Uchaguzi DRC: Zoezi la upigaji kura lafika tamati

Vituo vya kupigia kura vimefungwa DRC
Maelezo ya picha,

Vituo vya kupigia kura vimefungwa DRC

Vituo vya kupigia kura vimefungwa kwenye nchi ya pili kwa ukubwa barani Afrika kwenye uchaguzi ambao umechelewa kwa zaidi ya miaka miwili.

Karibu watu milioni 40 wamejiandikisha kupiga kura nchini Jamhuri ya Demokrarsi ya Congo ambapo Rais Joseph Kabila ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2001 anaondoka.

Lakini siku chake zilizopita kumeshuhudiwa ghasia kufuatia uamuzi kwa kuwanyima karibu watu milioni 1.3 haki ya kupiga kura.

Maelezo ya picha,

Vituo vya kupigia kura vimefungwa DRC

Jana Jumamosi wagombea walishindwa kukubaliana kuhusu taarifa ambayo ingepunguza misukosuko kabla ya uchaguzi.

Upigaji kura ulianza mwendo wa saa kumia alfajiri na utaendelra hadi kumi na moja jioni.

Uchaguzi huu unamaanisha nini?

Ikiwa kila kitu kitakwenda sawa bila kisa chochote, hii itakuwa ndio mara ya kwanza kutakuwa na mabadiliko ya amani nchini DRC tangu nchi hiyo ipate uhuru wake kutoka Ubelgiji mwaka 1960.

Maelezo ya picha,

Watu wakiwa foleni kupiga kura mapema leo

Rais wa sasa Joseph Kabila alichukua madaraka kutoka kwa baba yake alipouawa mwaka 2001 lakini anazuiwa kuwania muhula mwingine kulingana na katiba.

Alistahili kuondoka madarakani miaka miwili iliyopita, lakini uchaguzi ulihairishwa baada ya tume ya uchaguzi kusema ilihitaji muda zaidi kuwaandikisha wapiga kura.

Uamuzi huo ulisababisha kuzuka kwa ghasia wakati upinzani ulimlaumu Kabila kwa kujaribu kusalia madarakani.

Maelezo ya picha,

Watu wakiwa foleni kupiga kura mapema leo

Kisha wiki iliyopita uchaguzi ulihairishwa tena, kwa siku saba, kwa sababu za matatizo ya kusafirisha vifaa kwenda vituo vya kupigia kura.

Hii ilikuja baada ya maelfu ya mashine za kupigia kura zinazotumiwa kwa mara ya kwanza nchini humo kuharibiwa kwenye moto katika mji mkuu Kinshasa.

Maelezo ya picha,

Watu wakiwa foleni kupiga kura mapema leo

Nani wanawania urais?

Kuna wagombea 21 lakini watatu ndio wakuu:

  • Emmanuel Ramazani Shadary, Waziri wa zamani wa mambo ya ndani na mtiifu kwa Kabila, ambaye aliwekewa vikwazo na Muungano wa Ulaya kwa hatua zilizochuliwa upinzani wakati wa maandamano ya mwaka 2017.
  • Martin Fayulu, Mkurugenzi mkuu wa zamani wa mafuta ambaye ameahidi nchi yenye mafanikio lakini ambaye watu maskini wanahisi hawezi kuwatetea.
  • Felix Tshisekedi Tshilombo, Mtoto wa mwanasiasa mkongwe ambaye ameahidi kupambana na umaskini.

Habari za hivi punde kabisa ni zipi?

Wagombea watatu wanaoongoza na maafisa wa uchaguzi walikutana mjini Kinshasa siku ya Jumamosi kusaini makubaliano ya kutowepo jambo lolote baya wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.

Lakini mwisho wake Bw Tshisekedi alitaka kuwepo mabadiliko na kukataa kusaini makubaliano hayo.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Wagombea wa upinzani Martin Fayulu (kushoto) na Felix Tshisekedi (kulia) wanakabiliana na Emmanuel Shadary (kati kati), waziri wa zamani wa mambo ya ndani

Wiki hii, upigaji kura kwenye wilaya tatu ulihairishwa hadi Machi huku tume ya uchaguzi ikisema ukosefu wa usalama na ugonjwa wa Ebola ndivyo sababu.

Kutokana na hilo karibu watu milioni 1.2 hawatapiga kura leo Jumapili.

Umati ulivamia zahanati inayoshughulikia ugonjwa wa Ebola mashariki mwa nchi baada ya tangazo hilo kutolewa.

Zaidi kuhusu DR Congo

Nchi hiyo kubwa ya Afrika ya kati ina utajiri wa madini na ndiyo mzalishaji mkubwa wa madini ya cobalt, yanayotumiwa kwa simu na betri za magari.

Lakini ina viwango vya juu vya umaskini, miundo msingi duni na wanasiasa na wafanyabiashara wanalaumiwa kwa kujitajirisha huku wengine wengi wakibaki kuwa maskini.

Imekuwa kwenye hali ambayo waangalizi wengine wanataja kuwa vita vya dunia vya Afrika kati ya mwaka 1997 na 2003.