Tanasha Donna Oketch: Mkenya huyu 'anayependwa' na mwanamuziki Diamond Platnumz ni nani hasa?

Tanasha Donna Haki miliki ya picha TANASHA DONA/Instagram

Mwanamuziki nyota wa Tanzania Diamond Platnumz alitangaza kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram kwamba alikuwa katika uhusiano wa kimapenzi na Mkenya.

Platnumz Novemba alipakia video kuashiria kwamba alikuwa kwenye mahaba na dada kwa jina Tanasha Donna Oketch, na tangu wakati huo ikawa ni mapenzi hadharani.

Katika mitandao ya kijamii, picha zilisheheni. Lakini sasa, nyingi ya picha hizo zimefutwa na Tanasha mwenyewe ameandika ujumbe kwenye Instagram kwamba wawili hao wameafikiana kuweka faraghani mambo mengi kuhusu uhusiano wao.

Miongoni mwa picha za karibuni za wawili hao zilizoondolewa mitandaoni ni ya Jumatatu wakiwa safarini kurejea Dar es Salaam kutoka Mwanza baada ya Diamond kuachwa na ndege Jumapili.

Diamond alikuwa ameandika alivyofurahishwa na huduma wakati huo, baada ya kuzozana na Air Tanzania siku nzima kuhusu kuachwa kwake na ndege Mwanza.

Haki miliki ya picha Instagram

Bi Oketch, ni mtangazaji katika kituo cha redio cha NRG nchini Kenya.

NRG ni miongoni mwa vituo vipya vya redio nchini Kenya ambavyo vimekuwa vikilenga kuwavutia zaidi vijana.

Diamond, ambaye jina lake halisi ni Naseeb Abdul Juma, kwenye video ya Insta Stories Jumanne aliandika kuwa: "Maskini simba yuko kwenye mapenzi…Mmwamini, yupo kwenye mapenzi."

Mwanamuziki huyo kwa utani hujiita Simba au Chibu Dangote.

Video inayoonyesha vivuli vya wanaoaminika kuwa yeye na Tanasha wakitembea ufukweni inaonesha ujumbe wa "I love you Tanasha" (Nakupenda Tanasha) ambayo yameandikwa mchangani.

Diamond, ambaye amevuma kwa nyimbo kama vile Number One, Sikomi, Mawazo, Kamwambie, Nana, Mdogo Mdogo, na Ntampata Wapi, anasikika akisema: "Anapendeza hata kivulini." Mwanamuziki huyo amekuwa na tamasha kubwa la muziki la Wasafi Festival eneo la Mtwara, mji wa pwani ulio kusini mashariki mwa Tanzania.

Mwanamuziki huyo pia amewashirikisha wanamuziki wengine katika nyimbo maarufu kama vile Kwangwaru, Zilipendwa, African Beauty, Make Me Sing na wa karibuni zaidi Mwanza akiwa na Rayvanny ambao umefungiwa na Baraza la Sanaa Tanzania (Basata).

Mwanamuziki huyo kwenye video yake ya Instagram ameonekana kuwakosoa wapenzi wake wa awali akisema: "Hawakunichukilia kwa uzito. Nilipowahitaji, walinipuuza. Eti mimi ni mtu wa kuwacheza…lakini yeye ameniamini...!"

Bi Oketch mwenyewe bado hajazungumzia taarifa hizi za uhusiano baina ya wawili hao hadharani, jambo linaloibua maswali kuhusu iwapo kweli ni mapenzi, au 'kutafuta'.

Kwenye Instagram, picha zake za karibuni zaidi zimeonekana kupigia debe NRGTAKEOVER, inayoonekana kuwa kipindi cha redio ambapo wasikilizaji watakuwa wakizawadiwa.

Katika ujumbe mmoja, aliandika: "Chilling here waiting on that #NRGTAKEOVER like.." (Nimetulia hapa nikisubiri #NRGTAKEOVER hivi…"

Je, kuna uwezekano kwamba video za Diamond ni za kuvumisha kipindi hicho au labda kitu kingine wanachofanya kwa ushirikiano?

Hilo litabainika kadiri siku zinavyosonga! Mapenzi wenyewe walisema hayafichiki.

Tanasha Donna Oketch ni nani?

Jina lake kamili ni Tanasha Donna Barbieri Oketch lakini pia wakati mwingine mitandao ya kijamii hujiita Zahara Zaire.

Amezaliwa na wazazi wa asili mbili, Mkenya na Mwitaliano na amekuwa mwanamitindo kwa kipindi kirefu.

Haki miliki ya picha Tanasha Donna/Instagram

Alizaliwa Uingereza lakini akahamia Kenya alipokuwa na umri wa miaka miwili ambapo alikulia Kenya hadi alipokuwa na miaka 11 alipohamia Ulaya.

Huko, alipata fursa ya kushiriki katika shughuli za mitindo ya mavazi na maonesho mbalimbali.

Ameshiriki katika mashindan mbalimbali yakiwemo Miss Africa Belgium lakini aliambia chombo kimoja cha habari kwamba alitaka kurejea "nyumbani" na kushiriki shindano la Miss World Kenya, ndipo awakilishe taifa lake la kuzaliwa.

Akiwa Ubelgiji, alisomea somo la utalii.

Anaweza kuzungumza lugha tano ambazo ni Kiingereza, Kiswahili, Kifaransa, Kiholanzi na Kihispania.

Ingawa jamaa zake wengine wanaishi Kenya, mamake alisalia Ubelgiji, na kwa mujibu wa mtandao wa Tapmagonline, kwa sasa ana umri wa miaka 22 hivi.

Tanasha pia ni mwigizaji na mwanamuziki na ana kampuni yake ya nywele kwa jina 'For Her Luxury Hair' ambayo ndiye mwanzilishi wake na afisa mkuu mtendaji. Ni kampuni huuza nywele za binadamu.

Bi Oketch alikuwa na uhusiano na mwigizaji Mkenya, Nick Mutuma, ambaye jina lake kamili ni Nicholas Munene Mutuma.

Uhusiano wao ulifikia tamati mwanzoni mwa mwaka 2017, ambapo Bi Oketch alisema kwamba walikuwa watu "wasiopatana na wasiochukuana" na ndio maana wakaachana.

Bi Oketch, alishirikishwa kama video vixen kwenye video ya wimbo wa Ali Kiba na Christian Bella kwa jina "Nagharamia".

Mapema mwaka huu, alipuuzilia mbali tetesi kwamba alikuwa na uhusiano na mwanamuziki huyo.

"Kiba na mimi wakati mmoja tulifanyia kazi video ya muziki, lakini hatujawahi kuwa na uhusiano," alisema kwenye Instagram.

Kiba aadaye alifunga ndoa na Mkenya Amina Khaleef.

Baada ya video za Diamond kupakiwa Instagram, wafuasi wake wamekuwa wakimfuata kwa wingi Bi Oketch na kumuandikia ujumbe mbalimbali katika ukurasa wake ambapo kufikia sasa ana wafuasi zaidi ya 107,000.

Alitangaza kwamba atakuwa na kipindi cha redio katika kituo cha NRG akiwa pamoja na DJ Kace Aprili mwaka huu.

Diamond Platnumz na Kim Nana, Zari na wengine

Diamond kwa muda alikuwa na uhusiano na mzazi mwenzake Hamisa Mobetto.

Huwezi kusikiliza tena
Zari aeleza sababu za kumtupa Diamond

Hii ni baada ya uhusiano wake wa awali na raia wa Uganda Zari Hassan, ambaye ni mama wa watoto wake wawili kufikia kikomo Siku ya Wapendanao Februari mwaka huu.

Baada ya kuhusishwa kwa muda na Hamisa, Diamond alijitokeza na kusema kwamba hakuwa na uhusiano na mwanamke yeyote.

Kuna utata kwa sasa ikizingatiwa kwmaba mapema mwezi huu mamake Diamond, Sanura Kassim, alikuwa amethibitisha kwamba mwanawe alikuwa na uhusiano na mwanamke kwa jina Kim Nana, ambaye jina lake halisi ni Lilian Kessy.

Kim Nana ni video vixen pia, na mamake Diamond aliashiria kwamba mwanawe huyo amemshawishi mwanamke huyo kubadili hata dini yake kutoka Ukristo hadi Uislamu, wakijiandaa kufunga ndoa.

Diamond aliwahi pia kuwa na uhusiano na Miss Tanzania wa mwaka 2006 wema Sepetu.

Mada zinazohusiana