Jinsi kupika na kazi zingine za nyumbani zimebadili tabia za wanaume Rwanda

Man holding baby Haki miliki ya picha Elaine Jung
Image caption Jean Pierre, 32, lives in Mwulire in Eastern Province in Rwanda

Programu ya mashinani inajaribu kupunguza ghasia za nyumbani nchini Rwanda kwa kuwafunza wanaume jinsi ya kufanya kazi za nyumbani na utafiti wa hivi majuzi unaonyesha kuwa programu hii imekuwa ya manufaa kwenye jamii.

Muhoza Jean Pierre alikuwa anampiga sana mke wake. Alimuona kama mtu ambaye alimuoa kumzalia watoto na kuwalea.

"Nilikuwa nafuata mfano wa baba yangu. Baba yangu hakuwa akifanya chochote nyumbani," alisema.

"Kama ningekuja nyumbani na kupata kuna kitu hakikuwa kimefanywa, ningemdhulumu.

"Ningemuita mvivu, nimuambie hana maana na anastahili kurudi kwa wazazi wake."

Lakini kitu fulani kikabadilika - akajifunza jinsi ya kupika na kuosha.

Ilkikuwa sehemu ya programu katika kijiji chake cha Mwulire mkoa ulio mashariki mwa Rwanda, ambayo huwawezesha wanaume kutekeleza majukumu ya nyumbani ikiwemo kuwaangalia watoto.

Jean Pierre anasema mradi huo unajulikana kama 'Bandebereho', ulisaidia kubadili tabia yake.

Alihudhuria mafunzo ya ziada ambapo alifunzwa jinsi ya kupika, kusafisha na mafunzo kuhusu namna ya kuyakabili majukumu ya kitamaduni.,

Haki miliki ya picha Elaine Jung
Image caption Jean Pierre na mke wake wameona kwa miaka kumi

"Wangetuuliza kama mwanamume anaweza kufagia nyumba, na tungejibu ndio anaweza," alisema.

"Kisha watatuuliza: Yupi kati yenu anafanya hivyo? na hakukuwa na yeyote."

'Hakuna mwanamume kamili anaweza kupika'

Waalimu kutoka 'Bandebereho' walimfunza Jean Pierre jinsi ya kufanya kazi ambazo awali aliamini kuwa ni mke wake tu angefanya.

Aliongeza: Tungeenda nyumbani na kujaribu kufanya yale tulifunzwa.

Kisha tunarudi kwa mafunzo na mashuhuda ambao wangesema ikiwa waliona mabadiliko yoyote kwetu.

"Ninajua kupika. Kuosha watoto, ninajua jinsi ya kuponda muhogo na kuchunga unga."

Hata hivyo kufanya mabadiliko kama hayo hakikuwa kitu rahisi kwa kuwa marafiki zake Jean Pierre, walimshauri asifanye kazi za nyumbani, wakimuambia: Mwanamume kamili hapiki'.

Familia yangu na marafiki walianza kusema kuwa mke wangu alikuwa amenipa dawa... wangeniambia kuwa hakuna mwanamume kamili anaweza kubeba kuni barabani, alisema.

Lakini Jean Pierre aliendelea wakati aliona mafanikio kwa familia yake.

Alisema watoto wake wana uhusiano wa karibu naye na mke wake kwa sasa anaendesha biashara ya ndizi hali ambayo imeboresha zaidi maisha yao.

Haki miliki ya picha Elaine Jung
Image caption Mradi 'Bandebereho' ulimfunza Jean Pierre kufanya kazi za nyumbani

"Jinsi mke wangu hunitendea ni tofauti na vile alilkuwa akinitendea awali," alisema.

Alikuwa ananitendea vibaya kwa sababu hata mimi nilikuwa ninamtendea vibaya, lakini kwa sasa tunazungumza na kukubaliana kuhusu mambo ya kufanya.

Hofu na uhuru

Mke wake Jean Pierre Musabyimana Delphine anasema alikuwa na uhuru kidogo na aliishi kwa hofu.

Anasema: Wakati mwingine nilihisi kama mimi ni mfanyakazi tu, lakini ningekumbuka kuwa mfanyakazi huwa na mashahara.

Singefikiri kuwa mwanamke angekuwa na pesa zake, kwa sababu sikuwa na hata muda wa kufikiria kuhusu shughuli yoyote ambayo ingeweza kunipa pesa.

"Sasa nina uhuru nyumbani ninaweza kutoka na kutengeneza pesa kama mtu yeyote."

Delphine hutoka nyumbani saa 11 asubuhi kwenda kuuza ndizi sokoni huku Jean Pierre akibaki nyumbani kuwaangalia watoto wao wanne.

Ninarudi nyumbani nikiwa mtulivu na kupata chakula tayari, alisema.

Kituo cha wanaume cha Rwanda kilichoileta programu hiyo nchini sasa kinataka 'Bandebereho' kutumiwa zaidi na jamii na serikali ya nchi hiyo.