Kwanini watoto mapacha ni laana kwa Wakara Tanzania

Pacha Haki miliki ya picha Jenny Matthews

Jamii ya wakara kutoka katika kisiwa cha ukara mkoani Mwanza Tanzania wanaamini kuwa kuzaa watoto mapacha sio jambo la Kawaida.

Kwa hivyo watoto hao wakizaliwa kuna utaratibu wa kijamii unapaswa kufuatwa.

Utaratibu unaofatwa ni mwanamke aliyezaa mapacha anatakiwa afanye tendo la ndoa na mumewe baada tuu ya kujifungua.

Inaweza kuwa baada ya siku chache tu, baada ya hapo watoto sasa wanachukuliwa kuwa miongoni mwa watoto wa kawaida.

Kabla mwanamke aliyejifungua kufanya utaratibu huo, hawezi kwenda hata nyumba ya jirani wala kutumia vyombo na watu wengine ndani ya nyumba anayokaa.

Hii pia ni hivyo hivyo kwa watu walisaidia wakati wa kujifungua na wakunga waliomzalisha mama aliyezaa mapacha, Wanapaswa kusubiri afanye tendo la ndoa na mumewe kisha wao ndio waweze kuendelea na shuguli zao.

Image caption Jamii ya wakara ni miongoni mwa jamii chache nchini Tanzania yenye tamaduni nyingi

Wakunga waliomzalisha mama aliyezaa mapacha hawawezi kufanya tendo la ndoa na wao na waume zao hadi pale mzazi walieyezalisha akishakutana kimwili na mumewe.

Kwanini utamaduni huu?

Kwa mujibu wa viongozi wa kimila wa jamii ya wakara, ni lazima utamaduni huu ufanyike ili watoto mapacha wasafishwe na wachukuliwe kama watoto wa kawaida katika jamii.

Veronica Rweyoga Samweli mkaazi wa Ukara, aliwahi kumsaidia Mjamzito ambaye alizaa mapacha, na yeye aliufanya utaratibu huo kama sehemu ya kuwafanya watoto wale wasafashike na wakubalike kwa jamii.

''Ni lazima mama aliyejifungua mapacha afanye mapenzi na mumewe muda mfupi baada ya kujifungua ili watoto wake waweze kutakasika, bila hivyo wanasema watoto hao watapata magonjwa na huenda wakafa na magonjwa yasiyoeleweka kwani hawajafuata mila. Anasema veronica.

Hata hivyo kwa miaka ya zamani, watoto mapacha walikua hawakubaliki kabisa katika jamii hii.

''Zamani watoto mapacha walikua kuna sehemu wanatupwa na wanakufa huko, walikua wanadhani si jambo la kawaida kwa binadamu kuzaa mapacha, wanajua ni mtoto mmoja tuu, lakini kutokana na mabadiliko ya jamii kwa sasa wanawakubali lakini sasa ndio lazima ufanye hiyo mila ili watoto wako waweze kukubalika.

Image caption Veronica Rweyoga Samweli mkaazi wa Ukara, aliwahi kumsaidia Mjamzito ambaye alizaa mapacha

Scolastica Nyangona ni mkaazi wa Ukara na alijufungua wototo Mapacha wa kike na wa kiume, kwa upande wake pia alilazimika kufanya utamaduni huo ili watoto wake wakubalike katika jamii.

''Nilifanya hivyo, sikutaka watoto wangu wapate tatizo na ni sehemu ya utamaduni sioni jambo baya hapo , ingawa inakua baada ya kujifungua na kama mzazi bado unakua haujakaa sawa'' anasema Bi Scolastica.

Jamii ya wakara ni miongoni mwa jamii chache nchini Tanzania yenye tamaduni nyingi na zinaendelea kuzikumbatia mbali na kuwa baadhi wanaona zimepitwa na wakati.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii