India: 'Wasentinele' wanaoishi visiwa vya Andaman na Nicobar ni watu ambao wamejitenga kabisa na dunia

The Sentinelese have always resisted outside contact Haki miliki ya picha INDIAN COASTGUARD/SURVIVAL INTERNAT

Mmarekani mmoja ameripotiwa kuuwawa kwa mishale na kabila ambalo linaogopeka nchini India katika maeneo ya visiwa vya Andaman na Nicobar.

Wavuvi ambao waliokuwa wamemchukua mpaka kisiwa cha Kaskazini mwa Sentinel wanasema watu wa jamii hiyo walimrushia mishaleakiwa ufukweni na kumuua.

Mwili wake uliachwa kwenye ufukwe.

Vyombo vya habari vya nchini humo vilisema kwamba alikuwa anafanya kazi maalamu ya kueneza neno la Mungu.

Mwanaume huyo alitambulika kwa jina la John Allen Chau.

Ni kinyume na sheria kwa wageni kuwasiliana na makabila ya Andaman ambayo yamejitenga na ulimwengu.

Idadi ya watu wa kabila la Wasentinel ambao ndio walimuua inakadiriwa kuwa 50 mpaka 150.

Wavuvi saba walikamatwa kwa kosa la uvuvi haramu katika kisiwa hicho, polisi walithibitisha.

Vyombo vya habari vya nchini humo vimeripoti pia kuwa mmarekani huyo alikuwa anataka kuwahubiria ukristo watu wa kabila hilo.

Haki miliki ya picha Survival International
Image caption Watu wa baadhi ya makabila yanayoishi visiwa hivyo hufanana na Bushmen wanaoishi Afrika

Polisi wanasema kwamba Chau aliwahi kutembelea eneo hilo awali kama mara nne au mara tano akisaidiwa na wavuvi .

Idadi ya watu wanaoishi katika ukanda huo wa kaskazini wa kabila la Andaman ni ndogo, hawaelewi hata namna ya kutumia hela.

Vilevile ni hatia kwa mtu kuwa na mawasiliano na watu hao.

Mwaka 2017, serikali ya India ilisema kuwa mtu kupiga picha au kutengeneza video ya watu wenye asili ya visiwa vya Andaman, watahukumiwa kwa kuwekwa gerezani kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu.

Mishale ilikuwa inarushwa kwenye helkopta

Mara ya kwanza kabila hili la 'Wasentinel' lilianza kusikika mwaka 2004 mara baada ya maafa ya Tsunami katika bahari ya hindi.

Siku chache baadaye mamlaka ilitangaza katika mkutano na waandishi wa habari kuwa mtu mmoja wa kabila lililotengwa amepona.

Ndege ya jeshi iliyokuwa ikizunguka katika eneo la kaskazini la kisiwa cha Sentinel ilipita katika eneo hilo ili kuwaangalia.

Lakini wakati ndege hiyo aina ya helkopta ilipokuwa inakaribia, watu wa kabila hilo walianza kurusha mishale kwa wanajeshi hao.

"Na hivyo tulibaini kuwa wako salama,'' rubani alituambia.

'Wasentinele' wanatajwa kuwa ni kabila hatari zaidi duniani.

Ni miongoni mwa watu wa kwanza ambao walifanikiwa kuhama kutoka Afrika na wanasayansi wanaamini kuwa walikuja katika kisiwa cha Andaman miaka 60,000 iliyopita.

Mwaka 2006, kikundi cha kampeni ya uokoaji watu kimataifa walisema kabila hilo liliuwa wavuvi wawili ambao walikuwa wanajaribu kuingia katika kisiwa chao kinyume na sheria.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii