Rais Magufuli amuagiza Lowassa kuongea na wenzake la sivyo wataishia magereza, awasifu Wachina, misaada yao 'haina masharti'

Rais Magufuli akiwa na Balozi wa China nchini Tanzania Wang Ke wakati wa uzinduzi wa maktaba mpya, kubwa na ya kisasa ya Kikuu cha Dar es Salaam Haki miliki ya picha IKULU, Tanzania
Image caption Rais Magufuli akiwa na Balozi wa China nchini Tanzania Wang Ke wakati wa uzinduzi wa maktaba mpya, kubwa na ya kisasa ya Kikuu cha Dar es Salaam

Rais wa Tanzania John Magufuli ametuma salamu kwa wapinzani Tanzania akiwaonya kuishia jela iwapo 'hawataheshimu sheria'.

Magufuli amempa salamu hizo waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa ambaye sasa ni kiongozi wa chama cha upinzani Chadema.

Magufuli na Lowassa walikutanaJumanne Novemba 27 katika ufunguzi wa maktaba ya kisasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

"Ninakupongeza sana (Lowassa). Hii ndiyo Tanzania mpya tunayoitaka. Vyama vyetu visiwe chanzo cha kututenganisha bali viwe chachu ya kuleta maendeleo," amesema Magufuli.

"Hii ndio Tanzania mpya tunayoitaka, "Nimeona hili nilizungumze kwa heshima kubwa, Mzee Lowassa ili wale unaowaongoza kule, uende ukawashauri, otherwise (lasivyo) wataishia magereza ili wakajifunze namna ya kuheshimu sheria za Watanzania."

Maktaba hiyo kubwa Afrika Mashariki na Kati ilijengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 93.6 ikiwa ni msaada kutoka Serikali ya China na ndiyo maktaba kubwa kuliko maktaba zote ambazo China imezijenga barani Afrika.

Majengo ya maktaba hiyo yenye ghorofa mbili yamechukua eneo lenye ukubwa wa meta za mraba 20,000 yakiwa na uwezo wa kuhifadhi vitabu 800,000, kukalisha watumiaji 2,100 kwa wakati mmoja.

Aidha, yana kompyuta 160 zilizounganishwa na mtandao kwa ajili ya kusoma vitabu kwa njia ya kielektroniki, ofisi za wafanyakazi, eneo la wanafunzi wenye mahitaji maalum na ukumbi wa kisasa wa mihadhara wenye uwezo wa kuchukua watu 600.

Haki miliki ya picha IKULU TZ
Image caption Lowassa na Magufuli walikutana Ikulu Januari 2018 kwa mara ya kwanza baada ya uchaguzi wa 2015

Magufuli alimwagia sifa Lowassa kuwa licha ya kumshinda kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 ameendelea kuwa mtulivu.

Haki miliki ya picha CHADEMA
Image caption Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (kulia) yupo mahabusu baada ya kufutiwa dhamana

Viongozi kadhaa wa upinzani Tanzania wakiwemo wa chama cha Chadema ambacho Lowassa ni mjumbe wa kamati kuu wanashtakiwa mahakamani kwa kwa kesi mbalimbali.

Wiki iliyopita, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alifutiwa dhamana pamoja na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko kutokana na kukiuka masharti ya dhamana katika kesi inayowakabili ya kufanya mikusanyiko kinyume cha sheria.

Mashtaka mengine yanayowakabili viongozi wa upinzani ni uchochezi na kutoa maneno yasiyofaa dhidi ya Rais.

Misaada ya Uchina

Katika hafla hiyo Magufuli pia aliwasifu Wachina kuwa wanatoa misaada isiyokuwa na masharti.

"China ni marafiki wazuri wametoa zaidi ya Bilioni 90 fedha za walipa kodi wao bila masharti, maana wengine wangetoa masharti. Naomba Balozi ufikishe asante zetu kwa Rais wenu, asante kwa wananchi wa China pia."

Haki miliki ya picha IKULU, TANZANIA

"Jambo la kufurahisha ni kwamba misaada yao haiambatani na masharti. Wenyewe wakiamua kukupa wanakupa, walitujengea TAZARA, URAFIKI na pia wametusaidia katika maeneo mengine ya maendeleo," alisema Rais Magufuli na kumhakikishia Balozi Wang Ke kuwa serikali ya Tanzania itahakikisha kila msaada unaotolewa unatumiwa vizuri.

Aliwataka wana Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhakikisha maktaba hiyo inatunzwa vizuri na kutoa wito kwa Watanzania kujifunza lugha ya Kichina katika jengo mojawapo la maktaba hiyo litakalokuwa likifundisha lugha hiyo kwa kuwa kuna manufaa makubwa kwa Watanzania kujifunza lugha hiyo.

Hivi karibuni Tanzania imekuwa ikipitia wakati mgumu kwenye suala la masharti ya misaada na mikopo.

Benki ya Dunia imezuia mkopo wa dola milioni 300 wa kuboresha elimu ya sekondari ikitaka serikali ya Tanzania ibadili sera yake ya kuzuia wanafunzi wa kike kuendelea na masomo baada ya kujifungua.

Serikali ya Denmark imezuia msaada wa dola milioni 10 baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kutoa kauli kali dhidi ya wapenzi wa jinsia moja.

Mada zinazohusiana