Mo Salah: Mchezaji nyota wa Misri aingilia kati mzozo wa paka na mbwa

Mo Salah selfie with his cats Haki miliki ya picha Mo Salah
Image caption Straika wa Liverpool Salah akiwa na mbwa wake

Mchezaji nyota wa kandanda Mo Salah amepinga vikali mipango ya nchi yake kuwasafirisha ughaibuni mbwa koko na paka shume kwa hofu kuwa wanaweza kugeuzwa kuwa kitoweo.

"Paka na mbwa hawatasafirishwa kwenda popote. Hilo haliwezi kutokea na halitatokea kamwe," nyota huyo ameandika kupitia ukurasa wake wa Twitter na kupakia picha akiwa na paka zake anaowafuga nyumbani.

Wapigania haki za wanyama wamekasirishwa na maamuzi hayo ya mamlaka za Misri na wametaka hatua hiyo ikomeshwe mara moja.

Paka shume na mbwa koko wapo kwa wingi katika mitaa ya Misri.

Mzozo huo ulianza juma lililopita baada ya Wizara ya Kilimo ya Misri kutangaza kuwa imeidhinisha kusafirishwa ughaibuni paka na mbwa 4,000.

Jumatano iliyopita, gazeti binafsi la al-Masry al-Youm liliripoti kuwa wizara hiyo ilianza kutoa vibali vya afya kusafirisha paka wapatao 2,400 na mbwa takribani 1,600.

Siku moja baadae, msemaji wa wizara alikiambia kituo cha runinga cha TenTV kuwa wanyama hao tayari wameshapigwa chanzo ya magonjwa mbalimbali na watassafirishwa kwa kufuata hatua zote za kisheria.

Vitu vya ajabu vilivyogunduliwa katika makaburi Misri

Mamlaka hata hivyo hazikuweka wazi kuwa wanyama hao wangesafirishwa kueleka nchi zipi na kwa matumizi gani.

Mshambuliaji huyo wa klabu kongwe ya Liverpool na timu ya taifa ya Misri ambaye ni maarufu sana nyumbani kwao na eneo lote la Mashariki ya Kati amejitosa rasni katika mzozo huo hii leo Jumanne (Novemba 27) akituma ujumbe wa twitter kupitia kampeni (hashtag) ya "hapana kwa uvunjavi wa haki za wanyama".

Watu wengi tayari wanampongeza kwa kupaza sauti yake.

Baadhi wametuma picha zao wakiwa na paka ama mbwa wanaowafuga na kuunga kampeni ya Mo Salah.

Lakini wengine wanaona Wamisri wana mambo mengi ya msingi ya mupambania, mmoja wao alishauri kuwa: "Kwanza tuangalie haki za binaadamu halafu ndio tuangalie haki za wanyama."

Mwezi uliopita, mwanasiasa Margaret Azir alizua sokomoko aliposhauri mamlaka zinenepeshe mbwa koko na kisha kuwasafirisha ughaibuni ikiwa ni namna bora ya kupambana na wanyama hao wanaokithiri kila uchao katika mitaa ya Misri.

Aliuambia mtandao wa gazeti binafsi la Youm7 kuwa katika baadhi ya nchi, mbwa "wanathamani kama ya kondoo".

Mourinho huenda akatembea kwenda Old Trafford

Ijumaa iliyopita serikali ya Misri ilisemaitatoa leseni ya kusafirisha na si kusafirisha wanyama hao yenyewe.

Msemaji wa serikali Hamed Abdel Dayem ameliambia gazeti la al-Hadath al-Youm ripoti kuwa wanyama wanasafirishwa kwenye nchi ambazo wataliwa hazina msingi wowote.

Hata hivyo, mbunge Nadia Henry tayari ameshawasilisha ombi bungeni ya kutungwa kwa muswada ambao utaharamisha usafirishwaji wa paka shume na mbwa koko.

Mada zinazohusiana