Vicensia Shule: Mhadhiri aliyezua mjadala wa rushwa ya ngono chuoni UDSM, Tanzania ni nani?

Dkt Vicensia Shule anasema ulinzi wa Dkt Magufuli ulimfanya anyamae Haki miliki ya picha HISANI
Image caption Dkt Vicensia Shule anasema ulinzi wa Dkt Magufuli ulimfanya anyamae

Mhadhiri mmoja katika Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) amezua mjadala mtandaoni baada ya kudai kwamba rushwa ya ngono imekithiri chuoni humo.

Dkt Vicensia Shule aliandika kwenye Twitter kwamba alitaka sana kuufikisha ujumbe wake kwa Rais John Magufuli lakini aliwaogopa walinzi wake.

Dkt Magufuli alikuwa amezuru chuo hicho kufungua maktaba mpya, kubwa na ya kisasa ya Kikuu cha Dar es Salaam iliyojengwa katika Kampasi Mlimani (Mwalimu. Julius K. Nyerere) jijini Dar es Salaam.

Maktaba hiyo kubwa Afrika Mashariki na Kati ilijengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 93.6 ikiwa ni msaada kutoka Serikali ya China na ndiyo maktaba kubwa kuliko maktaba zote ambazo China imezijenga barani Afrika.

Dkt Shule alitaka kutumia bango kuufikisha ujumbe kwa rais huyo.

Aliandika: "Baba @MagufuliJP umeingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kufungua maktaba ya kisasa. Rushwa ya ngono imekithiri mno UDSM. Nilitamani nikupokee kwa bango langu ila ulinzi wako umenifanya ninyamae. Nasubiri kusikia toka kwako maana naamini wateule wako ni waadilifu watakwambia ukweli."

Haki miliki ya picha TWITTER

Ingawa hakueleza ni rushwa ya aina gani iliyokithiri, katika vyuo vikuu vingine kumekuwepo na tatizo la wahadhiri na wanafunzi kutumia ngono katika kutoa alama katika mitihani.

Aidha, baadhi ya wahadhiri hutuhumiwa kudai ngono kutoka kwa wenzao ndipo wawapandishe vyeo vyuoni.

Tamko lake limezua mjadala mtandaoni, baadhi wakikubaliana naye na wengine kumwambia angetumia tu ujasiri na kutimiza azma yake.

Sure boY ameandika: "Ungelificha then ungemsuprize rais time anahutubia".

Wankisa Elias akasema: "ungemwonesha tuu kutimiza adhma yako...sikuingine punguza woga jembe".

Thobias Odhiambo: "Hatari sana! Sasa nimeelewa kwanini wahadhiri wengi hufa 'baada ya kuugua kwa muda mrefu". Ndugu zangu wahadhiri wa kiume (na wachache wa kike) tumrudie Mungu."

Kasiga Damaris anawataka wakuu walishughulikie tatizo hilo: "Ni changamoto haswaa ifanyiwe kazi watoto wa kike wanahitaji kusoma bila hizo sexual harassments (udhalilishaji wa kingono)."

Pascal Kupewa amemtaka awe jasiri: "Acha uoga mzee mwenzangu."

Hulk Jr Cresent anasema tatizo hilo halipo vyuoni pekee: "Hili nalo ni janga la taifa sio vyuoni pekeyake sehemu nyingi sana wadada/wamama wanakojarbu kupata ridhik/stahiki na hata wanakojarbu kuomba maombi mbalimbali, wenye majukumu ya kupitisha hayo maombi na vya mfano wake wengi wao hudai rushwa tajwa ili afanikishe lengo."

Dkt Shule ni nani hasa?

Ni mhadhiri katika kitivo cha Sanaa ya Ubunifu katika Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM). Ni mbunifu wa kutumia vitu ambavyo vilishatumika mara ya kwanza, mwandaaji wa filamu na pia msomi wa ngazi ya juu.

Alizaliwa mnamo 14 Machi 1978

Ana shahada ya udaktari katika Fani ya Sanaa ya Maonyesho kutoka chuo kikuu cha Johannes Gutenberg Universit├Ąt Mainz, Ujerumani alikosomea 2007-2010, kwa ufadhili wa kimasomo wa DAAD.

Tangu wakati huo amekuwa mhadhiri katika UDSM.

Alisomea shahada ya kwanza UDSM na baadaye akaendelea na masomo ya shahada ya pili katika chuo kikuu hicho kati ya 2002-2004.

Mwaka 2002, alitunukiwa tuzo ya mwanafunzi bora zaidi katika mitihani ya mwisho ya shahada ya kwanza katika Kitivo cha Sanaa katika UDSM.

Mwaka huo pia alishinda tuzo ya mwanafunzi bora wa sanaa wa mwaka wa mwisho chuoni kutoka kwa Baraza la Taifa la Sanaa (Basata).

Katika ukurasa wake wa Facebook, ameandika kwamba alisomea masomo ya upili katika shule ya Budalangi High

Alianza taaluma yake katika sanaa kama mwigizaji miongo miwili iliyopita.

Kwa muda sasa amekuwa akifanya kazi kama mwandaaji huru wa filamu na michezo ya kuigiza ya kuonyeshwa kwenye kumbi za sanaa, kusikilizwa redioni na kutazamwa kwenye televisheni.

Amekuwa akitafiti sana kuhusu masuala ya sanaa, vyombo vya habari, utamaduni na jinsia Tanzania na Afrika.

Ndiye mwanzilishi wa Mkulima Market, soko la mtandaoni la kutumiwa na wahudumu wa kilimo biashara nchini Tanzania, na pia ni mwanzilishi mwenza wa jarida la kisomi la Sanaa: Journal of African Arts, Media and Cultures kuhusu sanaa, vyombo vya habari na utamaduni.

Haki miliki ya picha TWITTER

Aidha, ndiye mwasisi wa Sanaa App, ambayo ni programu tumishi inayowaleta pamoja wabunifu Tanzania.

Yeye ni mtaalamu katika masuala ya jinsia na mwanaharakati ambaye amekuwa akitetea haki za wanawake Tanzania.

Ndiye mwenyekiti wa TGNP Mtandao, shirika linalotetea haki za wanawake, wadhifa ambao ameushikilia tangu mwaka 2015.

Shirika hilo, mtandaoni, limekuwa likishiriki katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili dhidi ya wanawake.