Iran yamyonga mfanyabiashara ajulikanaye kama 'Sultani wa Bitumen' kwa sababu ya rushwa

Screen grab from Irna of Hamidreza Baqeri Darmani in court

Chanzo cha picha, IRNA

Maelezo ya picha,

Kesi ya Hamidreza Baqeri Darmani ilitangazwa hadharani kwenye TV

Mfanyabiashara mashuhuri nchini Iran anayefahamika kama "Sultani wa Bitumen", amenyongwa baada ya kupatikana na hatia ya kutoa rushwa na kujihusisha na ufisadi.

Hamidreza Baqeri Darmani alipatikana na hatua ya kughushi nyaraka ndipo apate mikopo ambayo ilikuwa ikitolewa kwa ushirikiano na serikali.

Kisha, alitumia kampuni mbalimbali kujinunulia zaidi ya tani 300,000 za bitumen - kemikali inayotumiwa kutengeneza lami - moja ya biashara zenye faida kubwa ziadi Iran.

Darmani, 49, ndiye mfanyabiashara wa tatu kunyongwa tangu operesheni ya sasa ya kukabiliana na rushwa kuanzishwa mapema mwaka huu.

Mwezi jana, Iran ilimnyonga mfanyabiashara wa sarafu aliyefahamika kama 'Sultani wa Sarafu', kwa kujilimbikizia tani mbili za sarafu ya dhahabu.

Kwa mujibu wa kituo cha habari za idara ya mahakama cha Mizan, Darmani alinunua bitumen ya thamani ya zaidi ya $100m (£79m) kupitia "ulaghai, kughushi nyaraka na kutoa rushwa."

Alikamatwa Agosti 2014.

Taarifa za kunyongwa kwa Darmani zimepeperushwa kwa kina na runinga ya taifa ya Iran, ambapo hata waliongeza sauti kama za filamu kuifanya ya 'kuogofya zaidi'.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

'Sultani wa Sarafu' pia alinyongwa mwezi jana. Alikamatwa Julai mwaka huu

Wachanganuzi wanasema serikali inataka sana kuonyesha ilivyojitoleza katika kuwaadhifu wanaofuja mali ya umma na kutaka kujitajirisha na uchumi wa taifa hilo ambao unayumbayumba.

Agosti, mahakama mpya za "kimapinduzi" zilianzishwa ili kuharakisha kesi zinazohusu ufisadi, na wafanyabiashara kadha wamefungwa.

Kunyongwa kwa mwanabiashara huyo kumetokea huku umma ukiendelea kulalamika kuhusu ongezeko la gharama ya maisha na ufisadi.

Uchumi wa Iran umedorora, kwa sehemu fulani kutokana na vikwazo ambavyo taifa hilo limewekewa na Marekani.