Barua ya Albert Einstein kumhusu Mungu yauzwa kwenye mnada, aliamini Mungu yupo?

The God Letter, an autographed letter signed by Albert Einstein Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Barua hiyo imekuwa ikichukuliwa na wengi kama thibitisho la imani yake

Barua iliyoandikwa kwa hati ya mkono na Albert Einstein, ambapo anajadili suala la dini na imani, imeuzwa kwenye mnada kwa bei ya karibu $2.9m (£2.3m).

Bei hiyo imepita makadirio.

Barua hiyo ambayo kwa utani imekuwa ikiitwa "Barua ya Mungu" aliiandika Einstein mwaka 1954 na ilitarajiwa kuuzwa $1.5m (£1.2m) mnadani New York.

Mwanasayansi huyo aliyeshinda tuzo ya Nobel, aliandika barua hiyo ya ukurasa mmoja unusu akiwa na umri wa miaka 74.

Lilikuwa ni kama jibu kwa mwanafalsafa Mjerumani Eric Gutkind kuhusu baadhi ya kazi zake. Gutkind alikuwa pia Myahudi.

Huwa inatazamwa na wengi kama tangazo la msimamo wa Einstein katika mjadala kuhusu sayansi na dini.

"Barua hii yenye uwazi sana, ya kibinafsi iliyoandikwa mwaka mmoja kabla ya kifo cha Einstein inasalia kuwa nyaraka pekee yenye kudhihirisha wazi msimamo wake wa kidini na kifalsafa," taarifa kutoka kwa waendesha mnada wa Christie inasema.

Barua hiyo iliuzwa karibu mara dufu ya bei iliyokadiriwa ambayo ilikuwa kati ya $1m-1.5m.

Katika barua hiyo, aliyoiandika kwa Kijerumani ambayo ilikuwa lugha yake asilia, Einstein amekosoa imani ya sasa kumhusu Mundu.

"Neno la Mungu kwangu tu ni jambo la kuelezea udhaifu wa binadamu na ni matokeo ya udhaifu huu wa binadamu," anaandika.

"Biblia ni mkusanyiko wa hadithi za kale lakini za kuheshimiwa na kutukuzwa, ingawa kwangu zinaonekana zaidi kuwa za kitoto."

Anaendelea: "Hakuna fasiri yoyote, hata iwe ya kina na ya kupambanua zaidi kiasi gani, ambayo kwanu inaweza kubadilisha mtazamo huu wangu."

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Albert Einstein alipigwa picha hii karibu na kipindi ambacho aliandika barua hiyo

Mwanafizikia huyo pia anajadili asili na utambulisho wake, Uyahudi.

Anaandika kwamba dini hiyo "ni kama dini nyingine zore, ni mtazamo mpya wa hadithi za kale".

"Wayahudi, ambao najivunia kuwa mmoja wao, na ambao nimejikita kwenye mtazamo wao wa maisha, bado kwangu hawana kitu chochote tofauti na wengine," ameandika.

"Kwa yale niliyoyaona, si bora kulikobinadamu wengine, ingawa wamelindwa dhidi ya saratani mbaya zaidi kutokana na kukosa mamlaka. Kando na hayo, sioni kitu chochote "kiteule" kuwahusu." (Aliandika hayo miaka michache tu baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia kumalizika, ambapo Wayahudi wengi waliuawa na utawala wa Nazi, na pia taifa la Israel lilikuwa bado halijapata nguvu).

Hii si mara ya kwanza kwa barua ya Enstein kuuzwa mnadani.

Mwaka jana, barua aliyomwandikia mwanafunzi wa kemia kutoka Italia ambaye alizuiwa kukutana naye iliuzwa $6,100.

Iliuzwa pamoja na barua nyingine za Einstein, ikiwemo barua moja ya mwaka 1928 iliyouzwa $103,000. Kwenye barua hiyo alikuwa ameeleza mawazo yake kuhusu awamu ya tatu ya kile ambacho baadaye kiligeuka kuwa nadharia kuhusu uhusiano wa vitu kwenye maumbile, kwa Kiingereza Theory of Relativity.

Haki miliki ya picha Getty Images

Mwaka 2017, barua yake ambapo alikuwa anatoa ushauri kuhusu maisha yenye furaha iliuzwa $1.56m mjini Jerusalem.

Barua hiyo yenye aya moja tu, inasema: "Maisha ya utulivu na ya kunyenyekea yatakuletea furaha zaidi kuliko juhudi za kutafuta ufanisi na misukosuko inayoambatana na harakati na ufanisi huo."

Einstein aliamini kwamba Mungu yupo?

Einstein alikuwa kwenye kundi la watu ambao imani yao huitwa Pantheism kwa Kiingereza.

Ni watu wanaoamini kwamba "Mungu ni kila kitu".

Mara kadha, alionyesha mtazamo huu kwenye mawasiliano yake na Rabbi Herbert S. Goldstein, "Ninaamini katika Mungu wa Spinoza, ambaye anajidhihirisha kupitia upatanifu wa vitu vyote vilivyomo, si katika Mungu anayejishughulisha katika hatima na matendo ya binadamu."

Pantheism kwa njia rahisi zaidi ni imani kwamba kila kitu humwakilisha Mungu. Wenye kufuata imani hii mara nyingi hueleza kwamba Mungu ni vitu vyote vilivyopo, au kwamba mambo na vitu vyote ni Mungu. Kwamba kila ukionacho ni sehemu ya Mungu.

Aina ya Pantheism ya Spinoza aliyoiamini Einstein huamini kwamba kila kitu kinafanana na Mungu. Kwamba Mungu hana ubinafsi na hayajali mambo ya binadamu. Kwa kila kitu kimeundwa na vitu vilevile vya msingi, ambavyo anatoka Mundu. Kwamba Sheria za Fizikia hazina la kuzipinga, na kwamba kila jambo lina matokeo yake. Kila jambo linalotokea au kuwepo lilitokana na hitaji lake kuwepo na lilikuwa nia ya Mungu. Kwamba kwa binadamu, furaha na kuridhika maishani hutokana na kuifahamu dunia na vitu vinavyoizingira badala ya kuomba Mungu aingilie kati.

Benedict de Spinoza alikuwa mwanafalsafa Myahudi aliyezaliwa Uholanzi na wazazi Wayahudi kutoka Ureno Novemba 24, 1632, Amsterdam na akafariki Februari 21, 1677 mjini The Hague, Uholanzi.

Licha ya haya yote Einstein bado alidumisha baadhi ya utamaduni na mila za Wayahudi.

Huwezi kusikiliza tena
Wanawake 100 wa BBC: Mke wa Albert Einstein alikuwa mtu wa aina gani?

Hali kwamba alikuwa Mwanasayansi na kwamba aliongozwa na fikira katika kuufahamu ulimwengu ilimzuia kuwa na imani ambayo inaweza kuwafanya watu waseme alikuwa wa dini fulani.

Alikataa kupewa mazishi ya kitamaduni ya Wayahudi.

Ingawa bado alikuwa anazungumzia kuhusu kuamini kuhusu Mungu, alikuwa si Mungu wa dini za Kiabrahamu (Kikristo, Kiislamu na Kiyahudi ) na pia hakuwa Mungu anayerejelewa na watu walioamini kwamba Mungu yupo.

Alikuwa mara nyingi anajizuia kujiingiza kwenye mjadala kuhusu nani msema kweli, dini au sayansi. Aidha, hakutaka kuamini kutumiwa kwa sayansi kama kielelezo katika kuamua maadili.

Wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, alinukuliwa akisema: "Bado wapo watu, wanaosema Mungu hayupo. Lakini kinachonighadhabisha zaidi ni kwamba huwa wananikuu wanapoeleza msimamo huo wao. Ni waolokole wasioamini Mungu yupo ambao kutowavumilia wengine kwao ni sawa tu na kutowavumilia wengine kwa walokole wafuata dini."

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii