Daktari mlevi afanya upasuaji ulioua mama na mtoto nchini India

Representational image Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mama na mtoto walifariki muda mfupi baada ya upasuaji

Daktari mmoja katika jimbo la Gujarat nchini India amekamatwa na polisi baada ya kumfanyia upasuaji mama mjamzito akiwa amelewa.

Polisi wameiambia BBC kuwa mtoto alifariki punde tu baada ya upasuaji, na mama akafuatia baada ya muda mfupi.

Kipimo cha pumzi ya mdomo baadae kilithibitisha kuwa daktari aliyefanya upasuaji alikuwa amelewa.

Hata hivyo uchunguzi bado unaendelea kubaini chanzo cha vifo hivyo kama ni uzembe ama sababu nyengine za kitabibu.

Daktari PJ Lakhani ni tabibu mwandamizi mwenye uzoefu wa kutosha na amekuwa akihudumu kwenye hospitali ya serikali ya Sonavala kwa miaka 15.

Mjamzito, Kamini Chachi, alipelekwa hospitali siku ya Jumatatu baada ya kupata uchungu.

Vyombo vya habari vya ndani vinaripoti kuwa familia yake ambayo ilikuwa inasubiria habari njema iliarifiwa kuwa mtoto amefariki, na mama alikuwa akivuja damu sana.

Familia hiyo iliamua kumhamishia katika hospitali binafsi, lakini hakufika, alifia njiani.

Polisi pia imeambia BBC kuwa Dkt Lakhani aliwapigia simu kuwaomba msaada kutokana na hofu kuwa familia ya marehemu ingemshambulia mara baada ya vifo hivyo kutokea. "Tulimkuta akiwa amelewa, ndio maana tukamkamata," amesema ofisa wa polisi HR Goswami.

Tayari kamati ya uchunguzi imeshaundwa ili kulipeleleza zaidi tukio hilo wakati huu ambao Dkt Lakhani akiwa mikononi mwa polisi.

Mada zinazohusiana