Watu waliojihami wamteka mfanyakazi wa shirika la misaada pwani ya Kenya

RAMANI

Kundi la watu wasiojulikana waliojihami wamemteka mwanamke mfanyakazi wa shirika la misaada, raia wa Italia kutoka kusini mashariki mwa Kenya, Polisi inasema.

Wanaume hao wanaoarifiwa kujihami kwa bunduki, "wamefyetua risasi kiholela" kabla ya kumteka msaidizi huyo mwenye umri wa miaka 23 nje ya mji wa pwani Malindi.

Watu watano pia wanaarifiwa kujeruhiwa na wamepelekwa hospitalini, mmoja kati yao akiwa yuko katika hali mahututi.

Haijajulikana wazi ni kwanini shambulio hilo limetokea na waliolitekeleza ni akina nani, polisi wanasema.

Hatahivyo, polisi imeeleza kwamba wanalichukulia tukio hilo, lililotokea mwendo wa saa mbili Jumanne usiku kama la kigaidi.

Katika ujumbe kwenye Twitter, idara ya Polisi nchini imesema wanaume hao walikuwa wamebebea bunduki aina ya AK47 walizozitumia kulivamia jumba la kibiashara la Chakama katika kaunti ya Kilifi pwani ya Kenya nje kidogo ya mji wa Malindi.

Polisi kwa sasa wametawanywa kuwasaka wahalifu hao.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii