Uchaguzi mkuu DRC: EU yalaani balozi wake kufurushwa DRC

Chanzo cha picha, Getty Images
Polisi walipambana na wafuasi wa upanzi mashariki mwa DRC Alhamisi
Muungano wa Ulaya umeukosoa uamuzi wa Jamhuri ya Demokrasi ya Congo kwa kumfukuza balozi wake kabla ya uchaguzi muhimu nchini humo siku ya Jumapili.
"Amri ya kumtaka Bart Ouvry kuondoka ndani ya saa 48 ni kinyume kabisa na sheria", msemaji wa EU alisema.
DR Congo ilisema ilichukua uamuzi huo kulipiza vikwazo alivyowekewa mgombea wa chama tawala Emmanuel Ramazani Shadary.
Maandalizi ya uchaguzi huo yamekumbwa na ghasia.

Chanzo cha picha, Reuters
Wafuasi wa Martin Fayulu wakiandamana mjini Beni
Siku ya Alhamisi wafuasi wa upinzani walivamia kituo cha Ebola kwenye mji ulio mashariki wa nchi wa Beni kupinga uamuzi wa tume ya uchaguzi wa kuahairisha uchaguzi kwenye miji mingine miwili hadi mwezi Machi.
Ghasia pia zilizuka kwenye miji miwili ngome za upinzani ya Goma na Butembo iliyo yote mashariki mwa nchi.
Tume ya uchaguzi ilisema uchaguzi kwenye miji wa Beni, Butembo na mji ulio magharibi wa Yumbi utaahirishwa hadi Machi kwa sababu ya ukosefu wa usalama na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola eneo la mashariki umesababisha vifo vya zaidi ya wtu 300.

Chanzo cha picha, Reuters
Maafisa wa uchaguzi wamekuwa wakifanyia majaribio mashine kabla ya uchaguzi
Kipi kilisababisha kuzuka mzozo wa kidiplomasia?
Vikwazo kwanza vilitangazwa dhidi ya Bw Shardary mwaka 2017 kwa ukiukaji wa haki za binadamu ikiwemo hatua kali dhidi ya upinzani.
Tarehe 10 Desemba mawaziri wa EU waliongeza vikwazo hivyo vikiwemo vya kuzuia mali na marufuku ya kusafiri kwa Bw Shardary na watu wengine 13 kwa kuhujumu uchaguzi na ukiukaji mwingine wa haki za binadamu.
Siku ya Alhamisi waziri wa mashauri ya nchi za kigeni nchini DRC Leonard She Okitundu, alisema serikali ilikuwa imeitaka EU kufuta vikwazo hivyo hadi baada ya uchaguzi lakini ilikataa.