Hamornize atengana na meneja wake Mr. Puaz

Msanii Hamornize kulia na meneja wake Mr. Puaz Haki miliki ya picha Mr. Puaz

Mmoja wa mameneja hodari wa muziki nchini Tanzania Joel Vincent ambaye anajulikana kwa jina maarufu kama Mr. Puaz ametengana na kundi la muziki la Wasafi au WCB baada ya kukosana na mteja wake msanii Harmonize.

Kulingana na meneja huyo wawili hao - Harmonize na Mr. Puaz -wameamua kutengana kutokana na kile alichokitaja kuwa ni ukosefu wa maelewano katika biashara hiyo.

Mr Puaz ambaye alizungumza na BBCSwahili kwa njia ya simu amesema kuwa Mwanamuziki Harmonize amekuwa akimdharau na kupuuza ushauri wake.

''Niliketi chini na Diamond Platinumz na kumuelezea yaliojiri na tukakubaliana kwamba sitaendelea kusimamia tena muziki wa Harmonize''. alisema Mr Puaz.

Ameongezea kwamba msanii huyo amejawa na ''kiburi'' tangu aanze kupata mafanikio ya kimuziki .

''Naelewa kwamba ni kijana mdogo ambaye ametoka katika familia masikini, lakini utajiri na umaarufu aliopata kutokana na mafanikio ya muziki wake umeathiri tabia yake''.

''Inawezekana kwamba huenda pia mimi nina mapungufu yangu lakini yote haya ilikuwa kujaribu kumuuza yeye katika muziki'', aliongezea Mr. Puaz.

Haki miliki ya picha Mr. Puaz
Image caption Msanii wa muziki wa bongo fleva kutoka Tanzania Harmonize na meneja wake Joel Vincent aka Mr. Puaz kabla ya wawili hao kuachana

Meneja huyo ambaye amehusika pakubwa katika wimbo wa 'Kwangwaru' uliotia fora katika jumuiya ya Afrika mashariki na kumpandisha hadhi Harmonize kuwa mmojwapo wa wanamuziki bora Afrika anasema kwamba mara ya mwisho kushirikiana na msanii huyo ni wakati wa Tamasha la Wasafi lililofanyika mjini Diani nchini Kenya tarehe nane mwezi Disemba mwaa uliopita.

''Baada ya tamasha hilo nilirudi Tanzania na kumuelezea Diamond kwamba mimi siwezi tena kufanya kazi na Harmonize na kiongozi huyo wa WCB akaheshimu uamuzi wangu'', alisema.

Mr Puaz hakuonekana katika Tamasha la Wasafi lililofanyika Mombasa na lile lililofanyika katika ukumbi wa Uhuru Gardens jini Nairobi kuaga mwaka uliopita.

Awali Bwana Puaz alimsimamia mwanamuziki wa mtindo wa Rap nchini Tanzania Shetta kabla ya kujiunga na Wasafi ambapo alisaidia katika kumsajili Harmonize kama msanii wa kwanza chini ya WCB.

Akishirikiana na Harmonize kama maneja wake Mr Puaz alihusika katika kuuza nyimbo kama vile DM Chick akimuhusisha msanii Sarkodie, Khadamshi ulioimbwa na Duly Syke, Nitarudi mbali na Kwangwaru uliogonga vichwa vya habari.

Juhudi zetu za kuwatafuta wasimamizi wa WCB pamoja na msanii Hamornize kwa njia ya simu ziliambulia patupu.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii