Hezron Mogambi: Wakati umefika Rais Kenyatta atawapiga shoka mawaziri wake wazembe karibuni?

Rais Kenyatta Haki miliki ya picha Uhuru Kenyatta / Facebook
Image caption Kenyatta amekuwa akiwakosoa mawaziri wake hadharani

Rais Uhuru Kenyatta aliwapa mawaziri wake likizo ya Krisimasi huku kukiwa na uvumi na ukisiaji kuhusu kuwepo kwa mabadiliko katika baraza la mawaziri ukiendelea kukua mwingi.

Imeanza kuaminika sasa kuwa likizo hii ambayo Rais ameitoa inaweza kuwa likizo kabla ya mabadiliko katika baraza la mawaziri.

Fununu hizi zinatoka na ukweli kwamba katika siku za hivi karibuni, Rais Kenyatta amekuwa akiwazomea na kuwakaripia mawaziri wake hadharani na kuwataja kwa majina kuhusiana na utendakazi wao katika wizara mbali mbali.

Aidha, ripoti na uvumi kuhusu mabadiliko katika baraza la mawaziri nchini Kenya umekuwepo kwa muda mrefu sasa huku ikiaminika kuwa baadhi ya mawaziri hawamsaidii katika kufikia ajenda zake kuu nne na jinsi atakavyokumbukwa ikikumbukwa kwamba hiki ni kipindi chake cha mwisho uongozini.

Rais Kenyatta amekuwa akiwaonya mawaziri wake kuwa hataweza kuvumilia uvivu katika utendakazi wao.

Zaidi inasemekana kuwa Rais Kenyatta amekuwa akiwakaripia mawaziri hao kwenye mikutano naye jambo ambalo limewafanya baadhi yao kuogopa kupokea simu kutoka kwa Rais.

Mtindo huu mpya wa kuwakaripia mawaziri wake kisiri na hadharani ili kuhakikisha kuwa ajenda zake uongozini zinafikiwa umewafanya wengi kubaki na maswali mengi kuhusu hatima ya mawaziri waliopo.

Baadhi ya mawaziri ambao wamekaripiwa hadharani siku za hivi karibuni ni pamoja na Waziri wa michezo, utamaduni na turathi Mohamed Echesa, Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri, waziri wa fedha Henry Rotich na Waziri wa Afya Sicily Kariuki.

Rais Kenyatta pia alilifokea baraza zima la mawaziri wakati alipozindua kikosi maalum cha kulinda pwani ya Kenya maarufu Kenya Coast Guard akieleza kuwa hata hilo lilikuwa wazo lake pamoja na mkuu wa majeshi ya Kenya Jenerali Samson Mwathethe akihofia kuwa mawaziri wake wangependa kuibia umma.

Inasemekana kuwa vita dhidi ya ufisadi, utendakazi mbaya, uhusiano wa karibu kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, ukosefu wa uzito wa kisiasa na haja ya kuweza kuwa na uwakilishi na maeneo mbali mbali katika baraza la mawaziri ni masuala muhimu yatakayosukuma kutokea mabadiliko katika baraza la mawaziri ambalo huenda likawaathiri mawaziri kumi.

Ripoti nyingine zaeleza kuwa kundi maalum ambalo limekuwa likielekeza vita dhidi ya ufisadi ambalo linaongozwa na mwanasheria mkuu wa Kenya, Paul Kihara limekamilisha ripoti yake kuwahusu mawaziri na kumpa Rais ripoti yao.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais Kenyatta alikutana na kumaliza uhasama na Raila Odinga Machi mwaka jana

Kundi hili linawaleta pamoja majasusi, mkurugenzi wa idara ya ujasusi wa jinai, kiteno cha kufunga akaunti kutokana na makosa ya biashara haramu ya pesa, kitengo cha kuzuia mali yaliyoptikana kwa njia zisizo halali, kituo cha masuala ya fedha,Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) vyote ambavyo vinaripoti moja kwa moja kwa Rais Kenyatta.

Haieleweki iwapo Rais Kenyatta atatumia ripoti hiyo pamoja na ripoti nyingine za utendakazi katika kuwatimua mawaziri ambao wameshindwa katika utekelezaji wa ajenda zake au la.

Sakata ya mahindi

Hakuna waziri hata mmoja ambaye amehusishwa katika ufisadi ingawa wizara mbali mbali zimekuwa zikichunguzwa, kutajwa na kushukiwa. Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri amekuwa akikumbwa na shutuma nyingi kutokana na malipo kwa wakulima wa mahindi ambapo ilisemekena kuwa, kwa muda mrefu, wakulima halali walikuwa hawajalipwa huku wanabisahara walaghai wakilipwa kwanza.

Mnamo mwezi wa Mei mwaka huu, Waziri wa kilimo Mwangi Kiunjuri alikubali kuwa huenda serikali ilipoteza mabilioni katika malipo kupitia kwa bodi ya nafaka nchini Kenya (NCPB) baada ya madai kutoka kwa wakulima ambao hawakuwa wamelipwa.

Waziri Kiunjuri amewahi kukaripiwa na Rais Kenyatta hadharani kwa kile Rais Kenyatta alichokiita utepetevu kazini. Akionge katika maonyesho ya kimataifa ya Nairobi, Rais Kenyatta alimkashifu waziri huyu kwa kukosa kuhakikisha kuwa wakulima wa mahindi walikuwa wamelipwa. Akiongeka kwa lugha yake ya mama, Rais Kenyatta alimwambia waziri Kiunjuri kuwa iwapo hangehakikisha kuwa wakulima wanaofaa walikuwa wamelipwa, angekiona.

"Mungiriha nimukuona," ambayo inatafsiriwa kuwa, "Iwapo mtalipa, mtakiona."

Katika sakata ya mahindi, ambayo imewafanya maafisa wakuu katika bodi ya mazao na mahindi kufikishwa mahakamani, waigizaji wa mahindi kutoka ngambo walilipwa mamilioni ya pesa kwa mahindi yao huku wakulima wengi wa kawaida wakiachwa nje.

Waziri wa fedha, Henry Rotich na mwenzake wa masuala ya Afrika Mashariki Adan Mohamed (waziri wa bishara hapo awali) wameonyeshewa lawama na kamati ya bunge iliyokuwa ikichunguza uingizaji wa sukari iliyokuwa na sumu humu nchini.

Huku waziri Rotich akinyoshewa kidole kwa kuingizwa kwa sukari nchini Kenya kupitia kwa notisi katika gazeti la serikali aliyotoa, kamati ilipendekeza kuwa waziri Mohamed ajibu kwa makosa ya taasisi ya ubora wa bidhaa katika ukaguzi wa sukari kutoka nje ya nchi ya Kenya.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Waziri Henry Rotich wakati wa kusomwa kwa bajeti

Matatizo wizara ya afya

Mwezi wa Aprili, Rais Kenyatta alimshutua waziri wa Afya CS Sicily Kariuki wakati alipomwambia hadharani kuhakikisha kuwa amejenga hospitali za kisasa katika mwaka mmoja. Huku akiifungua hospitali ya Tenwek katika kaunti ya Bomet, Rais Kenyatta alionekana kutambua urasimu katika ununuaji bidhaa na huduma serikalini.

Hospitali ya macho na meno ya Tenwek, ambayo itagharimu Sh300 milioni na iliyo na uwezo wa kuwahudumia wagonjwa 20,000 na kufanya upasuaji kwa wagonjwa 5,000 kila mwaka, kulimfurahisha Rais Kenyatta kiasi cha kuuliza ni kwa nini hali kama hiyo haingeweza kupatikana katika hospitali za serikali.

Ndipo Rais alipomwambia waziri wa afya ambaye alikuwepo katika hafla hiyo kuhakikisha kuwa hospitali kama hizo zimejengwa katika miji ya Eldoret, Nyeri, Nairobi na Mombasa kufikia mwaka ujao ama apoteze kazi yake ya uwaziri.

Katika hafla nyingine majuma mawili yaliyopita, Rais Kenyatta alimfokea waziri wa michezo na turathi za kitaifa Mohamed Echesa kwa utepetevu kazini mwakae na kutojua wajibu wake na badala yake akilenga kuhudhuria sherehe za mazishi na kuwatusi viongozi wengine.

"Inaonekana wewe unafikiri kuwa kazi ya waziri ni kuhudhuria sherehe za mazishi kote mgharibi mwa Kenya," Rais anasemekana kumwambia waziri Echesa ambaye alionekana kushangazwa na matashi ya Rais mbele ya kiongozi wa upinzani Kenya Raila Odinga na maafisa wengine wakuu wa serikali nyumbani kwa Jaramogi Oginga Odinga.

"Wewe kazi yako ni kungoja wikiendi ifike halafu unaenda kwa kila matanga kutusi watu. Hiyo sio kazi ya waziri. Hio ni kazi ya wabunge. Ni Kama hujui kazi yako."

RIS Kenyatta alikuwa amekasirishwa na hali ya kaburi la Jaramogi Oginga Odinga haukuwa nzuri kwa kutoshughulikiwa na serikali hata ingawa ni mmojawapo ya mnara wa kitaifa tangu mwaka wa 2005.

Kashfa ya NYS

Kwa upande wake, waziri wa afya Cicily Kariuki alikuwa na wakati mgumu wakati wabunge wa Kenya walipomhoji kuhusiana na kashfa katika wizara yake pamoja na utendakazi wake huku akishtumiwa kwa ujeuri na uongozi wa kiimla kwenye wizara yake.

Wizara yake ilipoteza pesa nyingi kupitia kwa kashfa ya Huduma ya Kitaifa kwa kwa Vijana (NYS) alipokuwa katika wizara hiyo.

Ingawa Kashfa hii imesahaulikwa sasa, imeipaka tope serikali ya Uhuru Kenyatta kiasi cha katibu wa kudumu Lilian Omollo na maafuisa wengine akiwemo afisa mkuu wa NYS Richard Ndubai kushtakiwa mahakamani.

Image caption Ufisadi umekuwa tatizo kubwa Kenya

Bungeni, mswaada dhidi ya waziri wa afya Cicily Kariuki ambao ulikuwa umeasisiwa na Mbunge wa Aldai Cornelly Serem kwa shutuma za kutumia mamlaka vibaya uliondolewa dakika za mwisho hata baada ya wabunge 166 kutia saini kuunga mkono mswada huo.

Mwezi wa Julai mwaka huu, Rais Uhuru Kenyatta aliwabadilisha mawaziri na makatibu miezi sita tu baada ya kuunda baraza lake la mawaziri. Katika wizara wakati waziri Adan Mohammed ambaye hapo awali alikuwa waziri wa Biashara na Viwanda alipohamishwa hadi wizara ya Masuala ya Afrika Mashariki na kubalishana nafasi na waziri Peter Munya ambaye sasa amechukua nafasi ya Bwana Aden Mohamed kama waziri wa Biashara na Viwanda.

Makatibu waliohusishwa katika mabadiliko hayo madogo ni pamoja na Coletta Suda (elimu) na Simon Kachapin (Nishati). Nelson Marwa(Ugatuzi) alihamishiwa wizara ya Leba ambapo atashughulikia masuala ya wakongwe huku aliyekuwa katibu wa michezo Joe Okudo akihamishiwa utalii naye . Fatuma Hirsi akihamia wizara ya teknohama kama katibu wa kudumu.

Makatibu wnegine waliohusishwa walikuwa Francis Owino (Wizara ya vijana, na masuala ya jinsia), Bi Esther Koimett (Uchukuzi na muundo mbinu) na Paul Mwangi Maringa.

Je, wakati umefika wa Rais Kenyatta kufanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri ili kufikia ajenda zake?

Prof Mogambi, ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi: hmogambi@yahoo.co.uk

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii