Jitihada za kutafuta miili zaidi baada ya ajali ya mashua ziwa Victoria Uganda

Watu wanafuatilia shughulia ya uokozi Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wakaazi wanafuatilia shughulia ya uokozi

Shughuli ya kutafuta miili ya watu waliokuwa kwenye mashua iliyozama katika Ziwa Victoria nchini Uganda siku ya Jumamosi inaendelea.

Taarifa za awali zinasema zaidi ya watu 90 walikuwa ndani ya mashua hiyo wakati ilipohusika katika ajali.

Maafisa wa uokozi wamethibitisha kuwa maiti 33 zilikuwa zimeopolewa ziwani kufikia siku ya Jumapili jioni huku manusura 26 pia wakiokolewa.

Muda mfupi baada ya kisa hicho kutokea, vikosi vya polisi na jeshi na jamaa na waokoaji wengine walianza shughuli ya kujaribu kuokowa maisha ya watu hao.

Miongoni wa mwatu 26 walionusurika alikuwemo mwana Ufalume wa Buganda nduguye mfalme wa sasa wa Buganda, pamoja na wasanii mashuhuri wa Uganda.

Inadaiwa wasanii hao walikuwa wanajianda kuwatumbuiza watu kwenye boti hilo la burudani.

Haki miliki ya picha Reuters

''Injini ya boti hiyo ilikuwa na hitilafu kwa sababu ilikuwa inazimika zimika, pia ilikuwa na tundu kubwa iliyokuwa ikiingiza maji ndani ya boti, na kuna wakati boti hiyo ilishindwa kuenda''

Alisema mmoja wa manusura wa boti hiyo.

Punde tu baada ya ajali hiyo maiti 10 zilipatikana, lakini shughuli ya uokozi zikasitishwa kutokana na hali mbaya ya anga na giza kutanda.

Vikosi zaidi vya polisi na jeshi la UPDF ikiwemo jeshi la angani viliendelea na zoezi hilo ambapo maiti kadhaa zilizokuwa zimekwama kwenye boti hilo ziliopolewa majini.

Mashua hiyo iliyokuwa na watu waliokuwa wanaelekea sherehe, ilipata ajali katika kaunti ndogo ya Mpatta wilaya ya Mukono.

Naibu waziri wa uchukuzi nchini Uganda Aggry Bagire anasema ''Boti hii ilikuwa halijasajiliwa wala kufanyiwa ukaguzi na timu yetu ilikuwa ikiitafuta kwa mda wa siku tatu''.

Wamiliki wake walijua kuwa iko katika hali mbaya kiufundi lakini wakalazimisha kufanya safari nayo.

Kisa hiki kimezusha mjadala miongoni mwa wananchi kuhusu usimamizi na usalama wa safari za majini nchini Uganda.

Haki miliki ya picha AFP

Mambo matano kuhusu ziwa Victoria

  • Ziwa Victoria ni ziwa la pili kwa ukubwa duniani na ni ya kwanza kwa ukubwa barani Afrika.
  • Upana wake ni mkubwa kuliko taifa la Uswizi.
  • Maji yake yanatumiwa na mataifa ya Uganda, Kenya na Tanzania.
  • Karibu watu milioni 30 wanalitegemea ziwa Victoria.
  • Ziwa hilo linakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na uharibifu wa mazingira na kushuka kwa viwango vya maji.
  • Uhai anuai katika ziwa hilo umepungua kwa 50% tangu miaka ya 1980.
  • Muingereza John Hanning Speke alilipatia ziwa hilo jina la Malikia Victoria wa Uingereza aliyezuru hapo mwaka 1858.
  • Kumekuwa na mapendekezo ya kulibadilisha jina ziwa hilo - ikiwa ni pamoja na jina la kiganda la Nalubaale, na ziwa Jumuiya inayomaanisha "pamoja" kwa Kiswahili.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii