasa unalaaniwa.

Baada ya kupitia katika mikono tofauti ya umiliki, mafuvu hayo 5,500 ikiwemo 200 kutoka Tanzania yalikabidhiwa kwa SPK mwaka 2011.

Wakfu huo sasa unachunguza sehemu hasa mafuvu hayo yalipotokea.

Mpaka sasa bado ni kitendawili kujua hasa ni nini kilitokea kwa fuvu la Mangi Meli ambalo limepotea.

Haki miliki ya picha SLUB / Deutsche Fotothek
Image caption Mangi Meli ni shujaa kwa watu wake kwa kupambana na utawala wa kikoloni wa Kijerumani

Ukiachana na harakati za mjukuu huyo, Mtanzania mwengine, Mnyaka Sururu Mboro amekuwa katika harakati za kulisaka fuvu hilo kwa miaka 40 sasa.

Amesema ni muhimu kwake "kulirudisha fuvu hilo kwa watu wake ambao bado wanahuzunika na kifo cha Mtemi wao."

Hata hivyo baadhi ya wanaharakati wanamatumaini madogo juu ya kufanikiwa kwa kipimo hicho cha DNA.

Mafuvu sita yanayotarajiwa kufanyiwa vipimo yalipelekwa Ujerumani na Luteni Kanali Moritz Merker ambaye aliuwa moja ya maafisa wakuu wa jeshi la Wajerumani mjini Moshi wakati Mangi Meli akinyongwa, mwanaharakati Konradin Kunze ameiambia BBC.

Lakini Kanali Merker hakusema kama ana fuvu lolote la Chifu katika rekodi zake, ameongeza Kunze.

Isaria Meli amejiandaa pia kupokea habari za kuwa hakuna fuvu lililoendana na vinasaba vyake lakini anaimani kuwa fuvu la babu yake litapatiikana akiwa bado yu hai.

Mada zinazohusiana