Papa akemea maisha ya anasa na umasikini wa kutupwa

Pope Francis leads the Christmas Eve mass in Saint Peter's Basilica at the Vatican, December 24, 2018

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Hii ni Krismasi ya sita kwa Papa Farncis, 82, akiwa kama kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani.

Papa Francis amewataka watu wanaoishi katika nchi zilizoendelea kuishi maisha ya kawaida na kupunguza anasa.

Pia amekemea pengo kubwa lililopo duniani baina ya masikini na matajiri, na kutaka watu watilie maanani katika kuyaendea maisha yao kuwa Yesu alizaliwa kwenye umasikini, kwenye hori la kulishia ng'ombe.

Papa amaeyaongea hayo wakati akiongoza Misa ya Mkesha wa Krismasi katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Hii ni Krismasi ya sita kwa Papa Farncis, 82, akiwa kama kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani.

Katika mahubiri yake, Papa amesisitiza kuwa kuzaliwa kwa Kristo kunaashiria mfumo mpya wa maisha "si ya ulafi na kuhodhi bali kutoa na kugawa kwa wengine pia."

Hebu tujiulize: Je ni kweli nahitaji nahitaji mali zote hizi na vitu vingine vianvyochangia maisha kuwa magumu? Je naweza kuishi maisha bila kuwa na vitu vya ziada ambavyo si vya msingi na kufanya maisha yangu kuwa mepesi?"

"Kwa waliowengi, maana ya maisha inapatikana katika kumiliki mali na kuwa na ziada ya kutosha. Kiu hii ya ulafi inamulika historia yote ya mwanadamu, hata leo, wachache wanapata mlo wa anasa wakati wengi wanashindwa walau kupata mkate wao wa kila siku wanaohitaji ili kuweza kuishi."

Chanzo cha picha, AFP

Leo, Sikukuu ya Krismasi Papa anatarajiwa kutoa ujumbe wake wa "Urbi et Orbi" (kwa jiji na dunia) kutoka kwenye baraza ya ghorofani ya kanisa la Mtakatifu Petro.

Francis, Papa wa kwanza kutoka Amerika ya Kusini amefanya kusemea shida za masikini kama sehemu muhimu wa uongozi wake wa kanisa.

Katika mkesha wa Krismasi wa wa mwaka 2016 Papa huyo alionya kuwa maana halisi ya Krismasi ilikuwa inazamishwa na anasa,

Mtangulizi wake, Papa Benedikto alitoa ujumbe kama huo mwaka 2011.