Uhariri wa Vinasaba: Wachina 'wameunda' binadamu asiyeweza kuambukizwa Ukimwi?

embryo Haki miliki ya picha Getty Images

Mwanasayansi kutoka Uchina ambaye amedai kuwa amesaidia kuzalisha watoto wa kwanza ambao chembe zao za jeni zilihaririwa kabla ya kuzaliwa na kwamba hawawezi kuambukizwa Ukimwi, ameshutumiwa vikali na madai yake kutiliwa shaka.

Prof He Jiankui anadai kwamba wasichana hao pacha, waliozaliwa wiki chache zilizopita, vinasaba vyao (DNA) vilifanyiwa ukarabati wakiwa bado ni vinitete kuwawezesha kutoambukizwa Virusi Vinavyosababisha Ukimwi (VVU).

Madai yao aliyoyatoa kwenye kanda ya video iliyosambazwa na shirika la habari la Associated Press hayajapigwa darubini na yamewaghadhabisha wanasayansi wengine.

Wamesema wazo hilo lenyewe ni la kuogofya.

Kazi kama hizo za kisayansi, za kuhariri jeni za binadamu, zimepigwa marufuku katika mataifa mengi.

Vizazi vijavyo

Wanasayansi wanaamini kwamba uhariri wa jeni unaweza kuwaepushia watu magonjwa ya urithi yanayotokana na vinasaba, kwa kufuta chembe za jeni zinazosababisha magonjwa hayo au hata kuzifanyia ukarabati mtoto akiwa bado ni kiinitete.

Lakini wataalamu wana wasiwasi kwamba kuhaririwa huko kwa jeni kunaweza kusababisha madhara makubwa sio tu kwa mtoto mwenyewe bali pia vizazi vya baadaye ambavyo vitayarithi marekebisho yaliyofanywa na wanasayansi kwenye vinasaba.

Katika mataifa mengi, ikiwemo Uingereza, kuna sheria zinazoharamisha kuhaririwa kwa jeni hata katika mchakato wa kuwasaidia binadamu kutungisha mimba.

Haki miliki ya picha Getty Images

Wanasayansi wanaweza kufanya utafiti kuhusu uhariri wa jeni kwa kutumia viinitete vilivyotupwa baada ya mwanamke kutungishwa mimba kwenye maabara, shughuli inayofahamika kama IVF, lakini hilo huruhusiwa tu kwa sharti kwamba viinitete hivyo vitaharibiwa baada ya utafiti na visitumiwe kuzalisha mtoto.

'Watoto wa maabara'

Lakini Prof He, aliyesomea Stanford nchini Marekani na anayefanyia kazi yake katika maabara moja katika jiji la Shenzhen kusini mwa China anasema alitumia vifaa vya kuhariri jeni 'kuwaunda' watoto hao wawili pacha waliopewa majina "Lulu" na "Nana".

Kwenye video, amedai kwamba alifanikiwa kuondoa jeni kwa jina CCR5 kwenye viinitete vya na kuwawezesha watoto hao kuwa na kinga ya kudumu dhidi ya Ukimwi hata wakikumbana na virusi hivyo.

Anasema kazi yake imeangazia kuwaunda watoto ambao hawaugui maradhi mbalimbali na si kuwaunda watoto wa maabara wa kupendeza, wenye macho ya kuvutia au wenye kiwango cha juu cha werevu.

"Ninaelewa kwamba kazi yangu itazua utata - lakini ninaamini kwamba familia zinaihitaji teknolojia hii na niko tayari kushutumiwa mradi tu niwe nawasaidia," anasema kwenye video hiyo.

'Kuweza kutibiwa'

Hata hivyo, mashirika kadha, ikiwemo hospitali iliyohusishwa na madai hayo imekana kuhusika.

Chuo Kikuu cha Kusini cha Sayansi na Teknolojia mjini Shenzhen kimesema hakikuwa na ufahamu kuhusu mradi huo wa profesa huyo na sasa kitaanzisha uchunguzi.

Na wanasayansi wengine wanasema iwapo taarifa hizo ni za kweli, basi Prof He atakuwa amevuka mipaka, kwa kufanyia majaribio viinitete vyenye afya katika utafiti wake bila idhini wala msingi.

Prof Robert Winston, mtaalamu wa masuala ya uzazi, amesema: "Hii ni ripoti ya uongo, ni utovu wa maadili katika sayansi na ni kukosa uwajibikaji."

"Kama ni kweli, bado itakuwa ni utovu wa maadili kisayansi."

Dkt Dusko Ilic, mtaalamu katika seli za viinitete katika chuo kikuu cha King's College London, amesema: "Ikiwa hili linaweza kukubalika kimaadili, basi mtazamo wao wa maadili ni tofati sana na maeneo mengine ya dunia."

Anasema kwamba siku hizi Ukimwi ni ugonjwa unaoweza kutibiwa na kudhibitiwa na iwapo ni ugonjwa unaoweza kudhibitiwa kwa dawa, basi hakuna hatari yoyote ya mzazi kumrithisha mtoto.

Hatari zilizopo

Prof Julian Savulescu, mtaalamu wa maadili katika Chuo Kikuu cha Oxford amesema: "Kama ni kweli, basi majaribio hayo yanaogofya. Viinitete hivyo vilikuwa na afya - havikuwa na magonjwa yoyote."

Haki miliki ya picha Kathy Niakan
Image caption The embryo divides and develops from a single fertilised egg (top left) to a blastocyst (bottom right)

"Uhariri wa jeni wenyewe bado ni jambo linalofanyiwa majaribio na unahusishwa na matokeo mengine ambayo wakati mwingine huwa hayajatarajiwa, ya kubadilika kwa maumbile. Unaweza kusababisha matatizo ya kinasaba mapema au baadaye katika maisha ya mtoto, au hata kusababisha saratani."

"Majaribio haya yanawaweka watoto waliokuwa katika afya nzuri kwenye hatari za uhariri wa jeni bila kuwa na manufaa yoyote kwao."

Wanasyaansi wanasema uhariri wa jeni unaweza kukubalika siku za baadaye, lakini sheria zaidi na umakinifu unahitajika kabla ya kuruhusiwa.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii