Ole Gunnar Solskjaer: Mkufunzi wa muda wa Man United aahidi kuwafanya wachezaji kufurahia soka tena

Mkufunzi wa muda wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Ole Gunnar Solskjaer alifunga jumla ya mabao 126 katika misimu 11 kama mchezaji wa Man U

Mkufunzi wa muda wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer, anasema kwamba atahakikisha kuwa "wachezaji wake wanafurahia kabisa kandanda" tena, baada ya kufutwa kazi kwa mkufunzi mtangulizi wake Jose Mourinho.

Siku ya Jumatano wiki hii, Timu ya Man United, ilimteua mshambulizi huyo wa zamani kushikilia uongozi wa timu hiyo ya Uingereza hadi mwisho wa msimu, siku moja tu baada ya Mourinho kutimuliwa.

Solskjaer, mwenye umri wa miaka 45, anachukua uongozi wa United wakati ambapo timu hiyo inashikilia nafasi ya 6 katika jedwali la msimamo wa ligi kuu ya Premia.

Raia huyo wa Norway, amekiambia kituo cha runinga cha timu hiyo, MUTV, kuwa anataka kuwaona wachezaji, "wakijieleza" wakati wote atakapokuwa akiwaongoza.

"Tutahakikisha wachezaji wanafurahia soka na kisha kupata uungwaji mkubwa tena, " amesema.

Mourinho alifutwa kazi baada ya kutoandikisha matokeo mazuri au kutokana na mbinu zake za uongozi licha ya kutumia zaidi ya pauni milioni 400, kuwanunua wachezaji 11, katika misimu miwili na nusu, huku nyingi ya mechi za Man U msimu huu, ikizidi kudorora.

Man United inatazamia kumteuwa mkufunzi rasmi mwishoni mwa msimu huu.

Solskjaer alitumia misimu 11 uwanjani Old Trafford, na kufunga bao la ushindi katika mchuano wa Klabu Bingwa Ulaya mnamo mwaka 1999 , na amesema kurejea tena kwake "ni sawa na kurudi nyumbani".

Alipoulizwa kuhusu wasifu wake wa kuwa kipenzi cha mashabiki, alijibu huku akicheka: "Hadi lini hilo litadumu?"

Pia amewaahidi mashabiki kuwa, atafanya "kila awezalo" ili "kuiletea klabu hiyo ushindi" na kuwafanya wachezaji "kufurahia soka".

"Inafaa turejeshe hadhi yetu ya awali ya kuendelea kushinda daima, na kisha kupata mataji," aliongeza.

"Chochote kilichotokea kimeshatokea na kila mtu anafaa kuanza upya."

Chanzo cha picha, Getty Images

Mechi ya kwanza ya Solskjaer akiwa mkufunzi itakuwa dhidi ya Cardiff kesho Jumamosi- kocho huyo aliifunza Cardiff kwa miezi minane mpaka walipoteremka daraja mwaka 2014.

Anajiunga United akitokea Molde ambayo kwanza alianza kuifunza kati ya mwaka 2011 hadi 2014, alichukua ushindi wa ligi kuu nchini Norway mara mbili na mara moja akanyakuwa kombe kuu la soka bado nchini Norway.

Alirejea tena katika klabu hiyo mwaka 2015 na akatia saini mkataba mpya mapema mwaka huu.

"Kuna makosa mengi mtu anafanya, hasa anapoendelea kujifunza, lakini mimi nishafanya makosa machache," amesema.

"Nimewahi shinda ligi kuu, nimepata kombe, na pia nimewahi shushwa daraja, sasa ndio mwanzo ninafahamu zaidi taaluma hii."

Michael Carrick na Kieran McKenna, ambao ni sehemu ya wakufunzi waliokuwa chini ya Mourinho, wataendelea kuwa chini ya Solskjaer.

Solskjaer anasema kwamba, anahisi kuleta "ujuzi" wa Mike Phelan, ambaye pia anarejea Old Traford kama kocha wa kwanza wa kikosi, ambapo awali alifanya kazi kama naibu mkufunzi mkuu wa Man U, kwa pamoja na Sir Alex Ferguson.

"Amefanya mengi, ni mkufunzi mahiri aliyenipa tajriba hii na ujuzi wake katika kandanda ni nzuri sana," aliongeza Solskjaer.