Je ni kweli mswada wa mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa unalenga kuminya upinzani na demokrasia nchini Tanzania?

Rais John Magufuli Haki miliki ya picha IKULU, TANZANIA
Image caption John Magufuli amekuwa akilalamikiwa kuminya demokrasia nchini Tanzania toka lipoingia madarakani miaka mitatu iliyopita.

Viongozi wa vyama vya upinzani na asasi za kiraia nchini Tanzania wameonesha kushtushwa na mswada wa mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa.

Mswada huo, kwa mujibu wa wanaoupinga unalenga kurasmisha kisheria uminywaji wa vyama vya siasa na demokrasia kwa ujumla nchini Tanzania.

Tayari mswada huo umeshawasilishwa bungeni na kusomwa kwa mara ya kwanza mwezi uliopita, lakini je ni mambo gani hasa yanayolalamikiwa kwenye muswada huo?

Kifungu cha 5A kinataka msajili kupewa taarifa kimaandishi na taasisi yeyote ya ndani ama ya nje ya Tanzania itakapotaka kutoa mafunzo ya kiraia ama ya kujenga uwezo kwa chama cha siasa na kutaja wahusika, malengo na nyenzo zitakazotumika katika mafunzo hayo.

Msajili anayo nguvu ya kutoa kibali ama kukataa kufanyika kwa mafunzo hayo na endapo yatafanyika bila kibali taasisi hiyo inaweza kupigwa faini ya mpaka shilingi milioni 30 na watu watakaokutwa na hatia ya kwenda kinyume ni kifungu hicho wanaweza kufungwa kati ya miezi sita mpaka mwaka mmoja gerezani.

Kifungu cha 5B cha muswada kinampa nguvu, msajili wa vyama vya siasa nchini Tanzania kuomba na kupewa taarifa yeyote ile ya chama chochote cha siasa.

Afisaa yeyote wa chama cha siasa ambaye ataenda kinyume na takwa hilo, yaani kutokutoa taarifa husika atakuwa ametenda kosa na akikutwa na hatia atapigwa faini ya kuanzia shilingi milioni moja mpaka kumi au kifungo kisichopungua miezi sita na kisichozidi miezi 12.

Hata baada ya adhabu hiyo, afisaa huyo ama chama hicho bado kitatakiwa kutoa taarifa zilizohitajika na iwapo taarifa itaendelea kumininywa basi chama hicho kinaweza kusimamishwa ama kufutiwa usajili.

Wapinzani Tanzania wanadai iwapo kifungu hicho kitapita, mipango yote ya kimkakati ya vyama vya siasa itakuwa wazi na inaweza kutumiwa na serikali katika kuwaminya.

Hoja yao kuu ni kwamba msajili ni mteule wa rais, ambaye ni mwanachama pia wa chama tawala. Hivyo ofisi ya msajili inaweza kutumika dhidi yao.

Kifungu cha 6 cha muswada kinamlinda msajili na wanyakazi wa ofisi yake dhidi ya kufunguliwa mashtaka: "Shauri lolote halitafunguliwa dhidi ya Msajili, Naibu Msajili, Mkurugenzi ama maafisa wengine chini ya Msajili kwa lolote watakalolifanya ama kutolifanya kwa nia njema chini ya sharia hii," kinasomeka kifungu hicho.

Kifungu cha 11C kinaruhusu eleza vyama vya siasa kuunda ushirikiano wa kufikia malengo ya pamoja ya kisiasa lakini kanuni za kuunda ushirikiano zitatungwa na waziri.

"Waziri (ambaye ni CCM) atatunga Kanuni zitakazoweka masharti na utaratibu wa namna ya kuunda ushirikiano huo. Tukatae!" ameandika Ismail Jussa, kiongozi mwandamizi wa Chama cha Wananchi Cuf kupitia ukurasa wake wa twitter.

Swala lengine lenye kupigiwa kelele ni nguvu ya msajili kufuatilia chaguzi za ndani ya vyama na kufuta usajili wa chama ama mwanachama pale atakapojiridhisha kuwa inafaa.

Huwezi kusikiliza tena
Magufuli: Sijazima demokrasia Tanzania

Kifungu cha 19 A kinasema msajili anaweza kukisimamisha usajili wa chama kwa sababu atakazozitaja na kwa muda atakaouweka mpaka ili chama hicho kiweze kujirekebisha.

Chama ambacho kimesimamishiwa usajili hakitaweza kufanya shughuli zote za kisiasa.

Na iwapo msajili ataona chama hicho hakijajirekebisha anaweza kukifutia usajili.

Kifungu hiki, wapinzani wanadai kinaweza kutumika kuzuia vyama kushiriki uchaguzi kwa jusimamishiwa usajili kabla yay a uchaguzi na kurudishiwa usajili baada ya uchaguzi kupita.

Kifungu 21 E kinampa msajili nguvu ya kumsimamisha mwananchama yeyeyote wa chama chochote cha siasa ambaye atavunja kifungu chochote cha sheria hiyo.

Waziri pia atatunga kanuni za nama gani wanchama wa vyama vya siasa wanaweza kusimamishwa.

Swala la mapato ya vyama vya siasa pia linapendekezwa kufanyiwa mabadiliko kupitia muswada huo na endapo utapitishwa itakuwa ni marufuku kwa vyama vya siasa kupokea fedha kutoka taasisi au mtu yeyote nje ya nchi kama kinavyopendekeza kifungu cha 22.

Kifungu cha 24 kinampa uwezo msajili kuzuia ruzuku ya chama chama kwa muda atakaouweka wazi au usiowekwa wazi akiona matumizi ya fedha hizo yana mashaka.

Pia chama kitakachopata hati chafu ya mkaguzi haitapewa ruzuku kwa miezi 6.

Msajili pia wakati wowote ule anaweza kumtaka Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu (CAG) kufanya ukaguzi maalum pale atakapokuwa na mashaka na matumizi ya rasilimali za chama cha siasa.

Akiongea na mwandishi wa BBC Zuhura Yunus hivi karibuni Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif amesema endapo muswada huo utapita vyama vya upinzani vitakuwa na wakati mgumu kujiendesha.

Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema hatua hiyo ni muendelezo wa kile alichokiita ni hatua ya nne ya udikteta ambayo ni kudhibiti vyama vya siasa.

Hata hivyo msajili wa vyama vya siasa Jaji Francis Mutungi amesema muswada huo hauna nia yoyote ovu dhidi ya vyama vya siasa na amewataka wadau wote wenye maoni ya kuboresha wayawasilishe kwenye warsha itakayofanyika Zanibar Zanzibar Desemba 21-22.

"Kama kweli wana hoja za msingi basi wataziwasiisha kwenye warsha ya mashauriano itakayofanyika Zanzibar...lakini hakuna nia yoyote inayokusudiwa kutekelezwa kupitia muswada huu," jaji Mutungi ameliambia gazeti la Kingereza la The Citizen.

Mada zinazohusiana