Uingereza yaahidi msaada wa £50m kukabiliana na ukeketaji Afrika

An FGM "cutter" in Kenya shows the razorblade she uses to cut girls' genitals Haki miliki ya picha Barcroft Media via Getty Images
Image caption Mkeketaji Kenya aonyesha wembe anaoutumia kuwakata wasichana

Uingereza itatoa msaada wa £ milioni 50 ($64m) kusaidia kusitisha ukeketaji Afrika.

Serikali inasema huu ni uwekezaji mkubwa wa kipekee kufikia leo duniani katika kusaidia kusitisha ukeketaji kufikia mwaka 2030.

Ukeketaji ni utamaduni unaohusisha kukatwa kwa sehemu ndogo au nzima ya sehemu za siri za mwanamke, baadhi wakifanya kama sehemu ya utamaduni wa mtoto kuingia ukubwani.

Shirika la misaada la ActionAid limekaribisha msaada huo lakini limeongeza kwamba kulenga ukeketaji pekee, "haitoshi" kusitisha ghasia dhidi ya wanawake.

Mawaziri wamesema fedha hizo pia zitaifaidi Uingereza kutokana na kwamba itapunguza hatari kwa wasichana wanaosafirishwa katika nchi za nje kwenda kukeketwa.

Serikali inasema kuna wasichana wanaokadiriwa 24,000 na wanawake walio katika hatari ya ueketaji Uingereza.

Akitangaza msaada huo, waziri wa maendeleo ya kimataifa Uingereza Penny Mordaunt amesema ukeketaji hauwezi kumalizwa Uingereza, pasi "kuuangamiza duniani".

"Wanawake wajasiri, wanaotia moyo wa Afrika wanaongoza jitihada kusitisha utamaduni huo katika nchi zao, na kwa mchango wao, jamii nyingine zimeanza kujitenga na utamaduni huo,"amesema.

"Lakini hatua ipo katika kiwango muhimu, na ni lazima tushirikiane kuwalinda mamilioni ya wasichana ambao bado wamo katika hatari ya kukeketwa."

Nchi zinazofaidi zaidi na msaada huu:

Msaada huo utasaidia kufadhili mashirika kama vile mradi wa Saleema nchini Sudan, unaonuia kuwaonyesha wasichana kwamba wana uwezo hata wasipokatwa pamoja na kujaribu kubadili mitazamo ya wazee katika jamii.

Sudan mojawapo ya nchi zenye viwango vikubwa vya ukeketaji, lakini kwa usaidizi kutoka serikali ya Uingereza, watu zaidi wanaugeuzia mgongo utamaduni huo.

Katika kijiji cha Al Baseer jimboni Gazeera, kusini mwa mji mkuu Khartoum, sherehe inaendelea.

Wanaume wa kati ya 30- 40 wanasimama kwenye mduara wakiimba na kucheza.

Na wana kila sababu ya kusherehekea. Kijiji hiki kimeachana kabisa na ukeketaji.

Inaarifiwa mara ya mwisho utamaduni huo kufanyika katika eneo hili ni katika miaka ya 90.

Hakuna anayezungumzia ukeketaji.

Image caption Ahmed Mohamed na mkewe Khadija

Jitihada hizi zilianza mnamo 1983 wakati jamaa mmoja alipoamua kwamba imetosha kwa familia yake.

Ahmed Mohamed alikuwa akifanya kazi Saudi Arabia. Aligundua kuwa ukeketaji hautekelezwi huko.

'Kuna sababu nyingi kwanini ukeketaji ni makosa. Wanawake walifariki, inawasababisha wasichana wasiwe na hamu na tendo la ndoa. Dini yetu hailikubali hilo. Wasaudi hawafanyi ukeketaji, kwahivyo ni makosa, na ndio sababu tukaamua tusilifanye tena.

Mke wangu alikabiliwa na shinikizo kubwa, lakini nashukuru kwamba alikataa'.

Mkewe Ahmed, Khadija, alikabiliwa na unyanyapaa na kutengwa na jirani zake. Lakini leo hali ni tofuati, anakubalika.

Mwanamke anafunguka kuhusu madhila aliyoyapitia.

Image caption Idadi kubwa ya wanawake na wasichana kwengineko Sudan hukeketwa

'Mimi nilikuwa miongoni mwa wasichana wa mwisho waliokeketwa katika kijiji hichi. Nilizaliwa mnamo 1989. Niliteseka sana katika maisha yangu ya kwenye ndoa na pia katika kujifungua mtoto wangu na mpaka leo naendelea kuteseka. Sitokuwa kama msichana wa kawaida ambaye hajakatwa,' anasema Rehan.

Watu wengi wanatumia kigezo cha dini kutetea ukeketaji. Lakini hilo sasa linabishwa na kupingwa na viongozi wa kidini Sudan.

'Nadhani ukeketaji ni kinyume na maadili ya dini ya kiislamu na unasababisha matatizo ya ki afya kwa wasichana... tuliiomba jamii itufuate na wakafanya hivyo,' anasema Shekhe mmoja.

Lakini wakunga kama Amira Abdulrahman, mama na ma bibi wanaendelea kuwa na kauli kuu katika suala hili.

Amira anasema aliwakeketa wasichana wengi - wakiwemo mabinti na wajukuu zake. lakini aliachana na shughuli hiyo baada ya kisa kimoja cha msichana nusra kufariki.

Image caption Amira Abdulrahman mkunga aliyekuwa akiwakeketa wasichana

'Ningependa kuwaomba radhi... watoto waliniona kama malaika wa kifo. Ilinibidi niifiche sindano nyuma yangu…. kama ningeweza kuzungumza nao, ningewaomba msamaha' anasema Amira.

Wasichana wengi hukeketwa wakiwa wadogo wa umri wa kati ya miaka 7, 8 au wengine hata miaka 3. Kuna jitihada, zinazoungwa mkono na msaada wa Uingereza kuwafunza mapema kuhusu madhara ya hatari ya ukeketaji.

Kwengineko nchini, idadi kubwa ya wasichana na wanawake wanakatwa. Sasa serikali ya Sudan kwa usaidizi wa msaada wa kimataifa, inatumai kuangamiza ukeketaji kitaifa kufikia mwaka 2030.


Ukeketaji

  • Unahusisha kukatwa kwa sehemu ndogo au kamili ya sehemu ya siri ya mwanamke 'kwasababu zisizo za kiafya'
  • Utamaduni unafanyika katika mataifa 30 Afrika, na baadhi ya mataifa Asia na mashariki ya kati
  • Takriban wasichana milioni 3 na wanawake duniani wamo katika hatari kila mwaka
  • Hutekelezwa zaidi kwa wasichana wadogo, kawaida baada ya kuzaliwa hadi umri wa miaka 15
  • Mara nyingi hutokana na itikadi au imani kuhusu kinachofikiriwa kuwa ndio tabia sahihi za wakati wa tendo la ndoa, kumtayarisha msichana kuingia ukubwani na ndoa na kuhakikisha kuwa msichana "anakuwa mwanamke kamili"
  • Hatari ni pamoja na kuvuja damu kupita kiasi, matatizo ya wakati wa kukojoa, maambukizi, kushindwa kupata uja uzito na kuongezeka matatizo wakati wa kujifungua mtoto na hata vifo vya watoto wachanga.

Chanzo: World Health Organization


Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii