Mwanaume wa miaka 40 adaiwa kumbaka binti wa miaka mitatu India

A protest in India against child sex abuse Haki miliki ya picha AFP

Binti wa miaka mitatu yupo mahututi hospitalini nchini India baada ya kubakwa Jumapili Desemba 17.

Mtuhumiwa, mwenye umri wa miaka 40 ni mlinzi katika jengo ambalo mtoto huyo anaishi, na tayari ameshakamatwa.

Polisi walimkuta mtoto huyo akiwa amepoteza fahamu na kumkimbiza hospitali ambapo anafanyiwa upasuaji.

Tukio hilo limetokea jana ikiwa ni siku ya kumbukumbu ya miaka 6 tangu kubakwa kwa mwanafunzi na genge la wahuni katika basi jijini Delhi.

Kamishina wa masuala ya wanawake huko Delhi Swati Maliwal amesema tukio hilo limeangusha kumbukumbu ya mwathirika wa ubakaji katika basi ambapo tukio hilo lilipelekea kuibuka kwa maandamano makubwa nchi nzima na kuongeza makali katika sheria ya ubakaji.

Bado hakuna taarifa sahihi juu ya hali ya mtoto huyo au hata taarifa kuwa atapona au la, jambo ambalo vyombu vya habari vya ndani vinataja kuwa ni unyama.

Wakazi wa eneo hilo walimtafuta mtuhuhumiwa na kumvamia baada ya tukio hilo kuwekwa wazi, gazeti la The Times of India limeripoti. Pia limemnukuu polisi mmoja aikisema kuwa mtuhumiwa alitibiwa majeraha kabla ya kuwekwa chini ya ulinzi.

Wazazi wa mtoto huyo, ambao ni wafanyakazi walikuwa mbali wakati tukio hilo likitokea. Inasemekana kuwa mtuhumiwa alimlaghai mtoto huyo kwa pipi na kumchukua kutoka nje ya nyumba alipokuwa.

Polisi wamefungua kesi ya ubakaji chini ya sheria ya ulinzi wa watoto na unyanyasaji wa kingono, ambayo inaweza pelekea hukumu ya kifo kwa mtuhumiwa.

Tukio hilo ambalo limeibua hasira mpya huko India, linatokea baada ya mfululizo wa matukio makubwa yanayohusisha watoto mwaka huu.

Mwezi April tukio la kinyama la kubakwa kwa mtoto wa miaka 8 na genge la wahuni liligonga vichwa vya habari. Mwezi Juni mamia ya watu waliingia mtaani katika mji mkuu wa Madhya Pradesh baada ya kubakwa kwa mtoto wa miaka saba.

Mapema mwezi huu wanamke mmoja kaskazini mwa India alichomwa moto na wanaume wawili ambao inasemekana walimbaka. Mwanamke huyo alikuwa njiani kufungua kesi ya malalamiko polisi mkasa huo ulipomkuta.

Inaripotiwa kuwa awali polisi waliwahi kataa kumpa ushirikiano.


Viwango vya ubakaji India

  • Mtoto wa umri wa chini ya miaka 16 anabakwa kila baada ya dakika 115, mtoto wa chini ya miaka 10 ni kila baada ya saa 13.
  • Idadi ya kesi za watoto kubakwa imeongezeka kutoka 8,541 in 2012 mpaka 19,765 kwa mwaka 2016
  • Zaidi ya watoto 10,000 walibakwa mwaka 2015
  • Wanawake milioni 240 wanaoishi India waliolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18
  • Asilimia 53.22 ya watoto walioshiriki katika tafiti za serikali waliripoti kunyanyaswa ki ngono.
  • Asilimia 50 ya watuhumiwa wanao wabaka au kuwanyanyasa kingono watoto ni watu wanao aminiwa na familia au walio kabidhiwa kuwahudumia.

Chanzo: Serikali ya India, Unicef