Uchaguzi DRC 2018: Kwa nini huenda Rais Joseph Kabila akawania urais tena 2023, EU yamuongezea vikwazo Emmanuel Ramazani Shadary

Bw Kabila Kinshasa 9 Desemba, 2018 Haki miliki ya picha AFP/Getty Images
Image caption Bw Kabila anasema bado safari ni ndefu

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila amesema ataendelea kushiriki katika siasa nchini humo hata baada ya kuondoka madarakani baada ya uchaguzi utakaofanyika wiki mbili zijazo.

Aidha, hajafutilia mbali uwezekano wake wa kuwania tena urais uchaguzi mkuu mwingine utakapoandaliwa mwaka 2023.

Hayo yanajiri huku Umoja wa Ulaya ukitangaza kwamba umeongeza muda wa kutekelezwa kwa vikwazo dhidi ya watu 14 mashuhuri nchini DR Congo hadi Desemba mwaka ujao.

Miongoni mwa wanaoathiriwa na vikwazo hivyo ni mgombea wa muungano wa Bw Kabila, Emmanuel Ramazani Shadary.

Watu hao walikuwa wamewekewa vikwazo vya kuzuiliwa kwa mali yao na pia kupigwa marufuku ya kutoingia Umoja wa Ulaya kutokana na juhudi za kuhujumu machakato wa uchaguzi nchini DRC na ukiukaji wa haki za kibinadamu.

Bw Kabila alitarajiwa kuondoka madarakani miaka miwili iliyopita baada ya kuongoza kwa mihula miwili kwa mujibu wa katiba.

Hata hivyo, uchaguzi mkuu nchini humo uliahirishwa mara kadha, serikali ikisema maandalizi yake hayakuwa yamekamilika vyema.

Upinzani ulitazama hilo kama njama ya Bw Kabila kutaka kuendelea kuongoza.

Mwezi Agosti, Bw Kabila alimtangaza mshirika wake wa karibu Emmanuel Ramazani Shadary ambaye ni waziri wa zamani wa mambo ya ndani kuwa mgombea wa muungano wa kisiasa unaotawala kwa sasa.

Bw Shadary amewekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya kutokana na tuhuma za ukiukaji wa haki za kibinadamu.

Katibu wa chama cha upinzani cha Movement for the Liberation of Congo (MLC), Eve Bazaiba, ameambia BBC kwamba Bw Shadary atadhibitiwa na Bw Kabila na kwamba kimsingi itakuwa ndiye anayeongoza nchi.

"Anataka tu kusalia madarakani. Hata kama alimchangua Shadary, Shadary ni mtu tu wa kuonekana, ndiye atakayemuongoza Shadary kwa kila jambo. Kiuhalisia, atakuwa bado ndiye rais."

Bi Bazaida amesema serikali imekuwa ikiwazuia wanasiasa wa chama cha MLC kufanya kampeni.

Haki miliki ya picha PPRD

Kwa muda mrefu, ilikuwa bado haijabainika iwapo Rais Kabila, angewania tena hadi alipoamua kumtangaza Shadary kuwa mgombea wa muungano wake wa kisiasa.

Kwenye mahojiano na shirika la habari la Reuters, Rais Kabila amesema: "Mbona tusisubiri hadi mwaka 2023 … ndipo tuwe na uwazi kuhusu mambo haya," alisema.

"Maishani sawa na ilivyo katika siasa, hauwezi kufutilia mbali jambo kabisa."

Kumekuwa na wasiwasi kutoka kwa upinzani na jamii ya kimataifa kuhusu iwapo uchaguzi wa DRC utakuwa huru na wa haki.

Lakini Bw Kabila amesema wasiwasi huo haufai kuwepo.

Haki miliki ya picha FABRICE COFFRINI
Image caption Martin Fayulu awali alitangazwa kuwa mgombea wa muungano wa upinzani

"Tunakusudia kadiri ya uwezo wetu kuhakikisha uchaguzi huu hauna kasoro hata moja. Waangalizi wanaofikiria kwamba uchaguzi huu hautakuwa huru na wa haki, bado sijawaona wakija hapa na kusema ni kitu gani tumekikosa."

Kabila aliingia madarakani akiwa na miaka 29 baada ya babake Laurent Desire Kabila kuuawa na mlinzi wake mwaka 2001.

Aliahidi kurejesha amani na kuangamiza ufisadi na amekuwa akitaja hayo kama baadhi ya mafanikio ya utawala wake.

DRC ilikuwa imekabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 1998 na mwaka 2003 ambapo takriban watu 5 milioni walifariki kutokana na vita, njaa na maradhi.

"Tuna majuto yoyote? La hasha, hata kidogo. Tumepata mafanikio mengi. Jambo kuu zaidi ni kwamba tuliweza…kuliunganisha tena taifa na kulirejesha kwenye mkondo ufaao."

Kabila amesema anataka kusalia katika siasa ili kulinda mafanikio hayo na kuongeza kwamba wanaotaka kutoa uamuzi kuhusu mafanikio yake wanaweza kusubiri hadi amalize kazi yake.

"Bado kuna safari ndefu sana mbele yetu na kuna sura nyingi sana ambazo zitaandikwa kabla tuanze kuandika vitabu vya historia."

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Felix Tshisekedi ameungana na Vital Kamerhe ambaye ni mgombea mwenza wake

Katiba nchini DRC inamzuia mtu aliyeongoza kwa mihula miwili mfululizo kuwania tena urais, lakini haijazuia mtu kama huyo kuwania tena baada ya kiongozi mwingine kuingia madarakani.

Baadhi wanasema huenda kikawa kisa kama cha rais wa Urusi Vladimir Putin ambaye baada ya kuongoza kama rais kati ya 2000 na 2008, alikuwa waziri mkuu kati ya 2008 na 2012 kabla ya kurejea tena kama rais wa nchi hiyo. Alibadilishana na mwandani wake Dmitry Medvedev ambaye kwa sasa ndiye waziri mkuu.

Mwanamuziki atekwa

Mwanamuziki wa rap ambaye amekuwa mkosoaji mkuu wa Rais Joseph Kabila mashariki mwa DRC alitekwa usiku wa kuamkia Jumapili, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.

Akim Bufole Corneille, 26, alitwaliwa na watu wasiojulikana alipokuwa akiondoka kwenye tamasha moja mjini Bukavu katika jimbo la Kivu Kusini, AFP wamemnukuu babake Amuli Bufole akisema.

"Kabla yake kutwaliwa, aliandika ujumbe mfupi kwa haraka kutufahamisha kwamba alikuwa hatarini," alisema Bw Bufole.

Alitekwa si mbali sana na nyumbani kwao, na babake anasema walipofika walipata tu kiatu chake kimoja na kipochi chake.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii