Hezron Mogambi: Kitendawili cha usawa wa jinsia na wasiwasi wa Bunge kuvunjwa Kenya

Watetezi wa usawa wa jinsia walitetea kuwakilishwa kwa wanawake hata wakati wa kuandaliwa kwa Katiba Mpya Haki miliki ya picha AFP/Getty Images
Image caption Watetezi wa usawa wa jinsia walitetea kuwakilishwa kwa wanawake hata wakati wa kuandaliwa kwa Katiba Mpya

Kuahirishwa kwa mjadala na kutopigiwa kura kwa mswada kuhusu utekelezwaji wa takwa la Katiba ya Kenya kuhusiana na usawa wa kijinsia kunaonyesha jinsi suala la jinsia lilivyo na changamoto nyingi.

Ili kuahirisha mjadala na upigaji kura kuhusiana na mswada huo ambao ulikuwa umewasilishwa na kiongozi wa wengi bungeni katika Bunge la Kenya, Aden Duale, spika wa bunge la kitaifa la Kenya Justin Muturi alikubaliana na maombi ya Bw Duale, kusitisha shughuli hiyo hadi Februari mwaka ujao kwa sababu bunge linakwenda likizo ya Krisimasi.

Ili kupitisha mswaada huo, bunge lilihitaji wabunge 233 wauunge mkono mswaada huo.

Wakati akiliomba bunge kuahirisha mjadala huo, ni wabunge 212 tu waliokuwa bungeni, ikimaanisha bunge lilihitaji wabunge 21 zaidi ili kufanikisha shughuli hiyo.

Itakumbukwa kwamba katika mwaka wa 2012, mahakama ya juu zaidi nchini Kenya iliamua kwamba suala la kanuni ya usawa wa jinsia linafaa kushughulikiwa kwa muda mrefu wala si mara moja.

Wengi wanahofu kuwa hatua ya sasa ya kukosa kupitisha mswaada huu kwa theluthi tatu ya wabunge kunamaanisha kitu kimoja tu— kulingana na katiba ya Kenya, na uamuzi wa mahakama ya juu zaidi wa mwaka wa 2012, uamuzi wa mahakama kuu wa mwaka wa 2015 na 2017, na ushauri wa tume ya jinsia na usawa, itakuwa ni kufuata kifungu cha katiba 261 (6) na (7), ili kulivunjilia mbali Bunge.

Haki miliki ya picha AFP/Getty Images

Hata hivyo, wengine wanadai kuwa hii ilikuwa ni matamanio tu ya waliounda katiba wala si jambo la kushikilia tu kuwa lazima lifanywe.

Mara tu baada ya kutofanikiwa kujadiliwa na kupigiwa kura kwa mswaada huo, baadhi ya wabunge kutoka chama kinachotawala cha Jubilee wanaripotiwa kuandaa mswada mwingine na kumpa spika wa bunge la Kitaifa Justin Mutiri.

Lengo la mswada huo ni kuhakikisha kuwa taasisi zote nchini Kenya hazitalazimika kufuata hitaji hilo la theluthi mbili ya jinsia.

Aidha, kesi nyingine mbili zimewasilishwa kwenye Mahakama ya juu zaidi nchini Kenya baaada ya bunge kukosa kupitisha mswada huo wiki iliyopita.

Ombi la kulivunja Bunge

Kesi hizo zimewasilishwa na mwanaharakati Okiya Omtatah na Nyakina Wycliffe wanaotaka mahakama ya juu zaidi kudurusu uamuzi wake wa mwaka wa 2012 ambao ulikuwa umelipa bunge jukumu kuhakikisha kuwa sheria husika kuhusu jinsia inatungwa.

Katika kesi ya pili ambayo imewasilishwa mblele ya jaji mkuu wa Kenya David Maraga, mahakama imeulizwa kulivunja bunge kwa kukosa kupitisha sheria husika.

Itakumbukwa kuwa jaji John Mativo alikuwa amewapa wabunge wa Kenya siku 60 mwaka uliopita ili kuipitisha sheria hii.

Katika pendekezo hili la hivi karibuni, kipenegele cha katiba 27 (8) inapendekezwa kifanyiwe mabadiliko kwa kuyafuta maneno "two-thirds of the members of elective or (theluthi mbili ya wanachama wa taasisi ambazo wanachama wanachaguliwa" na kubadilisha kwa maneno "40 per centum of the members of" (asilimia 40 ya wanachama).

Nia ni kuhakikisha kuwa viti vitaongezeka kwa mgao wa jinsia kwa 60:40. Msingi wa mswaada huu ambao uliwasilishwa kwa spika wa bunge la kitaifa la Kenya na mbunge maalum David Sangkok ni kuwa sheria iliyopo kwa sasa imeleta matokeo ambayo hayakukusudiwa kwani wanawake ambao wameteuliwa hawaakisi matakwa ya wale waliotarajiwa huku misingi ya uteuzi wao ikitiliwa shaka pia.

Itakumbukwa kuwa uongozi wa bunge la Kenya wenyewe kwa mfano, unawajumuisha wanaume tu — tofauti na ilivyokuwa katika bunge lililopita, ambapo naibu spika wa bunge na naibu kiongozi wa walio wengi walikuwa wanawake.

Kwa sasa, wanawake wabunge nchini Kenya ni asilimia 19% ya wabunge hali ambayo inakwenda kinyume na mahitaji ya kikatiba ya angalau 30%.

Itakumbukwa kuwa mswada sawa na ulioahirishwa wiki jana haukufanikiwa katika bunge lililopita la Kenya baada ya wabunge wa kiume kuungana pamoja na kuhakikisha kuwa mswaada huo haukufanikiwa ingawa wabunge wa kike waliiuunga mkono kwa dhati.

Wakati huo, wabunge wanaume walipanga na kuhakikisha kuwa mswada huo haukupita kwa kutofika bungeni na hivyo kuuangusha mswada huo.

Baadhi ya wabunge wa kiume walidai kuwa mswada huo ulikuwa unakwenda kinyume na demokrasia kwa sababu mswada huo ulikuwa unawapa wanawake viti vya bure na kutoa nafasi kwa wanaosimamia vyama vya kisiasa kuwateua wapenzi wao wa kike.

Mswada wa sasa unatenga viti maalum kwa wanawake ili kuhakikisha kuwa idadi inayoelekezwa kwenye katiba inafikiwa kupitia kwa bunge la kitaifa na bunge la seneti.

Kulingana na mswada huo, mpangilio wake utahakikisha kuwa mahitaji ya katiba yatafikiwa baada ya miaka 20.

Kwa sasa, bunge la kitaifa la Kenya lina wanawake 76 - 23 wakiwa wamechaguliwa na wengine 47 wabunge wa kaunti wa kike na wengine 6 walioteuliwa.

Hii ina maana kuwa bunge la Kenya linahitaji wabunge 41 wa kike ili kufikia 117, ama theluthi moja, ya wabunge 349.

Katika bunge la seneti, kuna wanawake 21 - 3 wakiwa wamechaguliwa na 19 wengine wakiwa wameteuliwa- ikileta idadi ya kuwa na upungufu wa wengine 12.

Hii ina maana kwamba ili kufikia idadi inavyoeleza katiba, bunge la sasa linahitaji kuwateua wanawake wengine 53.

Kwa sababu za kihistoria kwamba wanawake hawakuwa wanachaguliwa kama ilivyofikiriwa, katiba ya Kenya ilitoa maelekezo na kutoa nafasi kwa wanawake 16 katika bunge la seneti na viti 53 katika bunge la kitaifa pamoja na wanawake 47 wanaowakilisha kaunti 47 za Kenya.

Haki miliki ya picha AFP/Getty Images

Sababu hizi za kihistoria zina uchangamano wa aina yake. Hadi sasa, kuna changamoto nyingi za kila aina zinazowatatiza wanawake na kuwafanya wanawake kutoshiriki na kupata nafasi za uongozi wa kisiasa. Ukweli unaobainika ni kuwa changamoto hizi haziwezi kushughulikiwa mara moja.

Katika uchaguzi wa 2013, wanawake wanane waliwania kiti cha Ugavana, na wanawake 19 waliwania kiti cha Useneta.

Wanawake 165 waliwania katika kiti cha ubunge katika viti vipatavyo 290, huku wanawake 155 wakiwania kiti cha mwakilishi wa wanawake katika kaunti.

Sababu za kuwepo na walakini

Kuna sababu kadhaa ambazo zilifanya marekebisho haya ya kikatiba yalikuwa na walakini na huenda yasifaulu hata siku zijazo.

Kwanza, katiba ya Kenya haikuwazia pendekezo la kupanua bunge la Kenya kwa kuongeza idadi ya wabunge ili kufikia hitaji hili la masuala ya kikatiba kuhusu jinsia.

Kinyume na haya, katiba ya Kenya inahitaji hatua za kisheria kuchukuliwa ili kufikia mahitaji haya bunge la kitaifa la Kenya likiwa na wabunge 349 na wabunge wa seneti wakiwa 67.

Katika misingi hii, kubadilisha katiba wakati ambapo kinachohitajika ni sheria ya bunge ni kwenda kinyume ya katiba yenyewe.

Pili, kifungu cha 27(6) cha katiba ya Kenya kinahitaji kuwa mipango yoyote ikiwemo ile ya kisheria na hatua na sera nyingine zenye nia ya kusawazisha hali zichukuliwe na serikali na kushughulikia masuala ya kihistoria ambayo yamekwamiza ufikiaji wa usawa kwa watu na makundi mbali mbali.

Hata hivyo, baadhi ya wanawake, kwa sababu ya sababu fulani, wameweza kuzichukua nafasi zote zilizowahi kutolewa na hali hii kwa niaba ya wale waliotengwa kama ilivyoelezwa na kifungu 27 cha katiba ya Kenya ili kwamba mahitaji ya theluthi mbili ya kijinsia ndiyo ya kipekee yanayohitaji kushughulikiwa.

Hata hivyo, ukiangalia kwingineko, iwapo sheria ya uajiri nchini Kenya ingebadilishwa na kushughulikia hili hitaji la kijinsi la theluthi mbili katika masuala ya uajiri katika sekta ya umma, nchi ya Kenya ingepiga hatua kubwa katika kushughulikia masuala ya kijinsia na wanawake kwa jumla.

Gharama na ubaguzi

Tatu, katika nchi ambayo ina changamoto za madeni na kulipa madeni hayo, inashangaza kuwa serikali inaweza kuoanga kuongeza mzigo zaidi kwa kuunda na kuwapa wanawake 40 hadi 70 zaidi kazi na kuongeza mzigo zaidi kwa serikali na uchumi wa Kenya.

Zaidi, wanawake hawa watakaopata nafasi hizi wanajulikana watakuwa ni wake wa wabunge, wakuu wa vyama, na maafisa wa ngazi za juu serikalini, wapenzi wao, na washirika wa kisiasa na wanaoshirikiana nao.

Nne, marekebisho ya katiba yaliyopendekezwa yalikuwa yanaelezwa kama yenye kuchangia nafasi zaidi kwa akina mama lakini ukweli ni kwamba hii ni mbinu mojawapo ya kuhakikisha kuwa uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta, William Ruto, Raila Odinga , Kalonzo Musyoka na Musalia Mudavadi katika siasa za Kenya unashamiri hata zaidi kwa sababu, baada ya haya yote, na wao watakaoamua ni akina nani wa jinsi ya kike watakaopewa viti hivi maalum.

Haya hayahusiani na kuwatetea wanawake kwa vyovyote.

Mwisho, kipengele cha 201 cha katiba ya Kenya kinahitaji kuwa fedha za umma zitatumiwa kwa uwazi na uwajibikaji. Maafisa wa umma wakiwemo wabunge na wafanyikazi wengine wa serikali wanalipwa kutoka na mfuko au hazina kuu ya serikali.

Hazina hii tayari inatumia zaidi ya asilimia 50 ya mapato ya serikali na kila wakati inapoongezeka kutakuwepo na kupungua kwa fedha kwa matumizi ya maendeleo kwa ajili ya Wakenya wote.

Linalobainika kutokana na vuta nikuvute kuhusiana na swala la jinsia na uwakilishi katika bunge la Kenya ni telezi na litachukua muda mrefu kupatiwa uvumbuzi.

Prof Mogambi, ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi: hmogambi@yahoo.co.uk

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii