Maandamano Sudan: Polisi wakabiliana na wapenzi wa mpira wa miguu wanaompinga Omar al-Bashir

demonstration in Atbara on 20 Dec

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Maandamano yamepamba moto kwa siku tano mfululizo

Polisi nchini Sudan wamewatimulia mabomu ya machozi mashabiki wa mpira mabao walikuwa wakiandamana kutaka kung'atuka kwa rais Omar al-Bashir.

Maandamano yaliyoanza wiki iliyopita yametanda nchi nzima huku waandamanaji wakitaka kuondoka kwa raisi huyo aliyedumu madarakani kwa miaka 29.

Mamia ya waandamanaji walizuia barabara moja iliyokaribu na uwanja wa mpira katika mji mkuu wa Khartoum, siku ya Jumapili kisha kukabiliana na polisi wa kutuliza ghasia.

Viongozi wa upinzani wanadai watu 22 wameuawa toka Jumatano ya wiki iliyopita, lakini viongozi wa serikali wanadai idadi hiyo imetiwa chumvi.

Maandamano hayo yalilipuka baada ya kuongezeka kwa bei ya mafuta mkate. Lakini sasa yamechukua sura mpya ya kutaka uongozi wa Bwana Bashir ufikie tamati.

Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita bei ya baadhi ya bidhaa muhimu zimeongezeka mara mbili nchini Sudan huku mfumuko wa bei kufikia asilimia 70.

Thamani ya sarafu ya nchi hiyo imeporomoka mara dufu na tayari kuna uhaba wa pesa katika miji mikubwa kama Khartoum.

Madaktari nao wamejitosa katika maandamano hayo leo Jumatatu ili kuongeza shinikizo dhidi ya Bashir shirika la habari la Associated Press limeripoti.

Bashir alichukua hatamu za uongozi katika mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika mwaka 1989.

Yapi yamejiri?

Maandamano ya Jumapili yalitokea wakati mamia ya watu wakitoka kutazama mechi ya mpira wa miguu.

Waifunga barabara na kisha kuanza kuimba nyimbo dhidi ya serikali kabla ya polisi kuwarushia mabomu ya machozi ili kuwatanya.

Awali, picha za video zilizotumwa kwenye mitandao ya kijamii zilionesha maadamano hayo yaliendelea katika baadhi ya maeneo ya jiji.

Kamati Kuu ya Madaktari nchini Sudan imesema wanachama wake wamewapokea waandamanaji waliopata majeraha ya risasi na kuwa kuna watu kadha waliouawa.

Presentational white space

Jumamosi mamlaka ziliwatia nguvuni viongozi 14 wa muungano wa upinzani wa National Consensus Forces akiwemo kiongozi wao Farouk Abu Issa mwenye umri wa miaka 85.

"Tunataka waachiwe huru mara moja, na kukamatwa kwao ni jaribio la dola kusimamisha harakati za mitaani," msemaji wa kundi hilo Sadiq Youssef amenukuliwa akisema.

Wapinzani wanasemaje?

Jumamosi, Sadiq al-Mahdi, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Umma, alipinga vikali "ukandamizwaji wa kijeshi" na kudai maandamano yamezalishwa na hali mbaya iliyoikumba nchi.

Pia ameitaka serikali ya Bashir kuachia madaraka kwa amani ama kukakabiliana na uma wa Wasudani.

"Itakuwa ni mpambano ambao serikali itashindwa, itaongeza makosa ya serikali na kuhitimisha muda wake," gazeti la Sudan Tribune lenye maskani yake Paris, Ufaransa limenkuu al-Mahdi akisema hivyo.

Sadiq al-Mahdi in Omdurman

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Kiongozi wa upinzani Bw Mahdi amedai watu 22 wameuawa mpaka sasa

Bw Mahdi - ambaye alipata kuwa Waziri Mkuu kati ya 1966 na 1967 na kwa mara ya pili kuanzia 1986 mpaka 1989 - amerudi Sudan Jumatano wiki iliyopita baada ya kuishi uhamishoni kwa takribani mwaka mmoja.

Serikali yake ndiyo ilikuwa ya mwisho kuchaguliwa kidemokrasia na aling'olewa madarakani kwa nguvu ya jeshi na Bashir ambaye anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai kwa makosa ya kivita na uhalifu dhidi ya binaadamu katika jimbo la magharibi la Darfur.

Maandamano yalianzaje?

Yalianza katika mji wa mashariki wa Atbara ambapo waandamanaji walichoma moto ofisi za chama cha Bw Bashir cha National Congress Party (NCP).

Mashuhuda wanadai kuwa katika baadhi ya maeneo, jeshi wala halikuingilia kati na lilionekana likiwa upande wa waandamanaji.

Mshauri wa rais Bashir Faisal Hassan Ibrahim, amesema kuwa waandamanaji walikuwa wakiongozwa na "taasisi zilizojipanga", lakini hakutoa maelezo ya ziada.

Omar al-Bashir (R) seen visiting President Assad in Syria in December 2018

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Bw Bashir - akilakiwa piachani na rais wa Syria Bashar Assad mapema mwezi huu - ameahidi kung'atuka mwaka 2020

Maandamano yakaenea mpaka jijini Khartoum na kisha Omdurman pamoja na maeneo mengine.

Jumamosi, shirika la habari la AFP limewanukuu mashuhuda katika eneo la Wad Madani, kusini mashariki mwa Khartoum wakisema polisi walitumia mabomu ya machozi na kuwapiga waandamanaji ambao walikuwa wakitaka Bashir aondoke madarakani.

Huko El Rahad, kusini magharibi mwa Khartoum, ofisi ya chama cha NCP pamoja na ofisi nyengine za utawala zilipigwa kiberiti huku waandamanaji waliokuwa wakiimba "hapana kwa njaa"wakimiminiwa mabomu ya machozi, shuhuda mwengine alieleza.

Kwa nini Sudan ina hali mbaya kiuchumi?

Bw Bashir alituhumiwa kufadhili ugaidi na Marekani kwenye miaka ya 90 na Sudan ikawekewa vikwazo ya kibiashara.

Mwaka 2011, Sudan Kusini ilijitenga na kuwa nchi hur huku ikiondoka na robo tatu ya maeneo ya uzalishaji wa mafuta. Utengano huo wa Sudan ulifuatia miongo kadha ya vita ya wenyewe kwa wenyewe iiliyogharimu maisha ya watu milioni 1.5.

Wakati huo huo, mgogoro wa Darfur umewakimbiza watu milioni mbili kutoka kwenye makao yao na kupelekea vifo vya watu zaidi ya laki mbili (200,000).

US sanctions were lifted in 2017 but there has been little improvement in the country's economy since.