BASATA: Diamond Platnumz na Rayvanny wafungiwa kufanya maonyesho Tanzania na nje ya nchi, amemfuata Paul Pogba?

Diamond Haki miliki ya picha AFP/Getty

Diamond Platnumz na Rayvanny wamefungiwa kufanya onyesho lolote ndani na nje ya Tanzania na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

Baraza hilo limesema marufuku hiyo ya muda usiojulikana inaanza kutekelezwa leo.

Wasanii hao wawili walikuwa awali wametakiwa kuuondoa wimbo wao kwa jina 'Mwanza' kutoka kwenye mitandao ya kijamii, lakini wimbo huo umeendelea kuwepo kwenye YouTube.

Aidha, wameendelea kuucheza kwenye matamasha.

"Baraza limefikia maamuzi ya kuwafungia rasmi kutokana na wasanii hawa kuendelea kuonyesha dharau na utovu wa nidhamu kwa mamlaka zinazosimamia masuala ya sanaa nchini na uvunjifu wa maadili uliokithiri unaofanywa na waandaaji wa Tamasha la Wasafi 2018, chini ya uongozi wake Diamond Platnumz," taarifa ya Basata ambayo imetiwa saini na Onesmo Kayanda kwa niaba ya Katibu Mtendaji inasema.

"Pamoja na maelezo hayo, Baraza linatoa taarifa kuwa kibali cha Tamasha la Wasafi 2018 kimesitishwa kutokana na ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu katika uendeshaji wa tamasha hilo hapa nchini."

Basata walitangaza kuufungia wimbo wa Mwanza mnamo 12 Novemba kwa kile walichosema ni "kwa kubeba maudhui machafu."

"Lebo ya Wasafi, wasanii wake sambamba na vyombo vya habari vinapewa onyo na tahadhari kuendelea kutumia wimbo huu kwa namna yoyote ile," baraza hilo lilisema.

Baraza hilo lilisema wimbo huo una "ukiukwaji mkubwa wa maadili ya Kitanzania" na kwamba umetumia "maneno yanayohamasisha ngono.

Baraza hilo wakati huo liliwaonya wasanii waliohusika, Rayvanny na Diamond, pamoja na uongozi wa Wasafi Limited kufuata sheria na "kutoutumia wimbo huo na nyimbo nyingine zilizofungiwa kwa namna yoyote ile."

Baraza hilo liliwataka "kuuondoa wimbo huo mara moja kwenye mitandao ya kijamii kabla ya kufika saa kumi kamili" siku hiyo.

Taarifa hiyo ilitiwa saini na Katibu Mtendaji wa Basata Godfrey Mngereza.

Diamond amemfuata Pogba?

Baada ya meneja wa Manchester United Jose Mourinho kufutwa kazi mapema leo, kiungo wa kati wa Ufaransa Paula Pogba alipakia picha mtandaoni, akiwa ametoa jicho na tabasamu, na kwenye maelezo 'Caption This', kwa maana ya weka maelezo kwenye picha.

Diamond, taarifa zake kufungiwa zikisambaa, amepakia picha mbili kwenye Instagram akionekana kucheka na kufurahia sana akiwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ambapo kwenye kitambulisha mada amemwita 'Kipenzi CHetu'.

Aliandika maelezo 'Please Caption this....... mie naanza na hizi mbili...1. "Basi mie na @rayvanny Tukatumbukia Pale Stejini" "Eti @_esmaplatnumz anamwita TARZAN kwasababu ya Vitopu vyake"😂 Earlier Today with our #FormerPresident #Daddy #KipenziChetu #BongoflevaGodFather Hon: @jakayakikwete."

Haki miliki ya picha INSTAGRAM

Faini ya Tshs 3m

Siku moja baadaye, Basata walitoa taarifa na kueleza kuwa kikao cha Basata na wawakilishi wa Wasafi Limited ambacho kiliwashirikisha pia maafisa wa mamlaka ya Mawasiliano ya Tanzania (TCRA) na Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kutoka kwenye Kitengo cha Matukio na Uhalifu wa Kimitandao, kiliandaliwa kuujadili wimbo huo.

Haki miliki ya picha InSTAGRAM

Basata walitoa maagizo zaidi ya kutolewa kwa wimbo huo kwenye YouTube na mitandao mingine haraka iwezekanavyo.

Diamond, Rayvanny na Wasafi Limited walitakiwa kila mmoja kulipa faini ya shilingi milioni tatu za Tanzania kabla ya siku 14 kupita.

"Kutokutekeleza ama kukaidi maagizo hayo kwa wakati uliopangwa kutapelekea Barazakuchukua hatua kali zaidi kwa wasanii hao na uongozi wao ikiwa ni pamoja na kuwafungia kabisa kujishughulisha na shughuli za sanaa nchini."

Haki miliki ya picha TWITTER
Image caption Pogba alipakia ujumbe huu Twitter kisha akaufuta muda mfupi baadaye

Matamasha tele Kenya na Tanzania

Diamond Platnumz na kikosi chake cha Wasafi wameandaa matamasha chungu nzima msimu huu wa Krismasi, ambapo walitarajiwa kuandaa tamasha mjini Embu katika eneo la Mlima Kenya nchini Kenya tarehe 24 Desemba

Jumapili alikuwa anatokea kutumbuiza tena Mwanza nchini Tanzania, siku chache baada ya kuwa Sumbawanga.

Mkesha wa Mwaka Mpya amepangiwa kuwa bustani ya Uhuru, Nairobi.

Diamond Platnumz alipozuiwa uwanja wa ndege Dar

Julai mwaka huu, mwanamuziki huyo alizuiwa kwa muda uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam kutokana na kutokuwa na kibali kutoka kwa Basata.

Basata walijitetea kwa kuandika: "Utaratibu wa msanii kuwa na kibali anapoenda nje, yaani kutambua wapi anaelekea kikazi si mpya.Upo ktk kanuni toka awali. Lengo ni kumhakikisha ulinzi wa haki na usalama wake pale kutakapotokea suala lisilo rafiki. Pia,kumuaga kwa kukabidhi bendera na mapokezi ikibidi."

Walikuwa wakiujibu ujumbe kwenye ukurasa wao wa Twitter wa Jamii Forums waliokuwa wameandika: "Julai, 26 BASATA ilimzuia Msanii Diamond kwenda kufanya 'show' nje ya nchi akiwa katika uwanja wa JKNIA kwa kukosa kibali kutoka BASATA."

Mwezi Agosti, taarifa zilisambaa mtandaoni kwamba Diamond alikuwa amezuiwa kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya sherehe ya siku ya kuzaliwa kwa mwanawe.

Basata walikanusha taarifa hizo na kusema ni za uzushi. Walisema: "Taarifa inayosambaa kwamba Msanii Diamond anatakiwa kuchukua kibali kwenda kuhudhuria sherehe ya kuzaliwa mwanaye si ya kweli.Vibali vya kwenda nje havihusiani na safari binafsi.Tunawakumbusha wasanii kufuata taratibu zote wanapoenda kufanya maonesho nje ya nchi."

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii