Blue Economy: Namna ya kufaidika na rasilmali bahari ya Mikoko katika uimarishaji biashara na mazingira

mikoko pwani ya Kenya

Kongamano la kwanza duniani la uchumi wa maji linafanyika mjini Nairobi Kenya.

Maelfu ya wajumbe wanakutana kuzungumzia namna ya kunufaika kutokana na raslimali za bahari, mito na ziwa bila ya kuziharibu.

Waandalizi wanatarajia mataifa na makampuni kutoa ahadi kusaidia kuhakikisha rasilmali za baharini duniani zinalindwa kwa vizazi vijavyo.

Mkutano huo unatathmini athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa rasilmali za baharini , na pia namna ya kuzuia uvuvi wa kupita kiasi na kupunguza uchafuzi wa mazingira ambao una athari kubwa kwa mataifa yenye maendeleo kidogo.

Manufaa ya rasilimali za baharini

Katika kijiji cha Gazi pwani ya Kenya jamii imepata namna ya kunufaika na misitu ya mikoko bila kuikatakata.

Hapa Josephat Mtwana na wenzake wanatembea katika matope mazito.

Wanafuatilia ukuaji wa mikoko walioipanda. Ni mradi huliopewa jina Mikoko Pamoja, ambao ni wa kwanza wa aina yake.

Jamii hapa inalipwa kuhifadhi misitu ya mikoko ambayo husafisha hewa.

Huwezi kusikiliza tena
Mikoko inavyoimarisha maisha pwani ya Kenya

Josephat ni mmoja wa wanaojishughulisha katika mradi huu.

''Kuna swala la mabadiliko ya tabia nchi na tatizo kubwa na gesi za viwanda, hususan carbon dioxide.

Kwahivyo tukipanda miti mingi, tutaweza kupunguza viwango vya hewa chafu kutoka kwenye mazingira kutokana na kwamba mikoko ina uwezo ya kuivuta hewa hiyo chafu kupitia mfgumo ujulikanao kama photosynthesis. Na faida kubwa zaidi tunalipwa kuyapanda mikoko haya''.

Wanajigawa katika makundi madogo na kutumia vifaa vyao kupima ukuaji wa Miti na jinsi inavyonyonya hewa chafu ya Carbon kutoka kwa mazingira.

Kwa miaka mingi misitu ya mikoko imekuwa ikikatwa kwa matumizi ya ujenzi na kuni na pia kurahisisha uvuvi.

Lakini sasa wakaazi wanakuza upya mikoko katika maeneo yaliyoharibiwa baada ya wanasayansi kufaulu kufanya hivyo katika mradi wa kwanza wa majaribio.

Misitu iliuokuzwa upya ina manufaa mengi:

  • Inazuia ardhi iliyokaribu kusombwa na maji
  • Ni makao ya viumbe wengi
  • Na pia ni maeneo ya samaki kutaga mayai

Wavuvi katika eneo la Gazi wanarejea kutoka bahari hindi.

Wamevua samaki wengi na kuwapakia katika magunia na hapa wanunuzi ni wengi. Juma Said, ni mmoja wa wavuvi.

Image caption Mvuvi Juma Said

Zamani watu walikuwa hawana ufahamu kwamba unapokata mikoko, samaki wanapotea.

'Kwahivyo waliyakata mikoko kwa wingi kuuza kupata pesa na katika hali hiyo walikuja kugundua kwamba samaki wanapotea'.

'Lakini mradi huu kuanzishwa, tumeelimika, na tumeyapanda mikoko na tukagundua idadi ya samaki ikiongezeka kwasababu wana sehemu ya kujificha na kuzaa'.

Mradi wa Mikoko Pamoja huiletea jamii zaidi ya dolla 10,000 kutokana na malipo ya kusafisha hewa, maarufu kama carbon trading.

Fedha hizo hutumika kufanikisha miradi ya kijamii kama vile elimu, usambazaji wa maji safi na utalii.

Wanasayansi wanasema misitu ya mikoko inaharibiwa mara tatu zaidi ya misitu ya nchi kavu. Hatahivyo huenda miradi kama hii ya ukuzaji mikoko ikaibadili hali hiyo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii