Uchaguzi DRC 2018: Felix Tshisekedi, Vital Kamerhe na Martin Fayulu walivyougawa upinzani

Vital Kamerhe (kushoto) na Felix Tshisekedi Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Vital Kamerhe (kushoto) na Felix Tshisekedi

Kiongozi wa chama kikongwe zaidi cha upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi amerejea leo nchini humo kuanza kampeni yakutaka kuchaguliwa kuwa rais katika uchaguzi wa mwezi ujao.

Yeye ni kiongozi wa chama cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS) na aliidhinishwa kuwa mgombea wa urais wa pamoja baada ya mazungumzo kati yake na mgombea wa chama cha UNC (Union for the Congolese Nation) Vital Kamerhe.

Mwafaka kati ya wawili hao uliafikiwa jijini Nairobi mnamo 23 Novemba, na leo ndiyo mara yao ya kwanza kurejea DR Congo.

Ingawa Tshisekedi ananadiwa kama mgombea wa umoja wa wapinzani, si yeye pekee anayeungwa mkono na ubia wa vyama vya upinzani.

Vyama vya upinzani nchini humo vilikuwa vimekutana Geneva na kumteua Martin Fayulu kuwa mgombea wa pamoja wa umoja wa vyama vya upinzani.

Bw Fayulu ni mbunge ambaye si maarufu sana kisiasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kuchaguliwa kwake kulionekana kutowafurahisha Tshisekedi na Kamerhe ambao walijiondoa kutoka kwa makubaliano hayo siku moja baadaye.

Katika muungano wa UDPS na UNC, Tshiskedi atagombea wadhifa wa rais naye Kamerhe anatarajiwa kuwa waziri mkuu iwapo muungano wao utashinda urais.

Haki miliki ya picha FABRICE COFFRINI
Image caption Martin Fayulu wakati wa kutangazwa kwake kuwa mgombea wa upinzani Geneva

Kwa jumla kuna wagombea 19 wa urais walioidhinishwa na tume ya uchaguzi, mgombea wa chama tawala cha People's Party for Reconstruction and Democracy, akiwa ni Emmanuel Ramazani Shadary. Bw Kabila ameongoza taifa hilo tangu 2001.

Rais Joseph Kabila anastaafu baada ya kuongoza kwa mihula miwili.

Uchaguzi utafanyika mnamo 23 Desemba baada ya kucheleweshwa kwa miaka miwili.

Mwandishi wa BBC Louise Dewast anasema kuna wasiwasi kwamba ubia wa Tshisekedi na Kamerhe huenda ukagawanya kura za upinzani.

Uchaguzi nchini D Congo huwa ni awamu moja pekee na anayepata kura nyingi hutangazwa kuwa mshindi.

Felix Tshisekedi ni nani?

Felix Tshisekedi, ni mwanawe mwanzilishi wa chama cha UDPS, mwanasiasa wa upinzani wa muda mrefu Etienne Tshisekedi.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Felix Tshisekedi akiwa katika mkutano wa kisiasa Aprili 2018 mjini Kinshasa

Babake alifariki Februari mwaka jana na sasa mwanawe anatarajia kutumia msingi wa umaarufu wa babake kuchaguliwa kuwa rais.

Marafiki zake humuita kwa jina la utani "Fatshi" kutokana na hali kwamba yeye ni mnene kiasi.

Kwa muda ilionekana kana kwamba Tshishekedi, 55, jina lake halingekuwa kwenye karatasi za kura.

Novemba 11, yeye na Vital Kamerhe pamoja na wagombea wengine watano wa vyama vya upinzani walikutana na kumchagua Martin Fayulu apambane na Emmanuel Ramazani Shadary.

Lakini makubaliano yao yalidumu saa 24 pekee.

Tshisekedi na Kamerhe walidai kushinikizwa na vyama vyao kujiondoa na wakajitenga na Fayulu hatua iliyougawanya upinzani.

Wakishinda, Tshisekedi atakuwa rais naye Kamerhe, ambaye ni rais wa zamani wa Bunge na ambaye aliwania dhidi ya Kabila mwaka 2011 awe waziri mkuu.

Tangu babake Tshisekedi alipoanzisha chama cha UDPS mwaka 1982, kilihudumu kama chama kikuu cha upinzani, mwanzoni wakati wa utawala wa Mobutu Sese Seko kisha wakati wa utawala wa babake Kabila, Laurent-Desire Kabila, aliyeongoza 1997 hadi kifo chake 2001.

Kujiondoa kwa Tshisekedi kutoka kumuunga mkono Fayulu kulizua lalama, kwani kuliugawanya upinzani uliokuwa umeonesha dalili za kuungana.

Tshisekedi ni baba wa watoto watatu na yeye na Fayulu ni waumini katika kanisa moja la kipentekoste jijini Kinshasa.

Watakuwa wanawania dhidi ya Shadary ambaye ni Mkatoliki.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Jean-Pierre Bemba alizuiwa kuwania urais na tume ya uchaguzi

Tshisekedi ana stashahada katika mauzo na mawasiliano kutoka Ubelgiji, lakini wakosoaji wake hutilia shaka hilo.

Wakosoaji wake pia wamekuwa wakisema hajawahi kushikilia wadhifa wowote wa juu au kuwa na uzoefu wa usimamizi.

Lakini amepanda cheo chamani, kuanzia mwaka 2008 ambapo alikuwa katibu wa taifa aliyeangazia masuala ya uhusiano wa nje.

Machi mwaka jana aliteuliwa kiongozi wa chama baada ya kifo cha babake.

Alichaguliwa kuwa mbunge 2011, akiwakilisha eneo la Mbuji-Mayi katika mkoa wa Kasai-Oriental lakini alikataa kuhudumu kwa kuwa hakutambua kushindwa kwa babake na Rais Kabila katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2011.

Tshisekedi, ingawa hana uungwaji mkono mkubwa kama wa babake, aliambia AFP mwaka jana kwamba akishinda urais ataunda tume ya ukweli, haki na maridhiano na kumuwajibisha Bw Kabila. Lakini alisema atamruhusu kusalia nchini DR Congo.

Image caption Moise Katumbi alizuiwa kurejea nchini DRC

Walioruhusiwa kuwania urais DR Congo

 • Emmanuel Ramazani Shadary
 • Kikuni Masudi Seth
 • Mukona Kumbe Kumbe Pierre
 • Ngoy Ilunga Isidore
 • Makuta Joseph
 • Kabamba Noel
 • Mabaya
 • Kinkiey Mulumba
 • Freddy Matungulu
 • Felix Tshisekedi
 • Allain Shekomba
 • Radjabu Sombolabo
 • Kamerhe Vital
 • Fayulu Martin
 • Bomba
 • Gabriel Mokia
 • Basheke Sylvain
 • Charles Gamena
 • Mbemba Francis

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii