Mzozo wa Ukraine-Urusi: Trump huenda akafutilia mbali mazungumzo kati yake na Putin katika mkutano wa G20

Baadhi raia wa Ukraine waliyokamatwa wamefikishwa mahakamani katika jimbo la Crimea Haki miliki ya picha AFP
Image caption Baadhi raia wa Ukraine waliyokamatwa wamefikishwa mahakamani katika jimbo la Crimea

Rais wa Marekani Donald Trump amesema huenda akafutilia mbali mkutano baina yake na rais wa Urusi Vladimir Putin kufuatia mzozo kati ya taifa hilo na Ukraine.

Trump ameliambia gazeti la Washington Post kuwa anasubiri "ripoti kamili" baada ya Urusi kuvurumiza moja ya meli ya Ukraine na kuteka zingine tatu siku ya Jumapili.

Ukraine inasema hiyo ni ''hatua ya uchokozi', huku Urusi nayo ikisema meli hizo ziliingia kiharamu katika mipaka yake majini.

Sheria ya kijeshi imewekwa katika baadhi ya sehemu ya Ukraine.

Huku hayo yakijiri Marekani imetoa wito kwa mataifa ya Ulaya kuisaidia Ukraine.

Mzozo wa sasa umezuka vipi?

Siku ya Jumapili meli za kivita za Berdyansk na Nikopol, pamoja na meli ya kuzisindikiza Yana Kapa, zilijaribu kusafiri mji wa bandarini kwenye Bahari Nyeusi wa Odessa kuelekea Mariupol katika Bahari ya Azov.

Ukraine inasema Urusi ilijaribu kuzizuia meli hizo zisiendelee na safari yake, ambapo meli moja iliigonga meli ya Yana Kapa.

Meli hizo ziliendelea na safari kuelekea mlango wa bahari wa Kerch, lakini zikapata njia imezibwa na meli moja kubwa.

Urusi wakati huo ilikuwa imetuma ndege mbili za kivita na helikopta mbili ambazo zilikuwa zikipaa angani katika eneo hilo na kufuatilia mwenendo wa meli hizo.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Volodymyr Lisovyi ni mmoja wa wanaume watatu waliyotoa taarifa kwa lazima kwa mkuu wa jeshi la maji la Ukraine

Urusi inaituhumu Ukraine kwa kuingia kinyume cha sheria katika maeneo yake ya bahari na usafiri eneo hilo umesitishwa kwa muda usiojulikana kwa sababu za kiusalama.

Jeshi la wanamaji la Ukrane lilisema meli hizo zilikuwa zimeshambuliwa na kuharibiwa zilipokuwa zinajaribu kuondoka eneo hilo.

Imesema wahudumu wake sita wamejeruhiwa.

Ukraine imejibu vipi hatua ya Urusi?

Siku ya Jumanne, Rais Petro Poroshenko alisema kuna tishio la ''vita kamili" kati yetu na Urusi.

"Idadi ya magari ya kivita ya Urusi yameongezeka katika mara tatu zaidi katika kambi yake ya mpakani," alisema.

Usiku ya Jumatatu, bunge la Ukraine liliunga mkono auamuzi wa rais Poroshenko wa kuweka sheria ya kijeshi kwa siku 30 katika maeneo 10 ya mpakani kuanzia Novemba 28.

Uchanganuzi wa Steven Rosenberg, BBC News, Moscow

Uhasama kati ya Russia na Ukraine umekuwa ukiongezeka kwa miezi kadhaa katika rasi ya Crimea.

Chini ya mkataba wa mwaka 2003 kati ya Moscow na Kiev, mlango wa bahari wa Kerch na Bahari ya Azov huchukuliwa kama maeneo ya pamoja.

Hata hivyo, karibuni, Urusi ilianza kuzikagua meli zote zilizokuwa zikisafiri kuingia au kutoka bandari za Ukraine.

Hatua ya Urusi kutumia nguvu kuzitwaa meli hizo za Ukraine - pamoja na mejeruhi - ni hatua inayozidisha zaidi uhasama.

Lakini hauwezi kutarajia Urusi wakubali lawama.

Chini ya Rais Vladimir Putin, Urusi ilipotumia nguvu awali, imekuwa ikijitetea na kusema: "Si sisi tulioanzisha haya."

Walifanya hivyo wakati wa vita vya Urusi na Georgia mwaka 2008 na pia kushiriki kwa wanajeshi maalum wa Urusi Crimea mwaka 2014, hatua iliyotangulia kutekwa kwa rasi hiyo ya Crimea na Urusi.

Kwa hivyo, tarajia Urusi imlaumu Rais Poroshenko na serikali yake kwa yaliyotokea Jumapili na yote yatakayofuata.

Hatua ya sasa ya Urusi imepokelewaje viongozi wa kimataifa?

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo amesema hatua ya kutekwa kwa meli ya Ukraine ni "ni hatari na ni ukiukaji wa sheria ya kimataifa".

Uingereza imelaani mienendo ya Urusi katika kanda ya ulaya na kutaja ''mzozo unaoendelea sasa ni ukandamizaji wa uhuru wa eneo la serikali ya Ukraine".

Akizungumza kwa njia ya simu na Chansela wa Ujerumani Angela Merkel, rais wa Urusi Vladimir Putin aalihoji kuwa Waukrainia walikuwa wamepuuza "makusudi sheria ya amani katika eneo lake", Kremlin ilisema.

Bi Merkel alisema "Kuna haja ya kutuliza mzozo huu na kukaribisha majadiliano," amesema msemaji wake.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii