Mkutano na 'salamu ya mikono' baina ya Rais Kenyatta na kiongozi wa upinzani Odinga ulivyozima mzozo wa kisiasa 2018

Raila Odinga (kulia) amekuwa akikataa kumtambua Uhuru Kenyatta kama rais halali wa Kenya

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Raila Odinga (kulia) amekuwa akikataa kumtambua Uhuru Kenyatta kama rais halali wa Kenya

Kenya iliuanza mwaka huu wa 2018 (uliobakiza siku chache kumalizika) ikiwa ndani ya mtanziko mzito wa kisiasa ambao suluhu yake ilionekana kuwa mbali kufikiwa.

Uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017 ulishuhudia Uhuru Kenyatta akitangazwa mshindi, lakini safari ya mahakamani ya Raila Odinga ikazaa matunda kwa ushindi huo kubatilishwa Septemba mosi.

Kwa amri ya mahakama, uchaguzi wa marudio ukafanyika Oktoba 26, lakini muungano wa upinzani chini ya Raila Odinga ukagomea uchaguzi huo kwa madai kuwa mabadiliko waliyoytaka kufanyika kwenye mfumo hayakufanyika.

Hapo ukaanza ukurasa mpya wa mgogoro wa kisiasa ulozaa vurugu katika baadhi ya maeneo na kupelekea watu kadha kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa hususani kwenye ngome za Odinga kama mgharibi mwa Kenya ambapo baadhi ya Kaunti uchaguzi huo wa marudio ulishindwa kufanyika.

Uhuru alitangazwa tena mshindi, na kuapishwa. Odinga na wafuasi wake wakagoma kumtambua Kenyatta kama rais halali wa nchi.

Katika hatua iliyochochea zaidi mpasuko wa kisiasa, Januari 30 mwaka huu, Bw Odinga alikula kiapo kuwa 'Rais wa Wananchi' na kusisitiza kutomtambua Bw Kenyatta.

Mkutano wa mahasimu

Walipotoka, wawili hao walionekana kuwa na sura za bashasha, na kupeana salamu ya mikono ambayo ndio imekuwa jina la mkutano huo, kwa kingereza wafahamika kama 'The handshake'.

Hiyo ilikuwa ni Machi 9, 2018.

Odinga aliyejilisha kiapo cha 'Urais' siku chache zilizopita aliwashangaza wengi kwa kumuita mtu ambaye alikuwa hautambui uongozi wake kuwa ni "ndugu" na kuongeza kuwa: "Ndugu yangu na mimi tumekutana pamoja leo na kusema yamefikia kikomo. Tumekataa kuwa watu ambao chini yake Kenya imekuwa taifa lililofeli."

Bw Odinga alisema kwa muda mrefu Kenya imeangazia kubadilisha taasisi na miaka saba iliyopita katiba mpya ilianza kutekelezwa.

"Sasa lazima tuwe na ujasiri wa kukubali kwamba hilo halijafanikiwa. Bado hatujabadilisha mengine," amesema Bw Odinga.

Amewataka Wakenya waunge mkono mpango wa viongozi hao wawili.

"Tumesafiri mbali sana kiasi kwamba hatuwezi kurudi tena bandarini. Isitoshe, hatuwezi kufika tunakoenda bila kufanya mabadiliko la sivyo tutazama baharini," amesema Bw Odinga.

"Tumekuja pamoja na ndugu yangu Kenyatta, tumeongea kwa kirefu na kukubaliana kwamba tunataka kuunganisha Kenya iwe taifa moja. Mgawanyiko ambao umekuwepo tangu uhuru utakwisha hapa na sisi. Tutembee pamoja," amesema Bw Odinga.

Wawili hao wakakubaliana kufanya kazi pamoja katika kufanikisha maboresho hayo na kuletea maendeleo Wakenya wote.

Kwa upande wa Kenyatta alisema wamekubaliana na Bw Odinga kwamba taifa la Kenya ni muhimu kuliko mtu binafsi na kwamba lazima viongozi washirikiane.

Rais huyo amesema siku za usoni za Kenya haziwezi kuongozwa na uchaguzi ujao bali "uthabiti wa taifa."

"Demokrasia si mwisho wa kila kitu. Ni shughuli na nia ya wananchi lazima iongoze."

"Tumekubaliana tutaleta pamoja wananchi na kujadiliana kuhusu matatizo yanayoathiri taifa letu na wananchi, na kuunda taifa lenye umoja na lililo imara ambapo hakuna raia anayehisi ametengwa."

"Huu ni mwanzo mpya kwa taifa letu."

"Tunaweza kutofautiana lakini kusalia tukiwa tumeungana kama Wakenya."

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rix Tillerson aliusifu mkutano wa Kenyatta na Odinga.

Mkutano huo ulifanyika muda mfupi kabla ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson kuwasili nchini humo kwa ziara ya siku nne.

Bw Tillerson, akihutubu baadaye aliwasifu wawili hao kwa kukutana.

Marekani ilikuwa mstari wa mbele ikihimiza kufanyika kwa mazungumzo na mashauriano kutatua mzozo wa kisiasa uliokumba taifa hilo baada ya uchaguzi uliojaa utata mwaka jana.

Nini kilichotokea baadae?

Naibu Rais William Ruto alikuwa ni miongoni mwa mamilioni ya Wakenya waliofurahishwa na mkutano huo.

Hata hivyo, kadri siku zilivyoenda mbele, chama tawala cha Jubilee kimeonekana kikisuguana juu ya mkutano wa Kenyatta na Raila.

Wakati wafuasi wa Kenyatta wakisifu hatua ya kiongozi wao katika kumaliza mzozo uliokuwa unatishia usalama wa nchi, wafuasi wa Ruto wamekuwa wakitilia shaka mapatano hayo.

Mpaka sasa wapo wanaoamini kuwa mapatano ya Uhuru na Raila yatakuwa na nguvu ya kuamua nani atakuwa raisi wa Kenya mwaka 2022.

Si siri kuwa Ruto amejipanga kumrithi Kenyatta atakapomaliza nafasi yake, lakini pia si siri kuwa mapatano ya Uhuru na Raila yametia wasiwasi ndoto ya Ruto na wafuasi wake.

Kwa kauli yake mwenyewe, Kenyatta alisema kwenye jumba linalokusanya watafiti na wanazuoni wa siasa wa kimataifa la Chatham jijini London mwezi Aprili kuwa mapatano yake na Odinga hayalengi uchaguzi wa 2022.

Matukio makuu mzozo wa kisiasa Kenya

  • 8 Agosti, uchaguzi mkuu wafanyika ambapo Bw Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi
  • 1 Septemba, Mahakama ya Juu yabatilisha ushindi wa Bw Kenyatta katika kesi iliyowasilishwa na Bw Raila Odinga, na kuagiza uchaguzi urudiwe
  • 26 Oktoba, uchaguzi wa marudio wafanyika, huku upinzani ukisusia. Bw Kenyatta atangazwa mshindi.
  • 30 Januari, Bw Odinga ala kiapo kuwa 'Rais wa Wananchi' na kusisitiza kwamba hatambui Bw Kenyatta kama rais halali wa Kenya
  • 9 Machi, Bw Kenyatta akutana na Bw Odinga katika afisi ya rais Jumba la Harambee, wawili hao waahidi kushirikiana kuwaunganisha Wakenya.