'Kama si mama mkwe wangu ningelifariki nje ya benki hiyo nikijifungua'

Khazanchi Nath with his mother
Image caption Khazanchi Nath alizaliwa miaka miwili iliyopita wakati mama yake Sarvesha Devi alikuwa kwenye foleni ya kuchukua pesa

Taarifa ya kuzaliwa kwa mtoto Khazanchi Nath wakati mama yake akiwa kwenye foleni ya kuchukua pesa benki ziligonga vichwa vya habari.

Khazanchi ambaye sasa ana miaka miwili amejipata kati kati ya malumbano inayohusisha familia yake na kijiji alikozaliwa mama yake kutokana na umaarufu wake

Mwandishi wa BBC Geeta Pandey alitembelea kijiji cha Kanpur kaskazini mwa India kuangazia maisha ya mtoto huyo.

Khazanchi, inamaanisha "tunu", alizaliwa katika jimbo la Uttar Pradesh Disemba 2 mwaka 2016, chini ya mwezi mmoja baada ya serikali ya India kupiga marufuku ghafla noti za rupee 1,000 na 500 rupee

Uamuzi huo wa waziri mkuu Narendra Modi, ulisababisha uhaba mkubwa wa pesa.

Kwa wiki kadhaa mamilioni ya watu nchini India walionekana wakipanga foleni nje ya mabeki kupata sarafu mpya.

Mwanamke mja mzito aliyefahamika kama Sarvesha Devi, aliyekuwa ametembea kutoka kijiji cha Sardar Pur hadi benki iliyopo mji wa Jhinjhak akiwa ameandamana na mama mkwe wake alipatwa na uchungu wa kuzaa akiwa kwenye foleni ya kubadilisha pesa nje ya benki.

Image caption Kuzaliwa kwa Khazanchi kuliangaziwa sana katika habari kote duniani

Kisa hicho kiligonga vichwa vya habari na kutokea wakati huo mtoto Khazanchi alipata umaarufu mkubwa kiasi cha picha yake kuchapishwa katika mabango ya kampeini ya uchaguzi wa jimbo hilo dhidi ya chama tawala cha BJP.

Akisimulia BBC kisa hicho wakati huu Sarvesha Devi alisema, '' Kama si mama mkwe wangu ningelifariki nje ya benki hiyo nikijifungua''.

Baada ya mtoto huyo kuzaliwa, serikali ilimlipa Sarvesha fidia ya rupee 200,000 sawa na dola 2,395.

Miaka miwili baada ya kulipwa fedha hizo maisha yake yamebadilika.

Alipoulizwa juu ya uhusiano wake na mama mkwe wake Sarvesha alisema uhusiano wao umekuwa mbaya kiasi cha yeye kutaka kujitoa uhai wake na wa mwanawe Khazanchi.

Sarvesha anadai kuwa mama mkwe wake amegeuka kuwa katili na kwamba amekuwa akimpiga akitaka sehemu ya fedha alizopewa.

Image caption Khazanchi anaishi na mama yake na ndugu zake wanne

Ni nini kilisababisha mvutano huo?

Kumekuwa na na hali ya kulaumiana kutoka pandezote mbili na imekuwa vigumu kujua nani kati yao anasema ukweli.

Sarvesha Devi anasema kuwa alitumia sehemu ya pesa hizo kumpeleka hospitali mwanawe mkubwa na kulipa deni lililoachwa na marehemu mume wake.

Anasema mume wake aliyefariki kutokana na maradhi ya kifua kikuu miezi minne kabla ya Khazachi kuzaliwa.

Pesa zilizosalia aliweka benki kama akiba.

Hata hivyo mama mkwe wake amekuwa akidai kupewa nusu ya pesa zote alizolipwa na serikali kama fidia.

Image caption Baada ya Khazanchi kuzliwa , Sarvesha Devi (kulia) alisema kama si mama mkwe wake angelikuwa amekufa

Anasema alipokataa , "familia ya mume wake ilimpiga na kumfukuza". Ni hapo ndipo aliamua kuondoka.

Mama huyo wa watoto watano mwenye umri wa miaka 37 aliielezea BBC kuwa yeye ni mlemavu na mjane.

"Mimi ni mlemavu na mume wangu amefariki, sina mtu wa kunisaidia kuwalea watoto wangu kwa hiyo ni jukumu langu kuwaandalia maisha yao ya baadaye".

Uhusiano wake na wakwe zake ulizorota zaidi alipoamua kuhama. Malkhan Nath, kaka yake mkubwa anasema kumekuwa na shinikizo kutoka jamii ya kuwataka wamrudisha nyumbani kwa wakwe zake.

"Tumekuwa tukimshauri arudi kwa familia yake lakini amekataa, anasema kuwa wanampiga na kumtelekeza. Hatujui la kufanya. Huyu ni dada yangu: nawezaje kumfukuza nyumbani kwao?"

Mzozo huo wa kifamilia sasa umewasilishwa mbele ya baraza la wazee wa jamii ya Baigas, ambayo Malkhan Nath anaiita "mahakama kuu".

Baraza hilo linajumuisha wazee mashuhuri wa jamii ya Baigas ambao wamepewa jukumu la kutatua mzozo unaohusu masuala ya jamii hiyo.

Uamuzi wao sio wa kisheria, lakini unachukuliwa kwa uzito mkubwa kwasababu yeyote anayekiuka uamuzi wao hutengwa na jamii nzima hadi pale atakapo lipa faini.

Image caption Malkhan Nath anasema jamii ilikuwa inamshinikiza kurudisha dada yake nyumbanni kwa wakwe zake

Malkhan Nath anasema mwaka jana alilazimika kufika mbele ya baraza hilo la wazee "koti" mara tatu, na wakati mmoja alitozwa faini ya rupee 650 kwa sababu dada yake amekaidi uamuzi wa kufika mbele ya baraza hilo akiandamana na mwanawe Khazanchi.

Mapema mwezi huu siku moja kabla ya siku ya kuzaliwa ya mtoto,mama yake anasema kulikuwa na tishio la kumteka nyara.

"Nilikuwa nimeketi nje saa za jioni wakati huo mtoto alikuwa amelala. Mara kukatokea gari mbili za watu waliyotaka kumchukua mtoto kwa lazima kuenda kusherehekea siku yake ya kuzaliwa ya mmoja wa wanasiasa siku iliyofuata. Nilipokataa ombi lao walimchukua kwa lazima na kuenda naye kwa gari lao. Walikuwa na njama ya kumteka mwangau," alisisitiza.

Japo mwanasiasa aliyetumia picha ya mtoto huyo katika mabango yake ya kampeini ya uchaguzi wa majimbo mwaka jana, ameendelea kudumisha uhusiano na mtoto huyo Khazanchi.

Wanahabari wa jimbo hilo wameripoti kuwa mwanasiasa huyo alikuwa na mpango wa kumzawadia nyumba mbili katika miji ya Sardar Pur na Anantpur Dhaukal endapo angelishinda uchaguzi huo.

Image caption Uhusiano wa Sashi Devi na mkaza mwanawe uligeuka na kuwa mbaya sana mwaka uliyopita

BBC ilipomtembelea Sashi Devi kupata kauli yake kuhusu matukio yaliyosababisha mkaza mwanawe kurudi kwao alisema kuwa akimlisha na kuwavisha Sarvesha Devi na watoto watano tangu mwanawe alipokuwa mgonjwa hadi alipofariki.

Alipoulizwa kwa nini alitelekeza na kumpiga Sarvesha Devi alisema. "Nina wakaza wanangu zaidi ya wanne na wajukuu 16. Kwanini ni mpige yeye peke yake?" aliuliza.

Mama huyo pia alielelezea jinsi jinsi mkaza mwanawe alivyompiga na kumtukana: "Nimeenda mara mbili kijiji kwao kumuomba arudi nyumbani na watoto. Kila nikienda wanamficha Khazanchi, na wanawake katika kijiji hicho wananitukana."

Sashi Devi pia amepuuzilia mbali madai kwamba yeye au mtu yeyote wa familia yake huenda akamdhuru Sarvesha Devi au Khazanchi. "Tunawezaje kumuua binti yetu na mjukuu wetu?"

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii