Kampeni za kura ya urais kumrithi Joseph kabila zaanza DRC, hali ya usalama mashakani

Josph Kabila Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Rais anayemaliza muda wake Joseph Kabila

Kampeni za uchaguzi wa urais zinaanza leo ya Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo huku kukiwa na mpasuko mkubwa kwenye upande wa upinzani na hofu juu ya usalama.

Mwisho wa wiki iliyopita wafuasi watatu wa chama tawala cha rais Joseph Kabila wanaripotiwa kuchinjwa katika jimbo la Kasai walipokuwa wakifanya kampeni.

Kura ya kumchagua mrithi wa Kabila aliyekaa madarakani kwa mika 17 itafanyika tarehe 23 ya mwezi ujao, Desemba 2018.

Wiki iliyopita Martin Fayulu alichaguliwa kusimama kama mgombea kinara wa upinzani na ameungwa mkono na wapinzani wengine wenye ufuasi mkubwa kama Moise Katumbi na Jean Pierre Bemba.

Hata hivyo, chama cha upinzani chenye wafuasi wengi zaidi nchini humo cha Union for Democracy and Social Progress tayari kimejitenga na mgombea huyo. Chama hicho kinaongozwa na Felix Tshisekedi kimekuwa mstari wa mbele dhidi ya utawala wa kabila.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Martin Fayulu (kati) alichaguliwa kusimama kama mgombea kinara wa upinzani lakini tayari wapo waliojitokeza kumpinga

Kiongozi mwingine wa upinzani Vital Kamerhe pia alijitoa kwenye makubaliano hayo akisema hakukuwa na uungwaji mkono wa kutosha kutoka mashinani baina ya wanachama.

Je Emmanuel Ramazani Shadary, ni nani?

Endapo mgogoro huo ndani ya upinzani utaendelea kupamba moto itakuwa ahueni kwa mgombea kutoka chama tawala Emmanuel Ramazani Shadary.

Shadary anaonekana na wengi kuwa ni kibaraka wa Kabila ambaye amezidisha muda wake madarakani kwa miaka miwili.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Felix Tshisekedi, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani ametangaza kutomuunga mkono Fayulu.

Siasa za DRC zimekuwa zikitawaliwa kwa mkono wa chuma na Kabila ambaye chini yake vyombo vya usalama vilitumika kuudhibiti upinzani kwa nguvu kubwa.

Uchaguzi DRC: Upinzani wavunjika vipande

Mapema mwezi huu wanafunzi wawili wa chuo kikuu cha kinshasa waliuwawa kutokana na majeraha ya risasi walizopigwa na polisi, wakati wa maandamano ya amani, polisi hao walichukuliwa hatua huku wakubwa wao waliwapa amri ya kuingia chuoni wakiachwa.

Haki miliki ya picha PPRD
Image caption Ramazani Shadary anagombea kupitia chama tawala cha rais Joseph Kabila

Mwezi wa nane watu wengine watano waliuwawa katika maandamano mjini lubumbashi wakati walipoingia mtaani kwa maandamano ya kupinga kukatiwa kwa Moise Katumbi kushiriki miongoni mwa wagombea urais katika uchaguzi wa mwaka huu.

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International limeonya kuwa kunauwezekano mkubwa wa uchaguzi huo kukumbwa na vurugu kutokana na chuki zilizokuwepo za kisiasa na uhasama baina ya raia na vyombo vya usalama.

Mada zinazohusiana