New Horizons: Chombo cha NASA kuweka historia uchunguzi wa anga za juu

Artwork: New Horizons karibu na Ultima Thule

Chanzo cha picha, NASA/JHU-APL/SWRI

Maelezo ya picha,

Picha iliochorwa: Kufikia sasa wanasayansi wanaweza kubahatisha umbo la Ultima Thule

Amri za mwisho kabla ya tukio la kihistoria kwa chombo cha Nasa kwa jina la New Horizons zimetumwa katika chombo hicho.

Kupita kwa chombo hicho karibu na kitu chenye upana wa kilomita 30 kwa jina Thule Ultima kutaweka rekodi mpya kwa uchunguzi uliofanyiwa mfumo wa sayari iliopo umbali wa kilomita bilioini 6.5 kutoka duniani.

Upakiaji ulijumuisha marekebisho ya pili ambayo yanahakikisha kwamba chombo hicho cha New Horizons kinajua ni muda gani na saa ngapi kuelekeza kamera zake inapolenga kwa kasi ya kilomita 14 kwa sekunde.

''Ndege hiyo haina tashwishi yoyote na tunafurahi!'' alisema meneja wa operesheni hiyo Alice Bowman wakati alipozungumza na wanahabari katika kituo cha udhibiti wake kilichopo katika chuo kikuu cha Fizikia mjini Maryland.

Chombo cha New Horizons kinatarajiwa kuruka urefu wa kilomita 3,500 juu ya sakafu ya Ultima, huku kikitarajiwa kuwa karibu na Ultima mwendo wa saa mbili na dakika 33 muda wa Afrika mashariki.

Kimetengezwa kuchukua picha nyingi za kiwango cha gigabyte pamoja na data nyengine ya kisayansi saa chache kabla na baada ya tukio hilo.

Ultima ni katika kile kinachoitwa Ukanda wa Kuiper ambapo ni bendi yenye nyenzo iliohifadhiwa inayozunguka jua zaidi ya sayari ya nane ya kale kwa jina Neptune.

Na Ultima iko mbali zaidi ya sayari ndogo zaidi ya Pluto ambayo ilitembelewa na chombo cha New Horizons 2015.

Inakadiriwa kwamba kuna mamia ya maelfu ya wanachama wa Kuiper kama vile Ultima, na mshikamano wake unatoa dalili za umbo la mfumo mzima wa sayari yapata miaka bilioni 4.6 iliopita.

Chombo cha New Horizons kimekuwa kikipiga mamia ya picha katika timbo yake kikikaribia. Na ijapoikuwa Ultima inaonekana kuwa ndogo katika picha hizo habari wanazopata ni muhimu katika kusaidia ujumbe huo kubaini njia zitakazotumika kuelekeza vitu hivyo viwili kukutana.

Hatahivyo kimezua kitendawili kwamba , mwangaza unaotoka katika kitu hicho hauonyeshi chochote zaidi kwa chombo kinachotarajiwa kuwa na sura isio ya kawaida na kinachozunguka.

Maelezo kadhaa kuhusu ukosefu wa tofauti iliopo katika "mkondo wa mwanga" yamependekezwa. Moja inaweza tu kuwa jiometri ya pembe ya kutazama; nyengine ni kwamba Ultima huenda ni vitu viwili au zaidi vinavyozunguka karibu.

Uwezekano huu wa mwisho umekuwa suala la uvumi.

Kwa nini chombo cha New Horizons kinaelekea karibu na Ultima Thule?

Nasa ilitaka kuonyesha kwamba kitu chochote kilicho zaidi ya umbali wa sayari ya Pluto kinaweza kufikiwa

Cha kushangaza ni kwamba kiligunduliwa miaka minne ilioipita na darubini ya Hubble.

Awali kilijulikana kama (486958) 2014 MU69, ilipatiwa jina zuri la Ultima Thule (ikitamkwa: Tool-ee) baada ya majadiliano

''Ni jina la Latin linalomaanisha eneo lililopo katika ulimwengu usiojulikana.".

Kama vitu vingine vilivyopo katika ukanda wa Kuiper, ni eneo linaloweza kuwa na barafu nyingi , vumbi na pengine vipande vikubwa vya miamba ambavyo vilikusanyika pamoja wakati wa mfumo wa jua.

Nadharia inaonyesha kwamba vitu hivyo huenda vinafanana na ''viazi ama njugu''.

Picha zilizonaswa na darubini zinaonyesha kuwa sakafu yake ni nyeusi tititi ikiwa na wekundu mchache. Giza hilo linatokana na joto linalosababishwa na miale mikali ya kawi.

Chombo cha New Horizons kitatoa ufichuzi kuhusu umbo la Ultima, mzunguko wake, eneo iliopo na mazingira yake. Wanasayansi wanataka kujua ni vipi dunia hizi zilizopo mbali ziliundwa.

Wazo moja ni kwamba zilitokana na kuongezeka kwa vipande vingi vidogo vidogo.

Je tutarajie nini kutoka tukio hilo la kihistoria?

Usifumbe jicho, unaweza kukosa uhondo. Ikilinganishwa na safari ya Pluto, Julai 2015 , hakutakuwa na picha za kuvutia wakati wa kukaribia Ultima.

Ultima haitaonekana vizuri hadi New Horizon itakapokaribia. Hatahivyo wakati New Horizon itakapokaribia maelezo sahihi katika sakafu yake yataonekana.

Vitu vilivyo na ukubwa wa hadi mita 33 vitaonekana iwapo kamera za horizons zitalenga.

Kwa kuwa Horizons italazamika kugeuka ili kuweza kulenga eneo inalotaka kuchukua picha, inaweza kuweka antena zake duniani huku ikichukua data.

Chanzo cha picha, NASA / JHUAPL / SWRI

Maelezo ya picha,

Maelezo ya picha hii yanatarajiwa kuwa mazuri zaidi ya wakati New Horizons ilipotembelea Pluto.

Je tukio hilo linakabiliwa na changamoto za kiwango gani?

Kwa upande mwengine tukio hilo ni gumu zaidi ya kupita kwa Pluto.

Kituo kinachoonekana katika kamera ni kidogo mara 100 katika jicho la kamera. New Horizons itawasili karibu sana zaidi ya Pluto, ikiwa ni habari njema kwa picha zinazoonekena vizuri: lakini hali hiyo pia inamaanisha kwamba uchunguzi huo unaweza kutuma picha za anga isio na kitu!

Na huo ndio wasiwasi mkubwa , kwa kuwa Ultima iligunduliwa miaka minne , eneo ililopo na mwenendo wake haujulikani ikilinganishwa na Pluto.

Kumbuka kwamba yote haya yanafanyika umbali wa kilomita bilioni 6.6 kutoka duniani.

Umbali huo unafanya ishara za mawimbi ya redio kuchukua saa sita na dakika nane ili kuwasili.