Sababu zilizochangia benki tano kupigwa marufuku ya kubadilisha fedha za kigeni Tanzania

Noti za Tanzania
Image caption Noti za Tanzania

Benki Kuu ya Tanzania imezipiga benki tano marufuku ya kuendesha biashara ya sarafu za kigeni kwa muda wa mwezi mmoja kwa kukiuka sheria kwa mujibu wa maafisa wa vyeo vya juu.

Marufuku hiyo inakuja baada ya Benki Kuu kufanya ukaguzi wa ghafla kwenye maduka ya kubadilisha fedha za kigeni kwenye mji ulio kaskazini wa Arusha kituo cha utalii na bishara ya madini.

Kwa sasa kuna zaidi ya benki 40 zinazotoa huduma kwenye taifa hilo la Afrika Mashariki.

Kwa nini zimepigwa marufuku?

Benki ya Barclays Tanzania, Exim Bank, UBA Bank, BancABC na Azania Bank zote zilipigwa marufuku ya kuendesha biashara hiyo Novemba 23 kwa kukiuka sheria za biashara, kwa mujibu wa Alexander Ng'winamila, mkurugenzi wa masoko ya fedha katika benki kuu.

"Benki zilizopigwa marufuku aidha zilifanya biashara nje ya viwango vya masoko au hazikuwasilisha kwa Benki Kuu rrekodi za biashara zao, suala ambalo ni kinyume na sheria," Ng'winamila aliliambia shirika la Reuters.

Barclays Tanzania ambayo ni sehemu ya beki ya Afrika Kusini Absa, ilithibitisha marufuku hiyo na kuongeza kuwa ilikuwa inashirikiana na benki kuu kutatua suala hilo.

Benki zimesema nini?

Gilbert Mwandimila, mkurugenzi wa biashara kwenye benki ya Azania amesema changamoto za teknolojia zilichangia kuchelewa kwa ripoti kuhusu biashara ya fedha.

Alisema marufuku ya mwezi mzima itaathiri pakubwa uwezo wa benki kuhudumia wateja.

Stanley Kafu, mkuu wa masoko na mawasiliano Benki ya Exim Tanzania, aliiambia Reuters kuwa marufuku ya benki ya Exim inahusu biashara kati ya dola ya Marekani na shilingi ya Tanzania pekee.

"Tumeruhusiwa kufanya biashara ya sarafu zingine kuu na pia tunaruhusiwa kuendelea na huduma zingine za benki," alisema.

Thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola

Thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani imezidi kuporomoka na kufikia kiwango cha chini zaidi katika miaka mitatu iliyopita.

Dola moja kwa sasa ni wastani wa Sh2,300 mara ya mwisho kwa kiwango hicho kufikiwa ilikuwa ni Julai 2015 ambapo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliingilia kati.

Mkurugenzi wa Masoko na Fedha wa BoT Alexander Mwinamila aliliambia Gazeti la The Citizen la Tanzania kuwa kuporomoka huko kwa thamani ya shilingi kulitarajiwa.

"Hali ya sasa si kitu cha kustaajabisha, na kwa kiasi imechangiwa na kuimarika kwa dola dhidi ya sarafu nyengine kwa siku za hivi karibuni."

Sababu nyingine zinazotajwa kuchangia kuporomoka huko kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ni kushuka kwa mauzo ya bidhaa nje ya nchi na kuingia kwa fedha za kigeni kutoka kwenye miradi ya wawekezaji.

Hata hivyo, wakati shilingi ikishuka, tarehe 19 Novemba mwaka huu katika hali isiyokuwa ya kawaida, wanajeshi walitanda kwenye maduka ya kubadilishia fedha jijini Arusha.

Hali iliyowafanya baadhi ya wananchi washindwe kufanikisha biashara waliyokusudia.