Rais Museveni amteua Luteni kanali Edith Nakalema kuongoza kitengo kipya cha kupambana na ufisadi Uganda

Museveni Haki miliki ya picha Getty Images

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amezindua kitengo kipya cha kupambana na rushwa na Ufisadi nchini Uganda na hasa katika idara zote za Serikali kuchunguza tatizo la rushwa.

Rais Museveni ameeleza kuwa jukumu la kupambana na rushwa liko kwa wananchi, ambao amewataka kuwasiliana na kitengo hicho kipya kitakachohudumu moja kwa moja chini ya ofisi yake.

Kiongozi huyo yupo katika shinikizo kuonyesha uwajibikaji wa serikali yake, wakati anakabiliwa na changamoto na upinzani kutoka kwa wanasiasa wanaowavutia wapiga kura vijana - kama mwanamuziki na mbunge Bobi Wine.

Aliyekuwa msaidizi wake wa kibinafsi, Luteni kanali Edith Nakalema, ndiye aliyechaguliwa kukiongoza kitengo hicho kipya.

Kitahudumu moja kwa moja chini ya ikulu nchini - ishara ya namna majukumu ya serikali yanavyoendelea kudhibitiwa chini ya urais Uganda.

Na vita hivi dhidi ya rushwa vipo karibu kwa rais Museveni.

Katika pengine kutaka kudhihirisha anachokimaanisha kwa kuidhinisha hatua hii, katika kashfa ya rushwa inayozungumwa kwa sasa nchini dhidi ya waziri wa mambo ya nje Sam Kutesa, Museveni ameeleza kwamba kiongozi huyo anachunguzwa kwa tuhuma za kula rushwa ya thamani ya dola nusu milioni kutoka kwa mfanya biashara mmoja wa Hong Kong.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Museveni anakabiliwa na changamoto na upinzani kutoka kwa wanasiasa wanaowavutia wapiga kura vijana

Kesi hii ni muhimu kwasababu Kutesa ni kiongozi mwenye ushawishi mkubwa nchini.

Rais Museveni anasema waziri Kutesa hana budi kueleze namna alivyozitumia fedha hizo.

Mahakama moja ya Marekani ilimpata na hatia Patrick Ho kwa kumhonga Kutesa ili anufaike na fursa za kibiashara.

Kutesa kwa upande wake amekiri kwamba fedha alizopewa ni kwa minajili ya kufadhili taasisi anayoianzisha ya msaada.

Waziri huyo aliwahi pia kuhudumu kama rais wa baraza kuu la Umoja wa mataifa kuanzia Septemba 2014.

Je utaratibu ni upi wa mpango huu mpya dhidi ya rushwa?

Rais Museveni amekiri kuendelea kukithiri kwa ubadhirifu wa fedha za umma katika serikali, rushwa au ufisadi kuwa ni mambo ambayo ni tatizo kubwa sana.

Kadhalika ameshutumu mtindo wa watu kuwaajiri wengine kazi kwa misingi ya kikabila na kujuana.

Na ndio sababu kuidhinisha kitengo hicho maalum cha kupambana na rushwa kitakachoongozwa na Luteni Kanali Edith Nakalema.

'Nimemuweka askari wangu mwanamke hapa Luteni Kanali Nakalema, njoo hapa wakuone. Lakini tafadhali kuwa makini sana, Usilete watu wafisadi katika ofisi hiyo.

Usilete wala rushwa, jihadhari nao', amesema rais Museveni.

Sheria kadhaa na taasisi zimeidhinishwa kwa miaka mingi Uganda ikiwemo ya ukaguzi wa serikali kuchunguza na kuwaadhibu wanaofuja mali za umma.

Haki miliki ya picha Kazuhiro Nogi/AFP/Getty Images
Image caption Mahakama moja ya Marekani ilimpata na hatia mfanyabiashara wa Hong Kong kwa kumhonga Waziri wa mambo ya nje Uganda Sam Kutesa (Pichani)

Je kitengo hiki kina tofuati gani na taasisi zilizopo tayari?

Mwandishi wa BBC mjini Kampala, Omar Mutasa anasema, hilo ndio suali ambalo wengi watajiuliza nchini.

Rais Museveni ametaja baadhi ya mashirika amabayo yapo mengi tu nchini, yanayopambana na rushwa likiwemo hasaa la ukaguzi wa mali ya umma IGG.

Swali sasa ni kwamba tofuati iko wapi? wakati bado tena kumeundwa kitengo kingine ambacho na kwa kauli ya rais Museveni, kitategemea ushirikiano mkubwa kutoka kwa umma katika vita hivyo dhidi ya ufisadi nchini.

Rais Museveni ameeleza matumaini na imani kubwa na kitengo hicho kipya na kushinikiza raia kujitokeza na kuwaripoti maafisa wowote wala rushwa.

Amewashutumu makatibu wa kudumu katika wizara tofauti serikalini, maafisa wakuu wasimamizi katika wilaya, wakuu wa tarafa kuwa ndio watuhumiwa wakubwa wa rushwa nchini.

Uganda imeorodheshwa katika nafasi ya 151 kati ya mataifa 180 yaliochunguzwa kwa rushwa katika ripoti ya Februari mwaka huu ya shirika la Transparency International.

Ni ya tatu iliyokithiri ufisadi Afrika mashariki baada ya Sudan kusini na Somalia.

Huenda sasa hatua hii ya Museveni ni katika kujaribu kuziba mapengo ambayo wakosoaji wanayataja kama ishara ya tatizo kubwa katika vita dhidi ya rushwa Uganda.

Shirika hilo la TI linaeleza katika ripoti yake hiyo kwamba pasi kushughulikiwa, huenda nchi hiyo isipige hatua.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii