Ghana: Baadhi ya vijana wa kiislamu wamvamia mchungaji mmoja aliyetabiri kifo cha Imamu

mchungaji Haki miliki ya picha GLORIOUS WORD POWER MINISTRIES/FACE
Image caption Mchungaji Isaac Owusu-Bempah ni miongoni mwa wahubiri maarufu wa injili nchini Ghana

Vijana wa kiislamu wenye hasira kali walivamia kanisa moja katika mji mkuu wa Ghana, mara baada ya mchungaji kutabiri kifo cha Imamu Mkuu wa kiislamu wa nchini humo kutokea mwaka 2019.

Baadhi ya vitu viliharibiwa kama madirisha na viti, baada ya vijana hao kulivamia kanisa la mchungaji Isaac Owusu-Bempah lililopo Accra.

Imamu mkuu Nuhu Sharabutu amekemea uvamizi huo.

Manabii wa kikristo wamekuwa na wafuasi wengi barani Afrika na mara nyingi huwa wanatabiri matukio kadhaa makubwa ambayo yanaweza kutokea ikiwa ni pamoja na vifo vya watu maarufu.

Mwaka 2006, Mhubiri maarufu barani Afrika , TB Joshua kutoka nchini Nigeria alitabiri kuwa Hillary Clinton atamshinda Donald Trump katika uchaguzi wa urais nchini Marekani.

Trump aliposhinda uchaguzi , alikosolewa vikali kwa utabiri wake ambao uliondolewa katika kurasa yake ya Facebook.

Tarehe 31,Desemba, Mchungaji Owusu-Bempah alitabiri mambo 18 ambayo yatatokea mwaka 2019, na miongoni mwa hayo ni kifo cha Imamu wa Ghana ambaye pia makamu wa rais wa Kiislamu Mahamudu Bawumia kikiwa miongoni.

Baadhi ya vijana wa kiislamu walimtaka mchungaji huyo kumuomba radhi imamu Sharabutu, lakini hakufanya hivyo.

' Mchungaji asamehewe'

Siku ya Jumatano, kikundi cha vijana wenye silaha kililizunguka kanisa la 'Glorious Word and Power Ministry'.

Kikundi hicho kiliweka shambulizi hilo katika mtandao wa kijamii wa Facebook, na kuonyesha namna walivyokuwa wakifanya vurugu za kuharibu vitu vilivyopo kanisani pamoja na kurarua picha ya mchungaji Owusu-Bempa.

Imamu Sharabutu aliwataka watulie na kusema kuwa, watu wote ambao wana hasira na utabiri wa mchungaji huyo wanapaswa kumsamehe kiongozi huyo maarufu wa makanisa ya kiinjili nchini Ghana.

Ghana ni nchi ambayo ina wakristo wengi huku ikiwa haina historia ya migogoro ya kidini.

Baada ya uvamizi huo wa kanisa la the 'Glorious Word and Power Ministry' lilisema "wakristo wanapaswa kuwa wajasiri na kuliombea kanisa".

Haki miliki ya picha Getty Images

Kwa nini wachungaji wanafanya utabiri

Kama ilivyo kwenye maeneo mengine ya bara la Afrika, makanisa yamegeuka kuwa biashara kubwa nchini Ghana.

Njia ambazo wahubiri wanazitumia kwa waumini wao makanisani ni kutabiri kile ambacho kinaweza kutokea mwisho wa dunia.

Licha ya kuwa baadhi ya wakristo nchini Ghana wamekuwa wakiwakosoa vikali lakini wahubiri hawa wameendelea kupata wafuasi wengi zaidi na wengi wao wakiwa ni watu ambao hawana elimu, watu wanaoacha kufanya kazi wiki nzima kwa ajili ya kuhudhuria maombi ya muda mrefu ili kuzuia vifo vyao.

Wanasiasa, wacheza filamu na wafanyabiashara huwa wanahudhuria mahubiri ya wahubiri maarufu kwa ajili ya kujilinda kiroho na kuongeza utajiri.

Wakati ambapo utabiri wa kifo unaposhindwa kutokea , wahubiri usema kuwa sala zao zimemsaidia mtu huyo kuokoa maisha yake.

Na wakati ambapo watu maarufu wanapokufa, video na picha kutoka kwa manabii mbalimbali usambaa na kudai kuwa Mungu alitoa ishara ya kifo cha mtu huyo kwao.

Manabii hao mara nyingi hubainika kuwa waongo , lakini wanatumia vyombo vya habari kusisitiza na kuongeza nafasi yao ya kuwa wahubiri maarufu.

Na kuendelea kuongeza idadi ya watu zaidi na zaidi ambao wana matumaini ya mafanikio ya kifedha au kupona magonjwa jambo ambalo limeathiri maisha ya watu wengi.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii