Moody Awori: Uhuru Kenyatta ajitetea kumteua makamu wa rais wa zamani mwenye miaka 91 'bodi ya vijana', asema vijana hawaaminiki

Rais Kenyatta August 11, 2017 Haki miliki ya picha AFP/Getty Images

Je, vijana wanaweza kuaminiwa kusimamia mali ya umma? Ndio mjadala ambao umekuwa ukipamba moto mtandaoni Kenya baada ya Rais Uhuru Kenyatta kumteua mwanasiasa wa miaka 91.

Bw Moody Awori ambaye ni makamu wa rais wa zamani aliteuliwa kuhudumu katika Bodi ya Mfuko wa Michezo, Sanaa na Ustawi wa Jamii.

Wakenya wamekuwa wakilalamika mtandaoni kwamba wadhifa huo ulifaa kukabidhiwa kijana, kwa sababu bodi hiyo inahusu masuala ya michezo na sanaa ambayo wadau wakuu ni vijana.

Awori aliteuliwa kwenye wadhifa huo kupitia ilani ya gazeti rasmi la serikali Novemba 28 ambayo ilichapishwa na Waziri wa Fedha Henry Rotich.

Miongoni mwa wanachama wengine wa bodi hiyo ni makatibu watano wa wizara wanaosimamia idara za Elimu, Sanaa, Afya, Hazina Kuu na Michezo.

Akizungumza katika uwanja wa kimataifa wa michezo wa Kasarani alipoongoza sherehe ya kufuzu kwa vijana 10,000 chini ya mpango wa mafunzo ya biashara na ufundi wa 2jiajiri unaodhaminiwa na benki ya Kenya Commercial Bank (KCB), Rais Kenyatta alionekana kudokeza kwamba hana imani na vijana katika masuala ya kifedha.

Huwezi kusikiliza tena
Je, ni kweli kuwa vijana Kenya wanabagua kazi?

"Jiwekeni kwenye nafasi yangu, ukiona vile watu wanaiba pesa. Na hizi ni pesa tuliidhinisha majuzi, kwa sababu tunataka kuona jinsi tunaweza kutumia pesa hizi kutusaidia katika miradi yetu ya michezo, sanaa, afya...na hii ni miradi itakayowafaidi nyingi (vijana)," alisema.

"Halafu tuseme tupatie kijana, mimi afadhali nikae na huyo mzee bwana achunge hizo pesa zitumike vile inatakikana. Eee bwana...au mnasemaje jamani? Si pesa ni zenu za afya, utamaduni, sanaa."

"Sasa mnataka twende na tumena vile watu wakipatiwa kazi kama hiyo vile wanaenda kufanya fanya. Si afadhali tupatie huyo mzee achunge ndio ziwarudie? Aaa, watu waniwache bwana mimi sitaki mambo mengi."

Wekenya wana maoni mbalimbali, wakisimulia kwamba Bw Moody alikuwa tayari amekomaa kiumri walipozaliwa.

Huyu anasema alikuwa amekaribia sana kupata kazi, kisha Rais akatoa tamko lake.

Wengine, nao wanamkumbusha Rais kuhusu sera yake ya vijana.

Moody Awori ni nani?

Haki miliki ya picha AFP/Getty Images
Image caption Bw Moody Awori akihutubu Havana, Cuba mwaka 2006

Bw Moody Awori alizaliwa 5 Desemba, 1927 na alihudumu kama makamu wa rais wa tano wa kenya kati ya Septemba 2003 na Januari 2009.

Hufahamika kwa utani kama Uncle Moody (Mjomba Moody).

Ameandika kitabu kwa jia Riding on a Tiger kuhusu maisha yake katika siasa.

Aliingia bungeni mara ya kwanza mwaka 1984 akiwakilisha eneo bunge la Funyula, magharibi mwa Kenya na akahudumu kama waziri msaidizi katika wizara kadha chini ya Rais Daniel arap Moi.

Aliteuliwa makamu wa rais na Rais Mwai Kibaki baada ya kifo cha Michael Kijana Wamalwa.

Alipoondolewa kwenye wadhifa huo Januari 2009, Bw Kibaki alimteua Bw Kalonzo Musyoka kuwa makamu mpya wa rais.

Huwezi kusikiliza tena
Wanasiasa Kenya wanawajali vijana?

Alipokuwa makamu wa rais alikuwa pia waziri wa mambo ya ndani ambapo anakumbukwa zaidi kwa kutekeleza mageuzi katika idara ya magereza.

Aliteuliwa na Rais Kenyatta mkesha wa siku yake ya kuzaliwa kuwa mwanachama wa Bodi ya Mfuko wa Michezo, Sanaa na Ustawi wa Jamii.

Miongoni mwa watu mashuhuri Afrika Mashariki, Bw Moody kwa umri anakaribiana sana na rais mstaafu wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi wa Tanzania (93), Rais Mstaafu wa Kenya Daniel arap Moi (94).

Anawazidi umri mke wa mwanzilishi wa taifa la Tanzania Maria Nyerer (87), rais mstaafu wa Kenya Mwai Kibaki (87), na mke wa mwanzilishi wa taifa la Kenya Mama Ngina Kenyatta (85).

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii