Kimutai Kemboi :Niliathirika na virusi vya Ukimwi kwa kushiriki ngono na mwanamke mwenye umri mkubwa

Kimutai Kemboi
Image caption Kimutai Kemboi , mwanafunzi wa chuo kikuu anayeishi na virusi vya ukimwi

Wakati dunia inaadhimisha siku ya ukimwi, ikiwa ni miaka 30 tangu harakati za uhamasishaji wa masuala kuhusu ukimwi. Mwaka huu watu wanaendelea kuhimizwa kufahamu hali zao za kiafya.

Kimutai Kemboi mwenye umri wa miaka 27 ni mwanafunzi wa chuo kikuu anayeishi na virusi vya ukimwi na aliathirika na virusi hivyo akiwa na umri wa miaka 22 wakati yuko shule ya upili.

Alisoma akiwa na umri mkubwa kutokana na ukosefu wa karo.

Kemboi alikuwa akiishi vijijini na baada ya muda aliamua kusafiri hadi katika jiji kuu la Nairobi, Kenya ili ajitafutie riziki kukimu maisha yake na kutimiza ndoto yake ya kuendeleza masomo yake.

Katika kutimiza ndoto zake alikutana na mwanamke mwenye umri wa miaka 40, aliyekuwa na watoto wawili ambaye alimuahidi kumsaidia na baada ya muda, wawili hao wakaaza kuwa na uhusiano wa karibu.

''Siku moja aliniuliza kwa undani kuhusiana na maisha yangu, nikamuelezea kwa uwazi kwani nilitaka kusaidiwa'', Kemboi alisema

Baada ya mazungumzo hayo mwanamke huyo akamwambia iwapo angetaka kusaidiwa basi lazima atekeleze masharti yake.

''Nilichanganyikiwa na sikujua ni masharti gani hayo, siku moja akaniuliza iwapo nimeamua kuyafuata masharti hayo kwa sababu sikuwa na la kufanya nikamwambia ndio.

Akaniambia tufanye tendo la ndoa na sikutumia kinga yoyote, niliweza kujielewa baada ya kufanya ngono naye na nilifanya tendo hilo mara moja pekee.''

Mwanamke huyo alipoteza kazi yake na Kemboi aliamua kujitafutia riziki sehemu nyengine na akaondoka kwa nyumba hiyo na kutafuta usaidizi kwingine bila ndoto yake ya kuendelea na masomo kutimia.

Baada ya miaka miwili Kemboi aliamua kujua hali yake ya kiafya, lakini hakuwa na dalili zozote za ugonjwa wowote.

'Nilipokuwa naenda kupimwa nilijua hali yangu ni salama. Nilipoangalia matokeo nilipatwa na mshtuko kwamba niko na virusi vya ukimwi, lakini nikajipa moyo kwamba kifaa cha kupimia labda kilikuwa na hitalafu.

Nilirudi nyumbani kutafakari zaidi na baada ya muda nikarudi kupimwa kwa mara nyingine na matokea yalibaki kuwa hayo hayo na nikarudia mara nne au tano hivi ndipo nikakubali kwamba nina virusi hivyo'' Kemboi amesema.

Kwa Kemboi alichukua muda wa mwaka mmoja ndipo akaanza matumizi ya dawa kwa kuwa alifahamu kwamba dawa hizo zilikuwa na madhara kadha wa kadha.

Kemboi amesema aliifahamisha jamii yake kupitia kaka yake mkubwa na familia ilishtuka lakini walikubali na hivi sasa wanampatia motisha katika maisha yake.

Image caption Mshauri wa kituo cha Dream Centre ,Grace Makani

Kulingana na mshauri mkuu wa kituo kinachoshungulia watu wenye virusi vya ukimwi cha Dream Centre kilichoko eneo la Langata jijini Nairobi Grace Makani, amesema vijana wengi wanapatwa na virusi hivi vya ukimwi kwani jamii nzima imeshindwa kuwalewa watoto.

Bi. Makani amesema watoto wa siku hizi ndio wanaojiamulia kile wanachotaka kuhusiana na maisha yao na pia wazazi hawana uwazi wakuzungumzia juu ya mapenzi na virusi vya ukimwi majumbani mwao.

Wakati vipindi vikipeperushwa kuhusiana na mapenzi au virusi vya ukimwi wazazi huvidharau.

Kimo chako huenda kinakuweka katika hatari

''Hatuna uwazi kwa watoto wetu kwa kuwaelezea kwamba virusi vya ukimwi vinapatikana kwa kupitia ngono ya kiholela holela.''

Image caption Dkt. Margret Wanjiru anayewashungulia wagonjwa wa virusi vya ukimwi jijini Nairobi

Daktari Margret Wanjiru wa kituo cha Dream Centre amesema mtu mwenye virusi vya ukimwi anaweza kuishi kama kwa miaka yoyote ile bora afuate maelezo ya daktari na atumie dawa kwa wakati ufaao.

Wanjiru amesema wakati huu kuna wanandoa wengi wanaoishi mmoja akiwa na virusi hivyo vya HIV na wameishi kwa muda mrefu.

''Wanandoa hao huwahimiza kutumia kinga na endapo wanataka kupata mtoto basi tunawapa dawa ili mtoto azaliwe bila virusi hivyo.''

Dkt Wanjiru amesema anakumbana na wagonjwa ambao hawataki kunywa dawa kwa madai kwamba wameombewa na wakapona lakini tunawapa ushauri kwamba dawa ni muhimu na hata wengine tunawapima kwa mara nyingine kuwadhihirishia kwamba bado wanaugua ugonjwa huo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii