Tanzania: Mbowe afutiwa dhamana kwa kukiuka masharti

Mwenyekiti waCHADEMA, Freeman Mbowe Haki miliki ya picha CHADEMA
Image caption Mwenyekiti waCHADEMA, Freeman Mbowe

Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA, Freeman Mbowe amefutiwa dhamana na mahakama ya hakimu mkazi kisutu mara baada ya kukiuka masharti aliyopewa.

Maamuzi hayo yametolewa leo kwa madai kuwa alidharau maamuzi ya mahakama.

Na sababu zilizotolewa kudaiwa kuwa hazina ukweli wowote.

Sababu zilizotolewa ni kwamba Mbowe alishindwa kuhudhuria mahakamani tarehe 8 November 2018 baada ya kuugua ghafla na kwenda Afrika kusini kwa matibabu.

Mwezi Oktoba 28,alielekea Washing DC Marekani kuhudhuria mkutano na aliporejea tarehe 31 Oktoba aliugua ghafla.

Wakati huohuo mbunge wa Tarime mjini, Esther Matiko pia alifutiwa dhamana wa kukiuka masharti.

Matiku alishindwa kuhudhuria mahakamani baada ya kwenda kwenye ziara ya wabunge nchini Burundi, sababu ambayo alielezwa kwamba haikidhi matakwa ya kushindwa kufika mahakamani.

Mbowe alishtakiwa katika mahakama ya Kisutu pamoja na viongozi wengine kwa kufanya maandamano kabla ya kufanyika uchaguzi wa eneo bunge la Kinondoni kinyume na sheria, hatua iliowalazimu maafisa wa polisi kupiga risasi juu ili kuwatawanya waandamanji.

Utaratibu wa Dhamana ukoje?

Betty Masanja, Mwanasheria na mchambuzi wa masuala ya jamii anasema kwamba dhamana huwa ni haki ya kila mtuhumiwa kama kesi yake sio ya mauaji.

Lakini kwa kawaida dhamana huwa inafutwa baada ya mtu kukiuka masharti.

Kuna aina mbalimbali za dhamana na masharti yake huwa yanategemea na kesi yenyewe.

"Kuna mtu akipewa dahamana anaweza kunyang'anywa hati yake ya kusafiria au anaweza kuachwa nayo lakini hawezi kusafiri mpaka apewe ruhusa na mahakama.

Kuacha kuhudhuria mahakamani kwa mshakiwa bila sababu au sababu yake kutokubaliwa na mahakama kunaweza kupelekea dhamana kufutwa" Masanja aliiambia BBC.

Kufutiwa dhamana kuna maana gani?

Mtu akifutiwa dhamana hii ina maana kwama mtuhumiwa atatakiwa kukaa mahabusu ili aweze aweze kuhudhuria mahakamani kama anavyohitajika bila vipingamizi vyovyote.

Mtu akifutiwa dhamana anaweza kupata dhamana kwa mara nyingine mpaka wakili wake aandike sababu za kisheria kwa mahakama na kueleza sababu za wa nini asifutiwe na kwa nini aendelee kubaki uraiani?

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii