Krismasi: Sikukuu ya kuzaliwa kwa Yesu ilipopigwa marufuku Uingereza na Marekani

Engraving depicts Puritans about to emigrate from England, dated 14th century

Chanzo cha picha, Universal History Archive

Maelezo ya picha,

Waumini wa Puritan walikuwa na msimamo mkali wa kimaadili

Wakati mamilioni ya watu duniani kote wakisherehekea msimu wa huu wa Sikukuu, karne kadha zilizopita baadhi ya Wakristo walipiga marufuku kusherehekea siku ya Krismasi.

Kulikuwepo wakati ambapo Waingereza waliona haja ya kudhibiti shughuli ambayo waliiona imekuwa kinyume na mafundisho ya Kikristo.

Kila Desemba, ilikuwa imeanza kuwa kawaida kwa watu kutekwa na hisia na msisimko, na kujihusisha na matendo ambayo hayakufuata mafundisho ya dini.

Kunywa pombe kupita kiasi, mkusanyiko wa watu wengi wanaopiga kelele za shangwe, biashara kufungwa mapema, familia na marafiki kujumuika pamoja kwa ajili ya chakula maalum cha sikukuu, nyumba kupambwa kwa miti na hata mitaani nyimbo za Krismasi kutawala.

Hii ilikuwa dhambi.

Sikukuu yenyewe ilikuwa Krismasi.

Wakristo wa kweli

Mwaka 1644, walokole wa Kiprotestanti nchini Uingereza ambao walifahamika kama Puritans walinuia kuifuta kabisa sikukuu ya Krismasi.

Walikuwa ni kundi ya Wakristo waliokuwa na msimamo mkali na walipigania kutekelezwa kwa mafundisho ya dini kikamilifu.Serikali ya wakati huo ilikuwa ya Puritan na waliitazama Krismasi kama sikuu ya watu wasiokuwa na dini, au wapagani).

Waliamini kwamba hakukuwa na pahala popote kwenye Biblia ambapo ilikuwa imeandikwa au kudokezwa kwamba Yesu Kristo alizaliwa 25 Desemba.

Mbona basi tarehe hiyo ilikuwa inasherehekewa kama siku ya kuzaliwa kwa Yesu? Hawakufurahishwa na hilo.

Kwa kiasi fulani, walikuwa sahihi.

19th century English illustration about Christmas

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Majani yaliyotumiwa wakati huo yalionekana sana kama ya Kirumi kwa watu hao wa Puritan

Turudishie Krismasi yetu!

Sherehe zote za krismasi zilipigwa marufuku Uingereza hadi kufikia mwaka 1660.

Tarehe 25 Desemba, maduka yote yalilazimishwa kuwa wazi, na makanisa yakashurutishwa kufunga milango yao.

Ilikuwa kinyume cha sheria kuandaa ibada za Krismasi.

Marufuku hiyo haukukubaliwa kwa urahisi.

Maandamano yalifanyika yakidai uhuru wa kunywa pombe, kuimba na kufurahia siku kuu hiyo.Ilikuwa ni baada ya Charles wa pili kuwa mfalme ndio sheria hiyo ya kupiga marufuku Krismasi ilipoondolewa.

Utamaduni wa kuandaa sherehe na kufanya shangwe ni jambo ambalo lilidharauliwa na waumini wa Puritan wa Marekani pia.

Illustration called 'Christmas under the Commonwealth'

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mchoro unaomuonyesha mwumini wa Puritan akiwashutumu watoto kwa kujaribu kusherehekea Krismasi

Na Marekani pia walipiga marufuku sherehe hizo wakiwa na sababu zinazofanana na za Uingereza.

Katika jimbo la Massachusetts, Marekani hawakuwa na Krismasi kati ya mwaka 1659 mpaka 1681.Hata baada ya marufuku ya sherehe za Krismasi kufutwa, waprotestanti wengi waliendelea kuamini kuwa sherehe ya Krismasi ni ya wapagani na imelaaniwa.

Yesu alizaliwa lini?

Bado hakujakuwa na maafikiano kuhusu ni lini hasa Yesu alizaliwa.

Wataalam wa dini wanafikiri kwamba labda ilikuwa majira ya kuchipua kwa sababu kuna taarifa za wachungaji wakiwa nyikani wakiwachunga kondoo wao.

Ingekuwepo Desemba, ambapo huwa msimu wa baridi, basi hawangekuwa malishoni, wangekuwa wametafuta hifadhi maeneo yenye joto.

Au pengine ilikuwa majira ya kupuputika kwa majani. Kuna uwezekano kwamba wachungaji walikuwa wanawaangalia kondoo wao msimu wao wa kupandana ili kuwatenganisha kondoo jike ambao tayari walikuwa wamepandwa na kutungishwa mbegu.

Biblia haijatoa tarehe yoyote.

Sherehe ya wapagani

Lakini tunafahamu kuwa kumekuwa na msimu wa matamasha na sherehe za wapagani mwishoni mwa Desemba tangu wakati wa Warumi, ambao ulikuwa utamaduni wa wapagani.

Bacchanalian Group, 1852, illustration by John Leech

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Picha hii ya ucheshi ya karne ya 19 inaonyesha Warumi walipenda sana kusherehekea

Ilikuwa ni tamasha la mavuno ambapo zawadi zilikuwa zinatolewa, nyumba zinapambwa kwa maua, chakula kilikuwa kingi cha kusaza na vinywaji vya kulewesha vilikuwepo tele.

Kwa mujibu wa mtaalam wa historia Simon Sebag Montefiore, Wakristo wa enzi hizo walilazimika kujaribu kushindana na raha na starehe ambazo ziliahidiwa na sherehe za kipagani wakati huo.

Warumi aste aste waliacha upagani na kuingia kwenye Ukristo.

Lakini kubadilika huku kwa imani yao kulibadilisha kalenda ya Kikristo.

Kwa kipindi fulani, Warumi walisherehekea tamaduni zote mbili.

Kufikia mwisho wa karne ya 4, matambiko na sherehe za kipagani za Kikristo zilifanyika kwa pamoja kwa kipindi cha siku 14 mwezi Desemba.Lakini hilo halikufanyika bila mfarakano.

Washindi na walioshindwa

Mwisho wa siku, wakristo walishinda.

Cartoon by George Cruikshank depicts a gluttonous man devouring a Christmas feast.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Wakati wa Krismasi, huwa wakati wa kula vyakula vitamu tamu miongoni mwa mengine. Lakini ulafi unaweza kuwepo!

Vita dhidi ya Krismasi vya karne ya 17 (miaka ya 1600), vilikuwa jaribio la kufuta kile ambacho Puritan walikitazama kama masalio ya utamaduni wa wapagani katika Ukristo.

Lakini hebu tazama yanayojiri kwa sasa. Bila shaka walishindwa.

Krismasi kote duniani huwa msimu wa sherehe, kula vinono, mapambo, kuvalia mavazi mapya na ya kupendeza, kujumuika na marafiki, kuwatembeleza marafiki, kuwajulia hali wazazi, kwenda likizoni, kufurahia kwa pombe na vileo na kadhalika.

Watu wengi huisherehekea siku hii kwa mtazamo wao wenyewe.