Ng'ombe mkubwa zaidi Australia kwa jina Knickers alivyookolewa na kimo chake

Knickers wagyu cattle Haki miliki ya picha Geoff Pearson
Image caption Knickers hufuatwa na ng'ombe wengine aina ya wagyu

Wapo mafahali, na kunaye huyu kwa jina Knickers. Ni kama jitu anaposimama pamoja na ng'ombe wengine malishoni au kwenye zizi.

Ni ng'ombe mnene ajabu. Knickers kwa Kiingereza maana yake ni suruali ya ndani ya mwanamke.

Uzani wake ni kilo 1,400kg na kimo chake 194cm (6ft 4in).

Ni ng'ombe mwenye miaka saba sasa na anaaminika kuwa ng'ombe mkubwa zaidi nchini Australia, taifa lililo na ng'ombe mamilioni.

Ukubwa wake umemuokoa. Mmiliki wake Geoff Pearson alipojaribu kumuuza kwenye mnada mwezi jana, wanunuzi wa ng'ombe wa kuchinjwa walikataa kumnunua.

Walisema ni mkubwa mno kiasi kwamba hawezi kutoshea vichinjioni, atawapa taabu tu.

Akarejeshwa nyumbani.

Sasa hatachinjwa, na ataishi maisha yake yaliyosalia katika shamba la kuwafuga ng'ombe wa kuchinjwa la Ziwa Preston eneo la Myalup, 136km (maili 85) kusini mwa mji wa Perth.

"Knickers ataishi," anasema Bw Pearson, ambaye amekuwa akipigiwa simu sana na wanahabari tangu alipoangaziwa na runinga ya taifa ya Australia.

Ng'ombe huyo ni wa aina ya Holstein Friesian, lakini ni mkubwa sana ukilinganisha na ng'ombe wa aina hiyo.

Alikuwa amenunuliwa mwanzoni kama ng'ombe kiongozi wa kuwaongoza wengine malishoni, akiwa na umri wa miaka 12.

Alishahasiwa, maana kwamba hawezi kutungisha mbegu.

"Alikuwa ng'ombe wa kipekee tangu mwanzo, ni mkubwa kuliko wengine," anasema Bw Pearson.

Ingawa wenzake walipelekwa kichinjioni mapema, "alikuwa wa kipekee hivyo tukaamua aendelee kubaki hapa."

"Huwa hamwumizi yeyote," anasema.

Baada yao kununua na kuwauza ng'ombe wengine, wafugaji hao wa ng'ombe waligundua kwamba alikuwa haachi kunenepa.

Sasa amekuwa mkubwa kiasi kwamba hawezi kuuzwa.

Bw Pearson - anayemiliki ng'ombe 20,000 hivi - anasema Knickers ana miaka mingine kadha ya kuishi.

Hupendwa sana na ng'ombe wengine, ambao anasema humfuata zizini.

Wengi ni wa aina ya wagyu na ni wa rangi ya hudhurungi iliyokoza. Knickers ambaye ni wa rangi nyeusi na nyeupe ni wa kipekee zizini kutokana pia na rangi yake.

Jina lake lilitoka wapi?

"Alipokuwa mdogo, tulipomnunua, tulikuwa na fahali aina ya Brahman aliyekuwa rafiki yake," anasema Bw Pearson. "Jina lake lilikuwa Bra (sidiria)... kwa hivyo [tukawa na] Bra (sidiria) na Knickers (suruali ya ndani ya mwanamke).

"Hatukudhani atakuwa suruali kubwa sana."

Kwa mujibu wa vitabu vya rekodi duniani, ng'ombe mrefu zaidi kuwahi kuishi alikuwa Bellino - aliyekuwa na kimo cha 2.027m alipopimwa mwaka 2010 nchini Italia.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii