Jean-Jacques Savin: Raia wa Ufaransa aanza safari ya kuvuka bahari ya Atlantiki kwa kutumia pipa

Jean-Jacques Savin works on the construction of his barrel at the shipyard in Ares, south-western France, 15 November 2018

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Jean-Jacques Savin ametumia miezi kadhaa kutengeneza pipa hilo katika chelezo kimoja kusini magharibi mwa Ufaransa

Bwana mmoja raia wa Ufaransa ameanza safari ya kuvuka bahari ya pili kwa ukubwa duniani, Atlantiki, kwa kutumia pipa kubwa aliloliunda mwenyewe.

Jean-Jacques Savin, mwenye miaka 71, ameanzia safari hiyo kutoka mji wa El Hierro uliopo kwenye visiwa vya Canary nchini Uhispania na anataraji kufika visiwa vya Caribbean ndani ya miezi mitatu.

Pipa hilo linategemea nguvu ya msukumo ya mawimbi pekee kufanikisha safari. Ndani ya pipa hilo kuna sehemu ya kulala, jiko na stoo ya kuhifadhi vitu.

Bwana Savin pia atakuwa anaweka alama katika safari yake ili kuwawezesha wataalamu wa bahari kuyafanyia tafiti zaid mawimbi ya bahari ya Atlantiki.

Taarifa zote kuhusu mwenendo wa safari hiyo zinawekwa kwenye ukurasa maalumu wa mtandao wa Facebook na ujumbe wa mwisho umeeleza kuwa pipa lilikuwa linaenda vizuri.

Katika mahojiano kwa njia ya simu na shirika la habari la AFP amesema: "Hali ya hewa ni nzuri...naenda kwa kasi ya kilomita mbili mpaka tatu kwa saa...utabiri wa upepo ni mzuri kwangu mpaka siku ya Jumapili."

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Pipa hilo lina sehemu ya kulala na jiko.

Bw Savin ni mwanajeshi mstaafu aliyekuwa akiruka kwa parashuti (askari wa mwamvuli) na pia ameshawahi kufanya kazi kama mlinzi wa mbuga na rubani.

Safari yake inakadiriwa kuwa na umbali wa kilomita 4,500 (maili 2,800) na pipa alitumialo lina urefu wa mita tatu na upana wa mita 2.10.

Kuna tundu lililozibwa na kioo kwa chini linalomuwezesha bw Savin kuona samaki wapitao.

Pipa hilo limetengenezwa kwa umadhubuti kupambana na mawimbi makali na mashambulizi kutoka kwa nyangumi aina ya okra. Pia inatumia umeme wa nguvu ya jua kwa ajili ya mawasiliano na mfumo wa kuweka alama wa kiramani ufahamikao kama GPS.

Bajeti nzima ilikuwa Euro 60,000 na kwa kiasi kikubwa alichangisha kutoka kwa watu.

"Labda (nitafikia) Barbados, japo ningependelea iwe kisiwa cha Kifaransa kama vile Martinique ama Guadaloupe," alisema kwa utani.

"Hiyo itakuwa rahisi sana kwangu kukamilisha kujaza nyaraka na kulisafirisha pipa kurudi nyumbani."

Bw Savarin ameweka kwenye stoo yake mvinyo mweupe kwa ajili ya kusherehekea Mkesha wa Mwaka Mpya na mvinyo mwekundu kwa ajili ya kusherehekea kumbukumbu yake ya miaka 72 ya kuzaliwa Januari 14.