BASATA yahaha kuhusu kusafiri kwa Diamond Platnumz na Rayvanny Kenya

Diamond

Utata umegubika kilichotokea hadi wanamuziki Diamond Platnumz na Rayvanny waliokuwa wamefungiwa kufanya maonesho ndani ya nje ya Tanzania wakaondoka nchini humo kwenda Kenya.

Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limeonekana kukanusha kuwapa idhini ya kuandaa maonesho ndani na nje ya nchi hiyo, ingawa kwa njia inayokanganya.

Ijumaa, Diamond na Rayvanny kupitia wa Instagram, walipakia video wakiomba radhi.

Baadaye, walijitokeza eneo la Westlands jijini Nairobi nchini Kenya na kueleza kwamba walikuwa wamewasilisha barua kwa Basata kujitetea na wakapewa idhini.

Lakini baraza hilo limekanusha hilo na badala yake likadai wawili hao walitoa taarifa za uongo.

"Wasanii @diamondplatnumz na mwenzake Rayvanny hawajaondolewa adhabu ya kutofanya onesho ndani na nje ya nchi kufuatia kupuuza adhabu ya awali iliyowaelekeza kutoutumia wimbo wa 'Mwanza' uliofungiwa kutokana na maudhui machafu na yasiyo na staha," ujumbe wa kwanza wa Twitter uliopakiwa kwenye ukurasa rasmi wa Basata unasema.

"Itakukumbukwa kwamba Wasanii hawa huku wakijua wimbo huo umefungiwa waliutumia katika moja ya onesho la Tamasha la Wasafi ambalo nalo kibali chake kimesitishwa kufuatia kukiuka kanuni ma taratibu za uendeshaji matukio ya Sanaa," ujumbe wa pili unasema.

Maelezo ya video,

Diamond Platnumz aeleza yeye na Rayvanny walivyojitetea Basata, Tanzania kuhusu Mwanza

Jumamosi, taarifa iliyotiwa saini na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Onesmo Kayanda, ilitolewa lakini baada ya muda inaonekana kuondolewa mitandaoni.

Chanzo cha picha, TWITTER

Maelezo ya picha,

Ujumbe huu wa Basata unaoonekana kupakiwa kwenye Instagram haufungui

Lakini wa Twitter uliokuwa umeambatishwa kiunganishi cha ujumbe wa Instagram bado upo, ingawa kiunganishi hicho cha Instagram hakifungui.

'Hatua kali zaidi'

Taarifa iliyotolewa na Bw Kayanda ilisema: "Ikumbukwe kuwa Desemba 18 tuliwafungia kutojihusisha na sanaa kwa kipindi kisichojulikana kwa kuimba kwa makusudi wimbo Mwanza tulioufungia kwa sababu za kimaadili.

"Baraza linasisitiza kuwa halijawafungulia wasanii hao, pia linawaonya kuacha kutoa taarifa za uongo kabla halijawachukulia hatua kali zaidi."

Maelezo ya picha,

Queen Darleen na Rayvanny

Juhudi zetu za kutafuta ufafanuzi kutoka kwa maafisa wa Basata bado hazijafua dafu, kwani simu zao hazipokelewi.

Ijumaa, baada ya kutolewa kwa taarifa ya Diamond, walikuwa wamedokeza kwamba bado kulikuwa na majadiliano zaidi yaliyokuwa yakiendelea na hawakuwa tayari kuzungumzia hilo.

Baadaye, simu zao zilikuwa hazipokelewi.

Diamond alikuwa amesemaje?

Diamond, akiandamana na mwenzake Rayvanny na Queen Darleen, aliwaambia wanahabari Nairobi kwamba waliiandikia serikali barua kueleza kwamba walikubali walikuwa wamekosea kuucheza wimbo wa Mwanza uliofungiwa kwenye shoo yao eneo la Mwanza mwishoni mwa wiki.

Kwenye barua hiyo, walijitetea kwamba awali, hawakuwa wameucheza wimbo huo kwenye shoo zao.

Kinachozua utata ni iwapo barua hiyo yenyewe iliandikiwa Basata au iliandikiwa taasisi nyingine za serikali. Kwa jumla walitakiwa kulipa faini ya Tshs 9 milioni, Diamond, Rayvanny na wasafi Limited kila mmoja akilipa shilingi milioni tatu.

Basata wenyewe bado hawajazungumzia hilo.

Kadhalika, walieleza kwamba marufuku dhidi yao ingewaharibia sifa na pia kuwasababishia hasara kutokana na tamasha zao walizokuwa wameandaa kipindi hiki cha sikukuu.

“Na tukawaambia pia kwamba tuna shoo nyingine ambazo ziko Kenya, na sehemu tofauti ambazo tayari zishalipwa (tiketi zishalipiwa),” amesema Diamond.

“Kwa hivyo, tusipotumbuiza pia tutatengeneza picha mbaya, pia na hasara kwa sababu pia sisi tunafanya biashara.”

Diamond, ambaye jina lake halisi ni Nasibu Abdul Juma Issaack na Rayvanny ambaye jina lake halisi ni Raymond Shaban Mwakyusa, wamepanga shoo kadha nchini Kenya chini ya Wasafi.

Jumatatu 24 Desemba watakuwa mjini Embu, kisha watumbuize Mombasa tarehe 26 Desemba kabla ya kurejea Nairobi Mkesha wa Mwaka Mpya.

Diamond ana shoo pia visiwani Comoro mnamo 28 Desemba.

Basata ni nani hasa?

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ni Shirika la umma lililoundwa kwa Sheria ya Bunge Na. 23 ya Mwaka 1984.

Sheria ya kuunda upya Baraza hili ilifanywa kwa kuunganishwa Sheria ya Baraza la Sanaa la Taifa ya Mwaka 1974 na Baraza la Muziki la Taifa (BAMUTA) ya Mwaka 1974. Baraza liliundwa ili lisimamie maendeleo ya sanaa nchini Tanzania.

Dira yake ni Kuwa chombo chenye uwezo wa hali ya juu wa kutoa huduma bora kitaifa katika maendeleo ya sanaa, na Lengo la e kuu ni Kufufua, kukuza na kuongeza maendeleo ya utengenezaji wa kazi bora za sanaa.

Maadili ya msingi ya Baraza la Sanaa la Taifa, kama yalivyoelezwa kwenye tovuti yake, ni "kuhimiza na kukukuza utamaduni halisi wa sanaa ya Kitanzania, kudumisha ubobezi na ubora wa hali ya juu na kuchochea ubunifu na uvumbuzi katika sanaa", na katika hili, limepania kuhimiza na kukuza utamaduni halisi wa sanaa ya Kitanzania, kudumisha ubobezi na ubora wa hali ya juu na kuhimiza ubunifu na uvumbuzi katika sanaa.

Mwenyekiti wa bodi ya BASATA ni Bw Habbi Gunze aliyeteuliwa na Rais Magufuli mnamo 1 Oktoba.

Wajumbe watano wa bodi ya baraza hilo Dkt Emmanuel Mwesiga Ishengoma, Bw Hamis Mwinjuma, Dkt Saudin Jacob Mwakaje, Bw Single Mohammed Mtambalike na Dkt Asha Salim Mshana ambao wana dhamana ya kuhudumu hadi mwaka 2021.