Bobi Wine aendelea kuitikisa Uganda

Bobi Wine

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Bobi Wine mwanamuziki mbunge Uganda

Nyota wa muziki wa pop na mbunge wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi Ssentamu amekataliwa kufanya tamasha lake leo Disemba 26 kama alivyokuwa amepanga hapo awali.

Msemaji wa polisi nchini Uganda, Emilian Kayima amesema kwamba Bobi Wine alikuwa hajaandika barua ya kuomba ruhusa kufanya tamasha hilo ndio maana hawawezi kumruhusu.

"Tutakuwa katika ufukwe wa Busabala kuzuia shughuli hiyo na kuhakikisha usalama upo.Tamasha hili halikuwa limeruhusiwa kufanyika kwa sababu ya kutokidhi vigezo", Kayimba alisema.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor la nchini Uganda limeeleza kwamba mapema leo, Bobi Wine aliandika kwenye mtandao wa kijamii kuwa kikosi cha usalama kimevamia tamasha lake la 'One Love Beach in Busabala'na kuwakamata wafanyakazi wake.

Hili lingekuwa tamasha la pili la Bobi Wine kufanyika, tangu ashtakiwe na kufungwa kwa mshtaka ya uhaini.

Mwanzoni mwa mwezi Novemba mwanamziki huyo aliruhusiwa kufanya tamasha lake la kwanza kwa sababu lilikuwa la kiburudani na halikuwa la kisiasa.

Maelfu ya watu waliohudhuria tamasha hilo walivaa nguo nyekundu, rangi inayohusishwa na vuguvugu za Bobi Wine.

Chanzo cha picha, AFP

Lakini vilevile tamasha hilo lilikuwa na idadi kubwa ya polisi.

Bobi Wine anadaiwa kuteswa na kupigwa akiwa kuzuizi mwezi Agosti, madai yanayokanwa na mamlaka.

Chanzo cha picha, Getty Images

Bobi Wine na wenziwe 32 walikamatwa baada ya kudaiwa kushambulia msafara wa Rais wa Yoweri Museveni mjini Arua mwezi uliopita na kuwekwa katika kizuizi cha jeshi.

Watuhumiwa hao waliwekwa chini ya ulinzi wa jeshi huku Bobi Wine awali akipandishwa katika mahakama ya kijeshi kwa tuhuma za kumiliki silaha kinyume cha sheria.

Rais Yoweri Museveni alijitokeza na kukanusha taarifa kuwa Bobi Wine ameumizwa vibaya na kuvishutumu vyombo vya habari kwa kueneza taarifa za uongo.

Baada ya kelele za upinzani kupazwa ndani na nje ya Uganda pamoja na kwenye mitandao ya kijamii, kesi yake mbele ya mahakama ya kijeshi ilifutwa na kuachiwa huru kabla ya kukamatwa tena na kufunguliwa mashtaka ya uhaini katika mahakama ya kiraia.

Ni kipi kilisababisha mashtaka ya uhaini?

Chanzo cha picha, Getty Images

Kabla hajakamatwa, Bobi Wine, alichapisha picha ya dereva wake ambaye alisema alipiwa risasi na kuuliwa na polisi waliodhani kuwa aliyekuwa ni yeye.

Bobi Wine alikamatwa tarehe 13 Agosti baada ya mkutano wa kampeni kaskazini-magharibi kwenye mji wa Arua ambapo kuna madai kuwa msafara wa rais ulitupiwa mawe.

Mwanamuziki huyo mwenye miaka 36 awali alishtakiwa kwenye mahakama ya kijeshi kwa makosa ya umiliki wa silaha kinyume cha sheria, mashtaka ambayo yalifutwa baadaye. Kisha akafunguliwa mashtaka ya uhaini kwenye mahakama ya kiraia.

Bobi Wine ni nani?

Chanzo cha picha, AFP

Nyota huyu wa mtindo wa Afrobeats aliingia katika taaluma ya muziki katika miaka ya 2000, na anaelezea kipaji chake kuwa ni cha kuelimisha na kuburudisha. Mojawapo ya vibao vyake vya awali Kadingo, inahusu usafi wa mwili.

Alizaliwa 12 Februari 1982, Bobi Wine na alikuwa na miaka minne pekee Museveni alipoingia madarakani mwaka 1986.

Jina lake rasmi Wine, ni Robert Kyagulanyi Ssentamu.

Alilelewa katika mtaa duni wa Kamwokya kaskazini mashariki mwa Kampala na alianza kujihusisha katika muziki mapema miaka ya 2000.

Nyimbo zake za mtindo wa dansi za 'Akagoma' na 'Funtula' zilikuwa maarufu sana miongoni mwa vijana.

Ana shahada ya muziki, dansi na uigizaji kutoka Chuo Kikuu cha Makerere ambapo alihitimu mwaka 2003.

Aprili 2018 alifuzu na stashahada ya masuala ya kisheria kutoka Kituo cha Maendeleo ya Sheria, Kampala.

Alichaguliwa kuwa mbunge katika uchaguzi mdogo baada ya kusimama kama mgombea huru mwaka 2017 wilayani Kyadondo mashariki, Uganda ya kati.

Aliwashinda wagombea kutoka chama tawala National Resistance Movement (NRM) na chama kikuu cha upinzani Democratic Change (FDC).

Baada ya kutangazwa mshindi, aliahidi kuangazia zaidi kuwaunganisha raia.

"Jambo langu la kwanza ninalotaka kufanya ni kufanikisha maridhiano kati ya viongozi wa Kyadondo Mashariki...Ninataka siasa zitulete pamoja... jinsi muziki ufanyavyo."

Ufuasi wa Vijana

Umaarufu wake miongoni mwa vijana nchini Uganda unaonekana kuwa changamoto kubwa kwa rais wa miaka mingi Yoweri Museveni.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Bobi Wine anajiita "Ghetto President" na anaungwa mkono zaidi na vijana

"Chama chake kitawaza iwapo sasa huu ni msururu. Bobi Wine sasa amemshinda Museveni na kiongozi wa upinzani Kizza Besigye mara nne'' katika uchaguzi mdogo.

"Bobi amepata ufuasi kwa nemba yake ya 'nguvu za watu', na ananuia kushinikiza na kupanga liwe vuguvugu," anaongeza.

Mchambuzi wa kisiasa Robert Kirunda anasema mvuto wa Wines unatokana na kuwepo 'pengo la uongozi' Uganda.

"Kuna vijana wengi Uganda ambao hawana haja ya kujua vita vya kihistoria vilivyoiingiza NRM uongozini, au ukaidi wa upinzani mkuu. Wengi wanataka ajira na wanahisi uchumi hauwasaidi."

Kirunda anasema Wine 'anapigia upatu sana'. "Anaweza kushinikiza watu pakubwa, lakini bado hajapata nguvu kama alizonazo Besigye katika upinzani".