Dhamana ya Freeman Mbowe na Esther Matiko yakwama, waendelea kusota rumande

Freeman Mbowe na Esther Matiko
Image caption Wabunge Freeman Mbowe na Esther Matiko wamekata rufaa Mahakama kuu kupinga kufutiwa dhamana

Mwenyekiti wa chama cha upinzani Chadema na kiongozi wa kambi ya upinzani Freeman Mbowe anatarajiwa kujua hatima ya dhamana yake kesho Alhamisi (Novemba 28).

Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai pamoja na mbunge wa Tarime Mjini Esther Matiko wanasota rumande toka Novemba 23 baada ya kufutiwa dhamana zao baada kutohudhuria mahakamani katika siku ambazo kesi yao ilikuwa ikitajwa.

Baada ya kufutiwa dhamana, Mbowe na Matiko wamekata rufaa juu ya uamuzi huo na leo hii rufaa yao ilikuwa isikilizwe lakini ilikwama kutokana na kutokuwepo kwa mwenendo wa uamuzi wa kuwafutia dhamana uliotolewa na Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri.

Kesi hiyo ya rufaa sasa imepangiwa kusikilizwa kesho katika Mahakama Kuu chini ya jaji Sam Rumanyika.

Wabunge hao wawili wamerejeshwa katika gereza la Segerea ambapo wanashikiliwa toka Ijumaa ya wiki iliyopita.

Onyo la Magufuli

Jana, rais wa Tanzania, John Magufuli alituma salamu kwa wapinzani Tanzania akiwaonya kuishia jela iwapo 'hawataheshimu sheria'.

Magufuli alimpa salamu hizo waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa ambaye sasa ni kiongozi wa chama cha upinzani Chadema walipokutana katika ufunguzi wa maktaba ya kisasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Haki miliki ya picha IKULU TZ

"Ninakupongeza sana (Lowassa). Hii ndiyo Tanzania mpya tunayoitaka. Vyama vyetu visiwe chanzo cha kututenganisha bali viwe chachu ya kuleta maendeleo," alisema Magufuli.

"Hii ndio Tanzania mpya tunayoitaka, "Nimeona hili nilizungumze kwa heshima kubwa, Mzee Lowassa ili wale unaowaongoza kule, uende ukawashauri, otherwise (lasivyo) wataishia magereza ili wakajifunze namna ya kuheshimu sheria za Watanzania."

'Makosa' ya Mbowe na Matiko

Hakimu Mashauri alifuta dhamana ya wawili hao Ijumaa iliyopita kwa "kudharau maamuzi ya mahakama."

Mbowe alishindwa kuhudhuria mahakamani tarehe 8 November 2018 baada ya kuugua ghafla na kwenda Afrika kusini kwa matibabu.

Mwezi Oktoba 28,alielekea Washington DC Marekani kuhudhuria mkutano na aliporejea tarehe 31 Oktoba aliugua ghafla.

Matiku alishindwa kuhudhuria mahakamani baada ya kwenda kwenye ziara ya wabunge nchini Burundi.

Sababu zote hizo, zilikataliwa kwa madai ya kutokidhi matakwa ya kushindwa kufika mahakamani.

Mbowe na Matiko wanashtakiwa katika kesi ya msingi pamoja na wabunge wengine wa Chadema kwa Uchochezi na kuitisha maandamano bila kibali.

Upinzani washikamana

Katika hatua nyengine viongozi wa vyama vyengine vya upinzani, CUF na ACT Wazalendo walijitokeza mahakamani hapo kuungana na wenzao wa Chadema kama alama ya mshikamano.

Joram bashange, naibu katibu mkuu CUF Tanzania Bara amesema kauli ya jana ya Magufuli imezidi kuwaunganisha.

"Upinzani tumeona tuongeze nguvu yetu ya umoja kwasababu hii vita si ya kwetu peke yetu. Kauli ya jana ya Rais, inatuthibitishia kuwa sasa kuna mpango wa kutukandamiza na wanaandaa sheria ambayo ni kanuni ya adhabu kwa vyama vya siasa , na inabidi tujiandae kukabiliana nao."

Mada zinazohusiana