Uchaguzi DRC: Kura yaahirishwa mpaka mwezi machi kwa majimbo matatu, wagombea saba wa upinzani walia na tume

UCHAGUZI DRC

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Moshi mkubwa ukifoka kutoka kwenye ghala la tume ya uchaguzi DRC mapema mwezi huu, mashaka yaeemendelea kutanda iwapo uchaguzi wa Congo utafanyika kwa haki

Mustakabali wa uchaguzi nchini Jamuhuri ya Demokrasi ya Congo (DRC) wazidi kuingia dosari baada ya tume ya uchaguzi leo Disemba 26 kutangaza kuahirishwa upigwaji kura katika mikoa mitatu mpaka mwezi machi 2019.

Kura hiyo ambayo ilitakiwa kupigwa Disemba 23 mwaka huu iliahirishwa kwa wiki moja mpaka Disemba 30, yaani Jumapili ijayo. Hata hivyo uchaguzi huo tayari umeshacheleweshwa kwa miaka miwili sasa, huku wapinzani na wanaharakati wakimlaumu rais amalizaye muda wake Joseph Kabila kwa kutafuta visingizio kusalia madarakani. Mgombea wa chama tawala Ramazani Shadary ni mshirika mkubwa wa Kabila na inatarajiwa ataendelea kulinda maslahi ya Kabila akiingia madarakani.

Maeneo hayo matatu ambayo yanaonekana kuwa ni ngome za upinzani ni Beni na Butembo kwa upande wa mashariki ambayo yamekuwa yakipambana na milipuko ya ugonjwa hatari wa Ebol toka mwezi Agosti mwaka huu.

Eneo la tatu ni Yumbi lilopo magharibi mwa nchi ambapo watu zaidi ya 100 wameuawa wiki iliyopita katika makabiliano ya kikabila.

Shughuli za uchaguzi katika sehemu nyengine zote zilizobaki za nchi hiyo kubwa zitaendelea kama ilivyopangwa siku ya jumapili.

Matokeo ya uchaguzi wa maeneo hayo matatu hayataathiri mbio za urais kwa sababu mshindi atatangazwa Januari 15 na kuapishwa Januari 18.

Katika taarifa yake, tume ya uchaguzi (CENI) imesema hatua hiyo inatokana na kusambaa kwa Ebola katika maeneo ya Beni na Butembo pamoja na kudorora kwa amani katika maeneo hayo.

Kampeni DRC
Maelezo ya picha,

Mikutano yote ya Kampeni imepigwa marufuku jijini Kinshasa saa chache kabla mgombea wa upinzani Martin Fayulu kuhutubia wafuasi wake. Katazo hilo la wiki iliyopita bado halijaondolewa.

Tayari hatua hiyo imeshaibua upinzani mkali nchini Congo. Mapema leo kabla ya kutangazwa rasmi kwa uamuzi huo, mgombea kinara wa upinzani Martin Fyulu alionya kuhusu hilo kupitia mtandao wake wa tweeter.

"Kisingizio cha Ebola ni cha uongo sababu kampeni zimefanyika katika maeneo hayo. Hiui ni mbinu nyengine ya kuteka nyara ukweli wa kura," ameandika Fayulu.

Maaskofu wa Kanisa Katoliki ambao wamekuwa mstari wa mbele kupambana ili uchaguzi ufanyike wanatarajiwa kukutana ili kutoa tamko la pamoja kutokana na hatua hiyo mpya.

"Kuahirisha uchaguzi eneo hilo haiwezi eleweka wakati walikubali kampeni ifanyike licha ya uwepo wa Ebola. Mimi binafsi kama raia nawaza kuwa kuna kitu wanaficha. Tunasubiri kwanza sisi Maaskofu tukutane (kabla ya kutoa taarifa rasmi)," amesema Donatien Shole, Katibu Mkuu wa Kanisa Katoliki DRC.

CENI kikaangoni

Mashine hizi za kupigia kura zimekuwa vikipingwa na upinzani
Maelezo ya picha,

Mashine hizi za kupigia kura zimekuwa vikipingwa na upinzani

Wakati huo huo wagombea saba wa urais kutoka upinzani nchini DRC wameituhumu tume ya huru ya uchaguzi nchini humo kuwa na njama kuchakachua matokeo ya uchaguzi mkuu ujao.

Wagombea hao wametoa tuhuma kadha ikiwemo matumizi ya mashine za kielektroniki jambo ambalo wanasema ni kinyume cha sheria.

Pili ni kuweko na taarifa za kuongeza kwa orodha ya wapiga kura kwenye daftari la wapiga kura.

Katika tamko lao ambalo limetiwa saini na wote saba pia wagombea hao wanawataka waangalizi wa kimataifa kutenda haki na kuamua kwa maslahi mapana ya Raia wa DRC.

"...Raia wa DRC wataenda kupiga kura kwa lengo la kuadhibu wale waliokuwa madarakani. Tunapenda mambo yawe wazi na hatutaki siku watakayotangaza matokeo watangaze kile ambacho si matarajio ya Wacongo," amesema Marie Ifoku ambaye ni mgombea pekee mwanamke katika kinyang'anyiro hicho.