Zijue faida na hasara za mbegu za kisasa za GMO zilizopigwa marufuku Tanzania

Waandamanaji wakipinga matumizi ya GMO nchini Afrika Kusini mwaka 2013 Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Waandamanaji wakipinga matumizi ya GMO nchini Afrika Kusini mwaka 2013

Serikali ya Tanzania imepiga marufuku shughuli za utafiti wa mbegu za uhandisi jeni (GMO) pamoja na kuamuru kuteketeza mazao yote ya aina hiyo tayari yanafanyiwa tafiti.

Uamuzi wa serikali ya Tanzania unakuja baada ya miaka 10 ya mijadala, upinzani na majaribio ya njia hiyo mpya na ya kisasa ya kilimo.

Kampeni za majaribio ya mbegu za GMO nchini Tanzania zilianza mwaka 2008 chini ya mradi wa Water Efficient Maize for Afica (WEMA) unaodhaminiwa na wakfu wa matajiri Bill&Merinda Gates lakini majaribio rasmi yalianza kufanyika mwaka 2016.

Jumanne wiki hii, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mathew Mtigumwe aliamuru kusitishwa kwa majaribio hayo yaliyokuwa yanafanyika katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (Tari) katika kituo chake cha Makutupora, Dodoma.

Mtigumwe amesema serikali imechukua uamuzi huo baada ya kujiridhisha kuwa taasisi hiyo ilikuwa imeshaanza kutangaza matokeo ya utafiti kabla ya kuthibitishwa na serikali.

"Walitakiwa kwanza kutoa ripoti hiyo kwa wizara kusudi ijiridhishe kama mbegu hizo ni salama kwa matumizi ya binadamu, baada ya majadiliano ndiyo serikali ingefanya uamuzi."

Mjadala wa GMO

Kama ilivyo duniani kote, mjadala wa GMO nchini Tanzania umegawanya wadau katika makundi mawili.

Kundi la kwanza ni la wale wanaotetea matumizi ya ya teknolojia hiyo wakisema ina tija katika kutoa mazao mengi katika eneo dogo. Kutokana na uwezo huo, wanaopigia debe GMO wanasema mbegu hizo zitaondoa upungufu wa chakula kwa muda mfupi.

Mbegu za GMO pia zipo kwa mazao ya biashara kama pamba na uzalishaji wake ni maradufu kulinganisha na mbegu za asili.

Mbunge wa Mwanga na waziri wa zamani wa Kilimo Tanzania Profesa Jumanne Maghembe ameliambia gazeti la Mwananchi kuwa kwa mazao ya viwandani mbegu za GMO huzalisha mpaka mara 10 zaidi.

"Hata nguo tunazovaa zinatoka nje, pamba yake ni GMO."

Korosho Tanzania: 'Hatima ya wafanyabiashara itajulikana baadaye'

Kwa wale wanaopinga matumizi ya mbegu hizo hoja zao kuu zipo katika usalama wa kiafya, mazingira na soko la mbegu.

Katika ulimwengu wa sayansi kuna msuguano mkubwa wa usalama wa kiafya kwa wanaadamu kula vyakula vilivyotokana na mbegu za GMO.

Tafiti nyingi ikiwemo za Shiririka la Kimataifa la Chakula na Kilimo (FAO) zinaonesha kuwa vyakula vinavyotokana na mbegu za GMO zinamadhara kiafya, lakini hakuna utafiti unaokubalika ulioonesha kuwa vyakula hivyo ni salama.

Hoja nyengine ni uchavishaji wa mimea. Mimea itokanayo na GMO ni jamii vamizi ( kwa kingereza invasive species) na hivyo itakapofanya uchavishaji (cross-polination) na mimea mingine uwezekano ni mkubwa kwa mimea mingine kuharibika.

Kutokana na hilo, wakulima wote watalazimika kutumia mbegu za GMO ili mazao yao yasiharibike.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Wakulima wakivuna pamba itokanayo na mbegu za GMO nchini Burkina Faso. Wakulima hao wamekuwa wakilalamikia bei ndogo ya zao hilo kutokana na kutawaliwa na kampuni moja tu inayouza mbegu na kununua mazao yao.

Hatari zaidi ipo kwenye mimea ya asili ambayo inaweza kupotezwa kabisa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dkt Richard Mbunda hivi karibuni aliandika barua ya wazi kwa rais John Magufuli akipinga matumizi ya GMO nchini akisema yataleta madhara makubwa kiafya, mazingira na ustawi wa soko la chakula.

Barua hiyo ilichagiza mjadala wa GMO kwa kiasi kikubwa. "Ninaishukuru sana serikali kwa kusikia kilio cha wakulima. Mie kama mtafiti nimetimiza wajibu wangu wa kupaza hoja za wakulima," ameiambia BBC.

Mbunda ni mtaalamu wa Sayansi ya Siasa na chapisho lake la shahada ya uzamivu (PhD) liliangazia usalama wa chakula na athari za GMO kiuchumi na kijamii.

Wafuasi wa chama cha Kabila wachinjwa DRC

Mbegu za GMO kutokana uvamizi wake wa kiasili hulazimisha wakulima wengine kuzitumia ili wapate mavuno na kufanya utegemezi wa mbegu hizo kuwa mkubwa.

"Watu wanapaswa kufahamu kuwa, mbegu za GMO hupandwa mara moja tu, hivyo msimu ujao lazima ukanunue tena mbegu. Pia mkulima anakuwa hana tena uwezo wa kufanya uchaguzi wa mbegu," amesema Mbunda na kuongeza: "Kwa sasa kuna makampuni machache, huu ukanda wetu lipo kampuni moja tu linalosambaza mbegu hizo kutoka Marekani. Kukubali kutumia mbegu hizo ni kukiweka kilimo chetu na usalama wa chakula rehani."

"Hata Ulaya na Marekani chakula kitokanacho na GMO huliwa na watu masikini tu, matajiri hula vya asili,"amesema.

Mwaka 2012 Kenya ilipiga marufuku uingizwaji na usambazaji wa mimea na mbegu za GMO baada ya mjadala mkubwa.

Mada zinazohusiana