Kijana maskini adaiwa mamilioni baada ya kugonga magari matatu ya Ferrari Taiwan

Yellow Ferrari

Chanzo cha picha, New Taipei City Police Department

Maelezo ya picha,

Bima ya Lin Chin-hsiang hakuwa imesimamia uharibifu kama huo

Kijana mmoja nmdogo wa Taiwan ambaye alisinzia huku akiendesha gari na kugonga magari matatu ya kifahari aina ya Ferrari amepata mshituko wa maisha baada ya kuambiwa itamgharimu dola za Taiwan milioni 12 ($390,000) kulipia gharama za kukarabati gari hilo.

Lakini watu mbali mbali wameonyesha nia ya kumuunga mkono kwa kutoa michango yao kutoka sehemu mbali na kumsaidia kulipa pesa ambazo awali ilionekana haiwezekaniki kwake kulipa.

Upendo wao umemshangaza kijana huyo wa miaka 20.

Kisa cha kijana huyo Lin chin-hsiang kimezungumziwa sana Taiwan watu wakionyesha kutoridhishwa na utofauti mkubwa wa kiuchumi katika kisiwa hicho kati ya matajiri na maskini, hali iliyopelekea wale wenye kipato cha chini kama kijana Lin kuhaha angalau kujipatia mahitaji muhimu.

Kijana huyo mdogo anayelelewa na mama peke yake aliacha shule mwaka huu ili kumsaidia mama yake anayefanya kazi katika duka la familia.

Baba yake alifariki kwa ugonjwa miaka michache iliyopita.

Anafanya kazi zamu ya usiku katika mgahawa wa kuchoma nyama, alipomaliza zamu majira ya saa tisa usiku Jumapili alirudi nyumbani na kumkuta mama yake anaumwa, hivyo akaamua kumsaidia kupeleka bidhaa iliyoagizwa katika hekalu jirani.

Ilikuwa ni majira ya saa kumi na moja alfajiri, alikua amechoka sana baada ya kufanya kazi usiku mzima, akasinzia akiwa anaendesha gari na kugonga magari hayo ya kifahari aina ya Ferrari.

Chanzo cha picha, New Taipei City Police Department

Maelezo ya picha,

Lin Chin-hsiang alikuwa anamsaidia mamake kufikisha bidhaa kwa mteja baada ya kufanya kazi hotelini usiku kucha. Gari la Lin pia liliharibika.

Magari hayo matatu yalikuwa ni miongoni wa magari manne ya kifahari yanayomilikiwa na marafiki ambao walikutana hapo. Wamiliki walikuwa wamesimama pembeni mwa magari hayo hivyo hakuna aliyejeruhiwa.

"Nilishituka sana, nikasema nimejiingiza kwenye balaa kubwa, nilihofia zaidi kumletea matatizo mama yangu kwa kulipa pesa nyingi sana wakati nia yangu ilikuwa kumsaidia mama yangu, ila ndio kwanza nikaharibu," Lin aliiambia BBC siku ya Jumatano.

Polisi walisema hakuwa amelewa na hana historia ya kulewa.

Vyombo vya habari vya ndani vikatafuta wataalamu wa magari ambao baada ya kupiga hesabu ya matengenezo ikaja dola milioni 12 za Taiwan.

Maelezo ya picha,

Eneo la ajali

Baada ya hapo Lin na familia yake wakajikuta wamepigwa na butwaa la maisha, wakifikiria watawezaje kulipa pesa zote hizo.

Cha ajabu maelfu ya watu walipiga simu polisi na kujitolea kumchangia kijana huyo ili aweze kulipa deni hilo. Baadhi ya watu walienda katika duka la mama yake ili kutoa misaada yao.

Mamlaka ya mji huo imewaelekeza watu wanaotaka kumsaidia Lin kutuma pesa hizo katika akaunti maalumu ya benki.

Zaidi ya michango 100 imeshapokelea na kufikia dola za kimarekani elfu 24000.

Hata hivyo shule aliyokuwa ameacha wamemualika arudi kwani alikuwa katika mwaka wake wa mwisho ambapo baba yake alifariki na yeye mdogo wake alikuwa anasoma.

Chanzo cha picha, New Taipei City Police Department

Maelezo ya picha,

Wamiliki wa magari hayo ya Ferrari walikuwa wanaenda safari ya pamoja

Watu mbali mbali wamewaomba wamiliki wa magari hayo ya kifahari kutomdai chochote Lin kutokana na historia ya maisha yake. Lakini mmiliki mmoja akaweka wazi kuwa anahitaji alipwe kwani anafanya kazi kwa nguvu zote mpaka kumiliki gari hilo.

Hata hivyo Lin anasema wamiliki hao wamekuwa wapole sana kwake kwani wamemruhusu kulipa kidogo kidogo.

Kwa mshahara wake wa mwezi inakadiriwa itamchukua miaka 28 kulipa deni hilo kwani gari la familia alilokuwa akiendesha lilikuwa na bima ya kulipia majeruhi tu na si matengenezo.

Na anasisitiza kulipa pesa hizo ni kitu chema hivyo lazima alipe.

"Wanisamehe sana haikuwa kusudi langu, japo itanichukua muda mrefu ila nimefanya kosa nitalipa tu"