Wasiwasi Urusi - Ukraine baada ya kutekwa meli za kivita

Wanaharakati wa mrengo wa kulia Ukraine, wamekuwa wakishinikiza kuidhinishwa kwa sheria ya kijeshi Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wanaharakati wa mrengo wa kulia Ukraine, wamekuwa wakishinikiza kuidhinishwa kwa sheria ya kijeshi

Bunge la Ukraine linatarajiwa kuamua iwapo litaidhinisha sheria ya kijeshi , baada ya meli zake tatu kutekwa na Urusi.

Meli hizo zilikuwa zikitoka pwani ya Crimea, iliyomeguliwa na Urusi mnamo 2014 kutoka kwa Ukraine, zilipotekwa.

Ukraine imesema Urusi ilivurumiza mojawapo ya maboti yake dhidi yao katika 'hatua ya uchokozi', huku Urusi nayo ikisema meli hizo ziliingia kiharamu katika mipaka yake majini.

Mkasa huu unadhihirisha kuongezeka kwa wasiwasi kati ya nchi hizo mbili.

Hii ni mara ya kwanza majeshi ya mataifa hayo mawili yanakabiliana wazi katika miaka ya hivi karibuni, licha ya kwamba vikosi vya Ukrain vimekuwa vikipambana nawanamgambo wanaoshinikiza kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi mashariki mwa nchi hiyo.

Maafisa waliokamatwa ndani ya meli hizo zilizotekwa, wanahojiwa huko Kerch, Urusi inasema.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Meli zilizotekwa zilisafirishwa hadi bandari moja mjini Kerch

Nini hasaa kilichotokea?

Urusi imezishambulia na kuziteka meli tatu za kivita za Ukraine zilizokuwa baharini katika rasi ya Crimea katika kisa ambacho kimezidisha uhasama baina ya mataifa hayo mawili.

Meli mbili ndogo za kivita, pamoja na meli moja ya kusindikiza meli ndizo zilizotekwa na wanajeshi wa Urusi.

Wahudumu kadha wa meli za Ukraine wamejeruhiwa.

Kila taifa linamlaumu mwenzake kwa kusababisha kisa hicho.

Wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la Usalama na Ulinzi la Ukraine, Rais Petro Poroshenko alieleza vitendo vya Urusi kuwa "uchokozi usio na sababu na za kiwendawazimu."

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wanaharakati wa mrengo wa kulia Ukraine, wamekuwa wakishinikiza kuidhinishwa kwa sheria ya kijeshi

Urusi imeomba kuandaliwe mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, mkutano ambao balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley amesema umepangiwa kufanyika saa tano asubuhi saa za New York (16:00 GMT) leo Jumatatu.

Uhasama umekuwa ukiongezeka katika Bahari Nyeusi na Bahari ya Azov katika rasi ya Crimea, eneo lililotekwa na Urusi mwaka 2014 kutoka kwa Ukraine.

Mzozo wa sasa umezuka vipi?

Asubuhi, meli za kivita za Berdyansk na Nikopol, pamoja na meli ya kuzisindikiza Yana Kapa, zilijaribu kusafiri mji wa bandarini kwenye Bahari Nyeusi wa Odessa kuelekea Mariupol katika Bahari ya Azov.

Ukraine inasema Urusi ilijaribu kuzizuia meli hizo zisiendelee na safari yake, ambapo meli moja iliigonga meli ya Yana Kapa.

Meli hizo ziliendelea na safari kuelekea mlango wa bahari wa Kerch, lakini zikapata njia imezibwa na meli moja kubwa.

Urusi wakati huo ilikuwa imetuma ndege mbili za kivita na helikopta mbili ambazo zilikuwa zikipaa angani katika eneo hilo na kufuatilia mwenendo wa meli hizo.

Urusi inaituhumu Ukraine kwa kuingia kinyume cha sheria katika maeneo yake ya bahari na usafiri eneo hilo umesitishwa kwa muda usiojulikana kwa sababu za kiusalama.

Jeshi la wanamaji la Ukrane lilisema meli hizo zilikuwa zimeshambuliwa na kuharibiwa zilipokuwa zinajaribu kuondoka eneo hilo.

Imesema wahudumu wake sita wamejeruhiwa.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Jeshi la wanamaji la Urusi lilizizuia meli hizo za Ukraine baada ya kuzituhumu kwa kuingia kinyume cha sheria kwenye maeneo ya bahari ya Urusi

Idara ya Usalama ya Urusi ifahamikayo kama FSM, ambayo inatekeleza mengi ya majukumu yaliyotekelezwa na KGB, ilithibitisha baadaye kwamba moja ya boti zake za kushika doria baharini ilitumia nguvu kuchukua udhibiti wa meli tatu za Ukraine.

Lakini walisema ni mabaharia watatu pekee waliojeruhiwa.

Ukraine imesema ilikuwa imeifahamisha Urusi kuhusu mpango wake wa kupitishia meli hizo zake eneo hilo kuelekea Mariupol.

Kulaumiana

Uchanganuzi wa Steven Rosenberg, BBC News, Moscow

Uhasama kati ya Russia na Ukraine umekuwa ukiongezeka kwa miezi kadha katika rasi ya Crimea.

Chini ya mkataba wa mwaka 2003 kati ya Moscow na Kiev, mlango wa bahari wa Kerch na Bahari ya Azov huchukuliwa kama maeneo ya pamoja.

Hata hivyo, karibuni, Urusi ilianza kuzikagua meli zote zilizokuwa zikisafiri kuingia au kutoka bandari za Ukraine.

Hatua ya Urusi kutumia nguvu kuzitwaa meli hizo za Ukraine - pamoja na mejeruhi - ni hatua inayozidisha zaidi uhasama.

Lakini hauwezi kutarajia Urusi wakubali lawama.

Chini ya Rais Vladimir Putin, Urusi ilipotumia nguvu awali, imekuwa ikijitetea na kusema: "Si sisi tulioanzisha haya."

Walifanya hivyo wakati wa vita vya Urusi na Georgia mwaka 2008 na pia kushiriki kwa wanajeshi maalum wa Urusi Crimea mwaka 2014, hatua iliyotangulia kutekwa kwa rasi hiyo ya Crimea na Urusi.

Kwa hivyo, tarajia Urusi imlaumu Rais Poroshenko na serikali yake kwa yaliyotokea Jumapili na yote yatakayofuata.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Waandamanaji 150 waliandamana nje ya ubalozi huo

Hatua hiyo imepokelewaje?

Mzozo wa sasa umepokelewa kwa ghadhabu na wakazi Ukraine.

Jumapili jioni, kundi la watu 150 hivi walikusanyika nje ya ubalozi wa Urusi mjini Kiev, baadhi wakiwa na mienge.

Gari moja la ubalozi huo lilichomwa moto.

"Tumekusanyika hapa leo kupinga vitendo vya Warusi leo, kuhusu kushambulia jeshi letu," Oleksiy Ryabov, mmoja wao, aliambia shirika la habari la Reuters.

"Tuna hasira sana. Tulifaa kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na taifa hili miaka mingi iliyopita."

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii